*Dk. Kawambwa aliamua, sasa anamrushia mzigo Dk. Ndalichako
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, ndiye aliyekuwa Mwenyekiti wa Kikao cha magwiji 14 wa elimu kilichobariki utaratibu mpya wa matumizi ya viwango vya ufaulu katika Mitihani ya Taifa ya Kidato cha Nne na Kidato cha Sita, uamuzi ulibadilika na kuonekana kama takataka katika jamii.
Hata hivyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uratibu na Bunge), William Lukuvi, alitoa kauli ya Serikali bungeni kuhusu taarifa ya awali ya Tume ya Taifa ya Kuchunguza Matokeo ya Mtihani wa Taifa Kidato cha nne mwaka 2012 jana, na kuagiza Baraza la Mitihani (NECTA), kupitia upya matokeo hayo.
Kwa mujibu wa nyaraka ambazo JAMHURI imezipata, Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Philipo Mulugo, ndiye aliyekuwa Katibu wa kikao hicho kilichofanyika Katika Ukumbi wa Mikutano wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi (WEMU), Desemba 10, mwaka jana.
Pamoja na viongozi hao wawili, wajumbe wengine walikuwa ni Selestina Gesimba (Kaimu Katibu Mkuu WEMU), Profesa E. P Bhalalusesa (WEMU), Paulina Mkonongo (WEMU), Marystella Wassena (WEMU), Bunyanzu Ntambi (WEMU), Bibi T.E Temu (WEMU), Dk. P.D. Kwera (WEMU), Bi. H. A. Luhawa, (WEMU), Dk. C.E Msonde (NECTA), Profesa Rwekaza Mukandala (Mwenyekiti Bodi ya NECTA), Dk. Joyce Ndalichako (NECTA) na Profesa Sifuni Mchome (TCU).
Kikao hicho ndicho kilichobariki maombi ya Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) ya kutaka kuwapo kwa mabadiliko katika utaratibu wa matumizi ya viwango vya ufaulu katika mitihani. Aidha, matokeo ya kikao hicho ndiyo yaliyomfanya Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Selestine Gesimba, amwandikie barua Katibu Mtendaji wa NECTA, Dk. Ndalichako mnamo Desemba 12, mwaka jana akitaka mabadiliko hayo yaanze mara moja.
Muhtasari unaonyesha kuwa kikao hicho kiliketi saa 8:10 mchana hadi saa 10:20 jioni. Mwenyekiti Dk. Kawambwa alianza kwa kumkaribisha Mwenyekiti wa NECTA, Profesa Mukandala kuwasilisha mapendekezo ya viwango vya ufaulu, na yeye akamkaribisha Katibu Mtendaji wa NECTA, Dk. Ndalichako kuwasilisha mapendekezo hayo kwa niaba ya Bodi.
“Katibu Mtendaji wa NECTA alianza kwa kutoa maelezo kuwa viwango vya ufaulu ambavyo vimekuwa vikitumiwa na NECTA kwa muda mrefu vimekuwa vikibadilika mara kwa mara, hivyo imeonekana haja ya kuwa na viwango maalumu vya ufaulu (fixed grande ranges).
“Katika kutoa mapendekezo ya viwango vipya vya ufaulu, alitaja kuwa viwango vinavyopendekezwa kuwa alama ya chini ni 35 kwa Kidato cha Nne na 40 kwa Kidato cha Sita. Alifafanua kuwa alama hizo zimefikiwa baada ya kupitia viwango vya ufaulu kwa nchi mbalimbali za Afrika zikiwamo Uganda, Congo DRC, Ethiopia, Afrika Kusini, Burundi, Ghana, Nigeria, Gambia, Libya na Siera Leone.
Alifafanua kuwa alama ya chini kwa nchi hizo ilikuwa ni alama 40 na NECTA walipendekeza alama 35 kwa kuzingatia mazingira ya shule nchini,” inasema sehemu ya muhtasari huo ambao JAMHURI imeupata.
Inaonyesha kuwa baada ya Dk. Ndalichako kuwasilisha, wajumbe walitoa maoni kadhaa kuboresha uamuzi huo.
Kwa upande wa matumizi ya alama za maendeleo, wajumbe walitaka kujua ni nini nafasi ya alama hizo katika mtihani wa mwisho wa mwanafunzi. Maelezo yalitolewa kuwa kwa sasa alama za maendeleo zinachangia asilimia 50 ya mtihani wa mwisho wa mwanafunzi isipokuwa kutokana na walimu kukosa uaminifu pamekuwa pakifanyika standardization ili kuepuka kumpa mwanafunzi cheti ambaye hakufaulu katika mtihani wake wa mwisho na utaratibu huo umdekuwa ukitumika kutoka mwaka 1988.
