Mashambulizi ya anga ya Israel kwenye jengo la ghorofa tano la makazi huko Beit Lahia kaskazini mwa Gaza yamesababisha vifo vya takriban watu 34, shirika la ulinzi wa raia la eneo hilo linasema.
Shirika hilo, lililonukuliwa na AFP, lilisema wengi wa waliofariki ni wanawake na watoto, huku makumi ya watu wakihofiwa kuwa chini ya vifusi. Watu saba pia walijeruhiwa.
Jeshi la Israel limesema limekuwa likishambulia maeneo ya wanamgambo kaskazini mwa Gaza, ikiwemo Beit Lahia, katika jaribio la kuwazuia Hamas kujipanga upya.
Kwingineko, katikati mwa Gaza mashambulizi matatu tofauti dhidi ya kambi za wakimbizi yamesababisha vifo vya watu 15, huku wengine watano wakiuawa katika shambulio la ndege zisizo na rubani za Israel huko Rafah kusini, ulinzi wa raia uliongeza.
“Uwezekano wa kuokoa waliojeruhiwa unapungua kwa sababu ya ufyatuaji risasi unaoendelea na mizinga,” msemaji wa ulinzi wa raia Mahmud Bassal alisema.
Kilichosalia kwenye jengo la makazi huko Beit Lahia ni rundo la vifusi, na saruji iliyovunjika na vipande vya chuma vilivyosokotwa vinavyotoka kwenye magofu.
Mwanamume mmoja, ambaye familia yake iliishi katika jengo hilo, lakini alikuwa anakaa mahali pengine, alisema, akinukuliwa na AFP: “Sote tulifikiri kwamba kifo kilikuwa karibu.”
Jeshi la Israel lilisema mashambulizi yake kaskazini mwa Gaza – yaliyoanzia Jabalia na kuzidishwa hadi Beit Lahia – yalihusisha mashambulizi kadhaa usiku kucha kwa kile ilichokiita “lengo la kigaidi katika eneo hilo”.
Iliongeza katika taarifa kwamba “kumekuwa na juhudi za kuendelea kuwaondoa raia kutoka eneo la vita “.