Na Allan Kitwe, JamhuriMedia, Tabora

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoani Tabora imeokoa zaidi ya sh bil 3za miradi ya ujenzi wa stendi kuu ya mabasi na soko la kisasa katika halmashauri ya manispaa Tabora zilizotaka kuibiwa na watu wasio waaminifu hata kabla ya kuanza utekelezaji miradi hiyo.

Hayo yamebainishwa jana na Mkuu wa Taasisi hiyo Mkoani hapa Abnery Mganga alipokuwa akitoa taarifa ya utekelezaji majukumu ya Taasisi katika kipindi cha miezi mitatu ya Aprili-Juni 2024 mbele ya vyombo mbalimbali vya habari.

Amesema kuwa wamebaini ubadhirifu huo uliotaka kufanyika kwenye mchakato wa zabuni ya kumpata mkandarasi atakaye tekeleza miradi hiyo yenye thamani ya zaidi ya sh bil 16 mjini hapa.

Amefafanua kuwa kama ilivyo ada kwa taasisi hiyo kuifanyia uchunguzi miradi yote inayotekelezwa na serikali kabla na baada ya kutekelezwa, walibaini kuwa kuna watu wanataka kuhujumu zabuni ya mradi huo ili kujipatia kiasi hicho cha fedha.

Mganga ameongeza kuwa miradi hiyo miwili ambayo itatakelezwa na mkandarasi mmoja kwa gharama ya zaidi ya sh bil 16 lakini wakati wa mchakato wa kumpata mzabuni wakafanya ujanja ili walipwe kiasi hicho.

Baada ya uchunguzi wa mchakato huo na kubaini mianya ya rushwa na ubadhirifu, waliamua kuzuia fedha hizo zisilipwe na sana wanaendelea na uchunguzi zaidi ili kubaini waliotaka kufanya ubadhirifu huo ili mkondo wa sheria utachukua nafasi yake.

‘Hatutakubali vitendo vya rushwa au ubadhirifu wa aina yoyote ile kwenye fedha za maendeleo, fedha yoyote itakayotolewa na serikali kwa ajili ya miradi ya wananchi tutaifuatilia mwanzo hadi mwisho’, amesema.

Amesistiza kuwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa haitasita kumchukulia hatua mtu au Ofisa yeyote atakayebainika kutumia vibaya fedha hizo au kuhusika kwa namna moja ama nyingine ikiwemo ukiukwaji wa sheria, kanuni na taratibu za manunuzi.

Mganga amefafanua mkakati wa Taasisi hiyo kuwa ni kuzuia zaidi vitendo hivyo na kutoa elimu kwa jamii juu ya madhara yatokanayo na rushwa, ubadhirifu na vitendo vingine vinavyofanana na hivyo.

Amebainisha kuwa kuzuia vitendo hivyo ni bora zaidi kwa kuwa gharama za kuendesha kesi ni kubwa, hivyo ni muhimu sana kwa jamii kutoa taarifa mapema ili kuzuia mianya ya kutoa au kupokea rushwa .

Aidha amewataka wananchi wote kuendelea kutoa ushirikiano kwa Taasisi hiyo kwa kutoa taarifa za vitendo hivyo ili kufanikisha juhudi za kupambana na kudhibiti vitendo vya rushwa.

Please follow and like us:
Pin Share