“Kutokana na hali hiyo kwa sasa inapendekezwa kuwa alama za maendeleo zichukue asilimia 30 ya mtihani wa mwisho ili kuepuka kutoa vyeti kwa wasiostahili kupata.
“Kuhusu nafasi ya wakuza mitaala kwenye tathimini ya wanafunzi yalitolewa maelezo kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania ni Mjumbe wa Bodi ya NECTA na anahusishwa kufanya moderation ya mitihani kabla ya kufanyika.
“Vilevile wajumbe walitaka kufahamu kuhusu utaratibu wa standardization na maelezo yaliyotolewa kuwa standardization hufanyika wakati hakuna kiwango alama zinazofanana, hivyo viwango maalumu vitakapokuwepo hakutakuwa na haja ya kufanya standardization.
Ilibainika kuwa alama za maendeleo kutoka ngazi ya shule haziaminiki kwa kuwa wakuu wa shule wengine wanadanganya. Ili kuondoa hali hiyo, ilishauriwa Wizara kufuatilia na kurekebisha kasoro hizo.
Wajumbe walijulishwa kuwa Wizara ilishaanza kulifanyia kazi kwa kupendekeza kuwa Mtihani wa Kidato cha Pili na ‘mock’ mkoa na wilaya utumike kwa ajili ya alama za maendeleo, badala ya mitihani ya shule. Wazo hili lilikubaliwa na wajumbe kwa vile mitihani ndani ya shule kwa ajili ya alama za maendeleo imekuwa haina uhalisia.
Kubadilisha “Subsidiary Pass-S” kuwa Grade kamili
Ilifafanuliwa kuwa alama hiyo (S) huwekwa kwa watahiniwa wa Kidato cha Sita kwa masomo ya nyongoza kama ‘General Studies (GS)’, ‘Basic Applied Mathematics (BAM)’, pamoja na kama alama ya ufaulu wa chini NECTA walilipokea hilo na kuahidi kulifanyika kazi.
Kulinganisha alama za ufaulu za nchi nyingine
Ilifafanuliwa kuwa ulinganisho wa mitaala na mitihani ya nchi nyingine huwa unafanyika. Hata hivyo, ilikubalika kuwa NECTA ifuatilie zaidi. Mwenyekiti aliongeza kuwa uzoefu unaonesha kuwa mitihani ya Tanzania ina kiwango cha juu zaidi ikilinganishwa na nchi nyingine.
Tofauti kubwa ya alama kutoka ‘grade’ moja kwenda nyingine
Ilishauriwa NECTA kupitia upya alama zilizopo ili kupunguza tofauti iliyopo. Mwenyekiti (Dk. Kawambwa) alipendekeza kuwa tofauti ya alama kati ya gredi moja na nyingine isizidi 10 kwa lengo la kupunguza mlundikano (bunching), isipokuwa kwa alama ‘A’ (Kwa mfano Kidato cha Nne, ufaulu A1=80-100; B2=79-70; C3=60-69; D4=50-59; E5=40-49; F6=35-39, na O-34.
Maagizo ya Mwenyekiti
Muhtasari huo unaonyesha kuwa baada ya majadiliano, Mwenyekiti Dk. Kawambwa aliagiza NECTA kutekeleza yafuatayo:
1: Gredi zilizopendekezwa na NECTA zitumike kwa mitihani ya Kidato cha Nne na Kidato cha Sita kwa mitihani ya mwaka 2012/2013.
2: Kurekebisha kiwango cha alama (Grade range) kutoka gredi moja kwenda nyingine ili kurekebisha tofauti kubwa iliyopo (bunching).
3: Kufanya utafiti kuhusu matumizi ya alama za maendeleo katika mitihani, na kupendekeza kwa usahihi mfumo mpya.
4: Kuwa na mtazamo wa mbali kuanzia sasa na baadaye na kurekebisha utofauti kati ya gredi moja na nyingine kwa kuepusha mlundikano wa alama katika gredi moja (bunching).
Muhtasari unaonyesha kuwa Mwenyekiti alifunga kikao saa 10:20 jioni kwa kuwashukuru wajumbe kwa ushirikiano na kuagiza utekelezaji wa maazimio hayo.
KAULI YA SERIKALI BUNGENI KUHUSU TAARIFA YA AWALI YA TUME YA TAIFA YA KUCHUNGUZA MATOKEO YA MTIHANI WA TAIFA WA KIDATO CHA NNE MWAKA 2012
UTANGULIZI
1. Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Kanuni ya 49(1) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la mwaka 2007, naomba kuwasilisha Taarifa ya Awali ya Tume ya Taifa ya kuchunguza matokeo ya Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne mwaka 2012.2.
Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge watakumbuka kuwa Matokeo ya Mitihani ya Kidato cha Nne mwaka 2012 yalionesha kuwa kiwango cha ufaulu kimeshuka kwa kiwango kikubwa ikilinganishwa na miakaya hivi karibuni.
Matokeo yaliyotangazwa mwezi Februari, 2012 yalionesha kwamba kati ya Wanafunzi 367,756 waliofanya mtihani huo, Watahiniwa 126,847 ndio waliofaulu. Katika idadi hii, Wanafunzi waliofaulu katika Daraja la Kwanza hadi la Tatu ni 23,520, sawa na Asilimia 6.4 na Daraja la Nne ni 103,327, sawa na Asilimia 28.1.
Watahiniwa 240,909 , sawa na Asilimia 65.5 ya Wanafunzi wote waliofanya Mtihani wa Kidato cha Nne mwaka 2012 walipata Daraja la Sifuri .
3. Mheshimiwa Spika, kushuka kwa kiwango cha ufaulu kulihusu shule za aina zote, yaani Sekondari za Serikali ikijumuisha zilizojengwa kwa nguvu za Wananchi, Shule Binafsi na Seminari.
Takwimu zinaonyesha kwamba ukilinganisha matokeo ya Kidato cha Nne mwaka 2011 na mwaka 2012, Shule za Wananchi matokeo yao yameshuka kwa asilimia 1.82 ; Shule za Umma za zamani (Kongwe) yameshukwa kwa Asilimia 6.43 ; Shule Binafsi yameshukakwa Asilimia 6.39 ; na kwa Shule za Seminari yameshuka kwa Asilimia 7.29.
Hali hii inaonyesha kwamba, matokeo katika Shule za Wananchi yameshuka kwa kiwango kidogo ikilinganishwa na yale ya Shule za Umma za zamani (Kongwe), Shule Binafsi na Shule za Seminari ambazo zilitegemewa kufanya vizuri zaidi ya zile za Wananchi ambazo matokeo yao yameshuka zaidi kwa kati ya asilimia 6.4 na 7.3.
4. Mheshimiwa Spika, kutokana na matokeo hayo yasiyoridhisha na ambayo yapo nje kabisa ya mwenendo wa ufaulu kwa miaka ya karibuni, Serikali iliamua kuunda Tume ya Kuchunguza Kushuka kwa Kiwango cha Ufaulu wa Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne mwaka 2012 kwa madhumuniya kupata ufumbuzi wa kudumu [kama ifuatavyo;-
5. 1. a) MMEM I ambayo ililenga katika kufungua Shule zaidi ili Wanafunzi wengi wa rika lengwa waweze kujiunga na Elimu yaMsingi;
b) MMEM II ambayo ililenga katika kuboresha ubora wa elimu itolewayo katika Shule za Elimu ya Msingi; na
c) MMEM III ambayo ililenga katika kuendelea kuimarisha ubora wa Elimu ya Msingi baada ya mafanikio ya MMEM I na MMEM II.
5. 2. Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari (MMES) wa mwaka 2004 ambapo:
a) MMES I ambayo ililenga katika kufungua Shule zaidi za Sekondari katika ngazi ya Kata ili Wanafunzi wengi zaidi wanaomaliza Elimu ya Msingi waweze kujiunga na Elimu ya Sekondari Kidato cha Kwanza; na
b) MMES II ambayo ililenga katika kuendelea kuimarisha ubora wa Elimu ya Sekondari kadri Idadi ya Wanafunzi wa Elimu ya Sekondari wanavyoendelea kuongezeka.
Changamoto zinazoambatana na mafanikio haya ni pamoja na mazingira yasiyoridhisha ya kufundishia na kujifunzia, ikiwemo upungufu wa miundombinu muhimu ya shule kama vile madarasa, maabara, madawati, maktaba, nyumba za walimu, hosteli na majengo mengine muhimu ya shule.
Vilevile, kuna tatizo la uhaba wa walimu, vitabu, zana za kufundishia na matatizo ya ukaguzi wa shule. Vilevile, Tume imebaini kuwa mfumo wa elimu ya msingi na sekondari unakabiliwa na changamoto nyingine mbalimbali ambazo taifa linapitia kwa sasa ikiwemo masuala ya kisera, kisheria, kimfumo, kimuundo pamoja na changamoto za uhaba wa rasilimali fedha na rasilimali watu.
