Na Andrew Peter, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Madai na shutuma za waamuzi kuhongwa ni moja ya mambo ya kawaida kuyasikia kila siku katika Ligi Kuu Tanzania Bara, lakini hadi sasa Takukuru haijafanya lolote kuwakamata wahusika.
Waamuzi wanalaumiwa kwa kufanya upendeleo na kuzibeba baadhi ya timu kwa maslahi yao jambo linalochangia kuitia doa ligi kwa kutengeneza washindi wasiotahiri katika michezo mbalimbali.
Miaka yote tumeona waamuzi wakifanya makosa katika uchezeshaji wao na TFF kwa kushirikiana na kamati zake wamekuwa wakitoa adhabu mbalimbali kama kuwasimamisha, kupewa onyo na kuwaondoa kabisa kutokana na kuchezesha vibaya mechi za ligi.
Ipo wazi na inajulikana hivyo kuwa mpira ni mchezo wa makosa hakuwezi kupatikana bao pasipo kuwa na kosa la wachezaji au waamuzi ndiyo maana wenzetu waliondelea wamekuja na teknolojia ya mstari wa goli pamoja VAR yote ikiwa na lengo la kupunguza makosa ya waamuzi.
Waamuzi wanapokuwa na makosa mengi ya uchezeshaji wanapochezesha timu kubwa ni wazi kunazua sintofahamu na kutegeneza mazingira ya kuonekana kuna upangaji wa matokeo wa mechi nyingi.
Makosa ya waamuzi yamekuwa mengi kiasi hatujui kama tatizo ni rushwa au uwezo wao ni mdogo wa kutafisiri sheria za mchezo jambo linalowafanya washindwa kutenda haki uwanjani.

Chama cha waamuzi (TAFCA) ndiyo inasimamia na kuzaliwa waamuzi hao je wanachangua waamuzi wasiokuwana uwezo kuchezesha ligi, kama ndivyo basi uongozi wa chama hicho unabidi ujitazame upya.
Kanuni inawazuia waamuzi kuzungumza, lakini TAFCA ina wajibu wa kutoka hadharani na kuwatetea wanachama wake na kuondoa hii sintofahamu ya madai ya rushwa, lakini kukaa kwao kimya ni wazi na wao wanaunga mkono kinachoendelea.
Ligi Kuu NBC imefika patamu sasa kuna timu zinataka ubingwa kwa gharama yoyote na zile zinazokwepa janga la kushuka daraja hivyo waamuzi wanapaswa kuwa makini kwani kosa moja linatosha kuipa timu taji au kushuka.
Wakati umefika kwa TFF na TAFCA kuwashirikisha Takukuru katika kumaliza mzizi wa fitna wa rushwa kwa waamuzi hiyo inaweza kuwa dawa kubwa katika kuona mpira wetu unapiga hatua zaidi kwa washindi kupatikana uwanjani.
Kwa sababu rushwa ina mtoaji na mpokeaji kwa kuwa waamuzi ni waathirika wa madai hayo basi wao wanaweza kuwa chanzo kizuri cha kuwakamata hao watoa rushwa na kumaliza kabisa hii kashfa inayowaandama.
Takukuru ina nafasi kubwa ya kumaliza tatizo ya rushwa katika soka, ikiwa itaweka nguvu zake huko kwa lengo la kuboresha mchezo huu.
Mbali ya hiyo tunahitaji kuwa na chombo cha kuchunguza na kujua chanzo cha kuporomoka kwa uwezo waamuzi kwa kufanya hivyo kutasaidia kuboresha uwezo wa kundi hili muhimu katika mchezo wa soka.
Pia, suala la malipo ya waamuzi pamoja na posho zao wanapokuwa katika vituo linabidi liboreshwe kuendana na wakati wa sasa, litasaidia kupunguza wimbi hili.