Na Allan Kitwe, JamhuriMedia, Tabora
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoani Tabora imetembelea na kukagua jumla ya miradi 11 ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya sh bil 28 na kubaini dosari katika utekelezaji baadhi ya miradi hiyo.
Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari jana Mkuu wa Taasisi hiyo Mkoani hapa Abnery Mganga amesema kuwa taasisi hiyo imebaini mapungufu katika miradi 8 kati ya 11 iliyochunguzwa kutokana na dosari mbalimbali za kiutekelezaji.
Ameeleza kuwa miradi hiyo yenye thamani ya zaidi ya sh bil 27 iliyotekelezwa katika Wilaya zote za Mkoa huo ni ya ujenzi wa shule (vyumba vya madarasa) katika shule za msingi na sekondari kupitia mradi wa SEQUIP na BOOST.
‘Naipongeza serikali kwa kuendelea kuleta fedha nyingi za utekelezaji miradi ya maendeleo katika sekta mbalimbali, ni jukumu la taasisi hii kuhakikisha fedha zote zinazoletwa na Mheshimiwa Rais zinatumika vizuri na si vinginevyo’, amesema.
‘Tumebaini dosari nyingi katika miradi hii ikiwemo kutumika vifaa visivyo na ubora ambapo tumeagiza kusitishwa mara moja kwa kazi iliyokuwa ikifanyika na kuelekeza wahusika wakafanye uthibitisho wa vifaa hivyo,’ amebainisha.
Ametaja dosari nyingine kuwa ni mafundi waliopewa kazi hiyo kutokuwa na uwezo, kukosekana elimu ya mfumo wa NEST hivyo mafundi (local fundi) kushindwa kuomba kazi hiyo kwenye mfumo na baadhi ya shule kujengwa katika maeneo yasiyo na huduma za kijamii.
Mganga amebainisha hatua zilizochukuliwa kuwa ni kuelekeza Mamlaka ya Manunuzi ya Umma (PPRA) kuandaa semina maalumu kwa ajili ya mafundi (local fundi) na wazabuni ili waelimishwe namna ya kutumia mfumo huo.
Ametaja maelekezo mengine kuwa ni kusitishwa mikataba ya mafundi wote walioshindwa kutekeleza kazi zao ndani ya wakati na kutafutwa wengine wenye uwezo wa kutekeleza kazi hizo.
Aidha amezitaka Halmashauri ambazo miradi yao imetekelezwa katika maeneo yasiyo na huduma za kijamii kuongeza fedha za kupeleka huduma hizo ili kutokuathiri gharama zilizotengwa kwa ajili ya utekelezaji miradi hiyo na waandaaji wa BOQ kuandaa bajeti inayoakisi uhalisia wa mahitaji ya eneo husika.