Tume inaendelea kufanyia kazi maeneo haya kwa kushirikiana na wataalamu na wadau wengine;
6.2. Kuhusu matokeo ya Kidato cha Nne mwaka 2012, Tume imebaini kwamba, pamoja na wanafunzi hawa kuwa katika mazingira yanayofanana na ya wenzao wa miaka iliyopita na kwamba ufanisi katika shule kwa ujumla umekuwa unashuka kwa sababu mbalimbali, ufaulu wao umeshuka zaidi kwa sababu ya mabadiliko ya mchakato wakuandaa na kutoa matokeo ya mtihani kwa mwaka 2012.
Mfumo uliotumika mwaka 2012 katika kupanga matokeo na madaraja ni tofauti na ule uliotumika mwaka 2011 na miaka iliyotangulia.
Uchunguzi unaonesha kuwa mwaka 2011, Baraza la Taifa la Mitihani lilikuwa linachakata alama za mwisho kwa kutumia mfumo ambao ulikuwa unabadilika kutegemea hali ya ufaulu wa mwanafunzi ambao ni “National Mean Difference” (NMD).
Utaratibu huu ulitokana natofauti ya Wastani wa Kitaifa wa Alama za Maendeleo kutoka Alama za Maendeleo Endelevu ( Continued Assessment – CA ) za watahiniwa wote na wastani wa kitaifa wa ufaulu wa mitihani ya mwisho kwa somo husika.
Kila mtahiniwa aliongezewa “National Mean Difference” iliyokokotolewa katika alama za mtihani wa mwisho ili kupata alama 4 itakayotumika kupata daraja la ufaulu.
Kimsingi, kila somo lilikuwa na NMD yake kulingana na Continued Assessment ( CA) zilivyo kwa mwaka husika. Lakini mwaka 2012 Baraza lilitumia mfumo mpya ambao ulikuwa haubadiliki kutegemea hali ya ufaulu wa mwanafunzi, yaani kuwa na viwango maalum vya kutunuku ( Fixed Grade Ranges).
Tume imebaini kwamba, pamoja na kwamba mfumo huo uliandaliwa kwa nia nzuri, utaratibu huo mpya haukufanyiwa utafiti na maandalizi ya kutosha kabla ya kutumika.
MAPENDEKEZO YA AWALI YA TUME
7. Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia masuala mbalimbali yaliyojitokeza wakati wa uchunguzi, Tume katika Taarifa yake ya awali imetoa mapendekezo mbalimbali yakiwemo yale yanayohitaji kutekelezwa kwa haraka.
Kutokana na kuwepo kwa mapendekezo hayo ambayo inabidi yafanyike kwa haraka, tarehe 29 Aprili, 2013 Baraza la Mawaziri lilipokea Taarifa ya Awali ya Tume na kuijadili ambapo liliridhia mapendekezo hayo yaanze kutekelezwa mara moja.
Maamuzi hayo ya Baraza la Mawaziri yanalenga kutenda haki kwa walimu na wanafunzi ambao juhudi zao za kufundisha na kujifunza zimepimwa kwa kutumia Mfumo mpya ambao hawakupata fursa ya kushirikishwa na kuandaliwa.
Mapendekezo hayo ni yafuatayo:-
- Matokeo ya Mtihani wa Kidato cha Nne mwaka 2012 yafutwe na yaandaliwe upya kwa kutumia utaratibu uliotumika mwaka 2011 ;
ii. Standardisation ifanyike ili matokeo ya wanafunzi yalingane na juhudi walizoziweka katika kusoma kwa mazingira na hali halisi ya Tanzania na uamuzi wa taifa kuongeza idadi ya shule na wanafunzi wakati uwekezaji katika ubora unaendelea;
iii. Baraza la Taifa la Mitihani limeelekezwa kuzingatia kuwa pamoja na kwamba sheria ya kuanzishwa kwake inawaruhusu kufanya marekebisho ya mchakato wa mitihani, lakini marekebisho yoyote ya kubadilisha utaratibu wa kupanga viwango vya ufaulu na madaraja ya matokeo ya mitihani, lazima yahusishe wadau wote wanaohusika na mitaala, ufundishaji na mitihani .
Wakati Tume inaendelea kukamilisha kazi yake, uamuzi wa Baraza la Taifa la Mitihani wa kutumia utaratibu mpya wa kupanga viwango vya ufaulu na madaraja ya matokeo ya mitihani uliotumika mwaka 2012 usitishwe na badala yake Baraza la Mitihani litumie Utaratibu wa mwaka 2011 kwa Kidato cha Nne na cha Sita kwa Mitihani yote ukiwemo utaratibu wa Standardization na kutoa matokeo mapya kwa kuzingatia maelekezo haya.
