Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Mkoa wa Temeke imesimamisha ujenzi wa kituo cha mafuta uliokuwa unaendelea katika kiwanja namba P.18435 eneo la Mbagala Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam.
Hayo yamejiri leo jijini wakati Kaimu Mkuu wa TAKUKURU Manispaa ya Temeke, Euginius Hazina mwisho akizungumza na waandishi wa habari kuhusu programu ya TAKUKURU ya kutatua kero ya ujenzi wa kituo cha mafuta kilichojengwa kinyume na utaratibu
Kaimu huyo ameeleza kuwa uchunguzi wa kina kuhusu kutolewa kwa kibali hiko cha ujenzi ulibaini kwamba wapo baadhi ya watumishi wachache wasio waadalifu wa Wizara ya Ardhi walikula njama na kufanikisha upitishaji wa kibali cha ujenzi kinyume na sheria.
Pia, Hazina mwisho amesema wanaendelea kukamilisha uchunguzi ili wote waliohusika waweze kufikishwa mahakamani kwa makosa ya kughushi, kula njama na matumizi mabaya ya ofisi.
“Tunaendelea kukamilisha uchunguzi ili wote waliohusika waweze kufikishwa mahakamani kwa makosa ya kughushi,kula njama na matumizi mabaya ya ofisi kinyume cha kifungu namba 31na 32 PCCA,2007 vikisomwa pamoja na sheria ya uhujumu uchumi sura ya 200,” amesema Hazina mwisho.
Amesema wameendelea kupokea taarifa zinazoonesha vipo vibali vingine maeneo mbalimbali nchini vilivyotolewa kinyume cha sheria, hivyo uchunguzi huo utakuwa endelevu ili kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza kutokana na ujenzi huo holela wa vituo vya mafuta
Pia, ametoa rai kwa wafanyabiashara wenye nia ya kuwekeza kwenye vituo vya mafuta katika Mkoa wa kitakukuru wa Temeke, kabla ya kuanza mchakato waombe vibali vya ujenzi ili wajiridhishe na matakwa ya sheria za mipango miji sura ya 355 na kanuni zake za 2018.