Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Mtwara

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Mtwara imefanikiwa kuokoa zaidi ya Sh milioni 31 fedha za viuatilifu katika msimu wa kilimo mwaka 2024/2025.

Akizungumza jana mkoani Mtwara, Naibu Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Mtwara Jumbe Makoba alipotoa taarifa hiyo kwa waandishi wa habari mkoani humo amesema tukio hilo limefanyika katika kijiji cha Chinyanyira kata ya Sengenya iliyopo wilayani Nanyumbu mkoani humo.

Alisema, kipindi cha kuanzia Julai hadi Septemba 2024 taasisi hiyo kupitia program ya Takukuru Ilitatua kero ya wakulima wa zao la korosho ambapo Chama cha Msingi cha Mgulura (Amcos) kiligawa kiuatilifu aina ya sulfa kwa wakulima kwa kuwazidishia baadhi ya wakulima viuatulifu hivyo kwa wasiyokuwa na mikorosho.

“Katika ufuatiliaji wa kero ya hiyo kwa wahusika hadi Julai 18, 2024 jumla ya mifuko 604 yenye thamani hiyo ya fedha ilirejeshwa na kuingiziwa kwenye mfumo wa kugaiwa tena kwa wakulima waliyokosa,”alisema Jumbe.

Aidha kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024, taasisi hiyo inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo taasisi za umma, asasi za kiraia na zisizo na kiraia.

Pia viongozi wa dini pamoja wa waandishi wa habari na wananchi kwa ujumla kwa kutoa elimu inayohusu namna ya kudhibiti rushwa katika uchaguzi huo pamoja na uchaguzi mkuu wa mwakani (2025).

“Kuwaeleza ubaya wa vitendo vya rushwa na athari zake iwapo watawachagua viongozi wa ngazi mbalimbali wanaotoa rushwa, nitoe wito kwa wananchi na wadau wakiwemo wanahabari kila mmoja kwa nafasi yake kushiriki katika kuzuia vitendo vya rushwa katika uchaguzi”alisisitiza.