Aidha, mchakato wa mfumo wa tuzo wa taifa ( National Qualifications Framework ) na Mfumo wa kutahiniwa/ kutathmini maendeleo ya mwanafunzi katika masomo yake (National Assessment Framework ) ukamilishwe haraka iwezekanavyo.
UTEKELEZAJI WA MAPENDEKEZO YA TUME
8. Mheshimiwa Spika, kutokana na umuhimu wa mapendekezo hayo, Baraza la Mawaziri limeamua kwamba utekelezaji wa mapendekezo hayo uanze mara moja.
9. Mheshimiwa Spika, Tume ya Uchunguzi itaendelea kukamilisha taarifa yake vizuri kwa kuhusisha wadau mbalimbali ili kupata maoni zaidi na ushauri wao juu ya mambo mbalimbali yaliyobainika wakati wa uchunguzi kabla ya kuikamilisha na kuitoa kwa matumizi ya umma na vyombo mbalimbali.
HITIMISHO
10. Mheshimiwa Spika, Serikali inaipongeza sana Tume kwa kutoa mapendekezo ya awali ambayo Serikali imeyaridhia.
Aidha, Serikali inawashukuru wananchi wote na wadau mbalimbali wa Sekta ya Elimu wanaoendelea kutoa maoni na ushauri wao kwa Tume.
11. Mheshimiwa Spika, Serikali inawahakikishia Wananchi kuwa itaendelea kuboresha Elimu Nchini ili kuwezesha Watoto wetu wapate mafanikio katika maisha na maendeleo yao, kwani Wahenga wanasema “Elimu ni Ufunguo wa Maisha.”
12. Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUNDI
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
UFAFANUZI KUHUSU KUPITIWA UPYA KWA MATOKEO YA MTIHANI WA KIDATO CHA NNE MWAKA 2012
Mnamo tarehe 03 Mei, 2013 Serikali kupitia Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Mheshimiwa Wiliam Lukuvi (Mb) ilitoa Kauli ya Serikali Bungeni Kuhusu Taarifa ya Awali ya Tume ya Taifa ya Kuchunguza Sababu za kushuka kwa ufaulu wa Mtihani wa Kidato cha Nne Mwaka 2012.
Kauli ya Serikali ilielekeza kuwa matokeo ya Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne mwaka 2012 yafutwe na yaandaliwe upya kwa kutumia utaratibu uliotumika mwaka 2011 ili wanafunzi hao wawe katika mazingira yanayofanana na ya wenzao wa miaka iliyopita kwa kuwa mfumo uliotumika mwaka 2012 katika kupanga matokeo na madaraja ni tofauti na ule uliotumika mwaka 2011 na miaka iliyotangulia.
Kwa kuzingatia mapendekezo ya Tume na Maelekezo ya Baraza la Mawaziri, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, kwa mamlaka aliyonayo chini ya Sheria ya Baraza la Mitihani Tanzania, kifungu cha 20, sura 107 ameliagiza Baraza la Mitihani la Taifa kupitia upya Matokeo ya Mtihani wa Kidato cha Nne mwaka 2012.
Aidha, imeagizwa kwamba matokeo hayo yaandaliwe kwa kutumia utaratibu uliotumika mwaka 2011. Serikali haikuagiza kufanyika upya kwa mitihani hiyo na wala haikuagiza kusahihishwa upya. Hivyo, Serikali inapenda kuwahakikishia wananchi kwamba hapatakuwa na zoezi la kurudia usahihishaji wa mtihani huo kwa sababu hakuna dosari zilizobainishwa kwenye usahihishaji wa mitihani hiyo.
Alama za watahiniwa ambazo zimehakikiwa zipo tayari, kitakachofanyika ni kwa Baraza la Mitihani kutumia alama hizo kuchakata matokeo upya kwa kutumia viwango vya ufaulu vilivyotumika mwaka 2011. Utaratibu ambao umekuwa ukitumika tangu mwaka 1973 wakati Baraza lilipoanzishwa, ni wa kuweka viwango vya ufaulu kila mwaka kwa kuzingatia ufaulu wa somo husika na ufaulu katika mwaka uliotangulia.
Kutokana na maelezo hayo, ni dhahiri kuwa zoezi la kupitia upya matokeo ya Kidato cha Nne 2012 litachukua muda mfupi na matokeo yatatangazwa hivi karibuni.
Selestine Gesimba,
KAIMU KATIBU MKUU,
WIZARA YA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUNDI
10/05/2013