Pamoja na kuwa na kocha mahiri nchini, Kapteni Mary Protas, timu ya taifa ya netiboli Tanzania (Taifa Queens) huenda ikawa kapu la magoli wakati wa Michuano ya Kombe la Afrika itakayotimua vumbi kwa siku tano kwenye Uwanja wa Ndani wa Taifa jijini Dar es Salaam, kuanzia leo.
Wiki iliyopita wake wa viongozi waandamizi wa Serikali wakiongozwa na mke wa Waziri Mkuu, Mama Tunu Pinda, walikabidhi Sh 77, 800,000 kwa Mwenyekiti wa Chama cha Netiboli Tanzania (CHANETA), Anna Bayi, kuisaidia timu hiyo ifanye vizuri – kubwa kuliko yote wakitaka ilibakize kombe hilo nyumbani.

Nchi nane zitashiriki michuano hiyo ambayo mbali na wenyeji – Tanzania, nchi nyingine zitazoshiriki ni Kenya, Uganda, Malawi, Namibia, Angola, Zimbabwe na Botswana.

Akikabidhi mchango huo kwa Taifa Queens iliyoweka kambi katika Shule ya Sekondari ya Filbert Bayi iliyopo Kibaha, Mama Tunu alisema zaidi ya Sh milioni 27 nyingine zilikuwa zinaendelea kukusanywa kama ahadi kutoka kwa wahisani na wafadhili, jambo linalolenga kuitafutia ushindi na ubingwa.

Hata hivyo, wasiwasi walionao wadau ni kufanya vibaya kwa kupoteza mechi zote tano za kujipima nguvu ilizocheza hadi sasa, mbili kati yake zikifanyika kambini kwake, na tatu nyingine zikichezewa mjini Zanzibar.

Katika mechi hizo, Taifa Queens ilipokea kipigo cha jumla ya mabao 247-163. Ilianza kwa kuchapwa mabao 55- 24 na kisha ikalambwa 54-18 katika mechi za kujipima nguvu dhidi ya JKU Zanzibar – zote zikifanyika kwenye Uwanja wa Shule ya Sekondari ya Filbert Bayi.

Ilipokwenda Zanzibar katika mwendelezo huo wa kujinoa, Taifa Queens ilianza kwa kupambana na JKU na kucharazwa mabao 45- 36, kikafuatia kichapo cha mabao 43- 40 kutoka Kombaini ya Zanzibar kabla haijakung’utwa mabao 50-45 na timu ya Polisi.

“Nimebaini upungufu wa wachezaji wangu, natarajia kutangaza majina ya kikosi (kamili) kitakachoshiriki mashindano hayo (ya Kombe la Afrika),” anasema Kapteni Protas, Afisa mstaafu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) aliyeifanya timu ya Jeshi Stars kuwa tishio katika mchezo huo nchini alipokuwa akiinoa.

Ilikuwa ikitisha kwa timu zote zilizokuwa vinara wa mchezo huo nchini katika miaka ya 1980- 2000 kama NBC Mwanza, NBC Arusha, NBC Lindi, Bandari Dar es Salaam, JKT Mbweni na JKU Zanzibar.

Iliogopewa pia katika nchi zote za Afrika Mashariki na Kati inaposhiriki mashindano ya kikanda na kukutana na timu ngumu kama za Kampala City Council (KCC) au Nakivubo Villa za Uganda, Coffee au Nairobi City Council za Kenya na mabingwa wa ligi za Burundi, Rwanda, Malawi na nchi nyinginezo.

Ilikuwa ikitamba na wachezaji waliokuwa mahiri chini ya kocha huyo kama akina Bhoke Matambalya, Mbuke Tubanga, Agnes Musoma, Dhamiri Mshamu, Rose William, Margareth Fundi, Christina Kimamla, Hawa Mohamed, Asha Mhina, Grace Mugyabuso, Grace Daud au Sister (ambaye sasa ni marehemu) na kadhalika.

Ilikuwa ikicheza mechi zote za Ligi Daraja la Kwanza, Tanzania Bara na Ligi Kuu ya Muungano bila ya kupoteza hata moja na hivyo kutwaa ubingwa. Pale inapofungwa – tena kwa bahati mbaya mno na mara moja kwa mwaka mzima au miwili- ilikuwa ikizidiwa bao moja tu, sana sana ikipoteza dhidi ya Bandari Dar es Salaam.

Katika hali hiyo, idadi kubwa ya wachezaji hao wa Jeshi Stars ndiyo pia waliokuwa wakiitwa na kuunda kikosi cha Taifa Queens.

Walichanganywa na wachache kutoka timu nyingine hasa za NBC Mwanza, NBC Arusha, NBC Lindi, JKT Mbweni na Bandari Dar es Salaam kama akina Mary Anyangisye, Mhoja Nyawawa, Matalena Mhagama, Brigitha Msamati (ambaye ni marehemu), Sikitu Rupia na wengineo.

Tangu kustaafu kwa Protas katika JWTZ na hivyo kuachana na Jeshi Stars, amekuwa kocha wa Taifa Queens, lakini kukosekana kwa ushindani uliosisimua enzi hizo huku JKT Mbweni kwa mfano, ikifundishwa na Mary Swai, kumesababisha netiboli nchini iyumbe na kupoteza mwelekeo.

Sababu kubwa iliyofanya kutokea hali hiyo ni kusambaratika kwa timu zilizokuwa mahiri kwa mchezo huo kama za Bandari Dar es Salaam, Bora Dar es Salaam, Bima Dar es Salaam, NBC Mwanza, NBC Arusha, NBC Lindi, CDA Dodoma na nyinginezo kwa Tanzania Bara.

Aidha, mchezo huo pia umeyumba kutokana na kupita kwa kizazi cha kikosi mahiri kabisa cha JKU Zanzibar cha miaka ile ya 1990. Bado kinakumbukwa kilivyokuwa na wachezaji wanaopiga chenga za mwili huku wakikimbia kwa kasi kama wanariadha wa mbio fupi, wakatoa pasi kama zinazopimwa kwa rula huku kila moja ikienda mahali pake utadhani ina macho!

Kibaya zaidi ni hatua ya Chaneta kumtimua pia aliyekuwa Katibu Mkuu mwenye ujuzi na uzoefu mkubwa wa netiboli, Rose Kisiwa na kumweka Rose Mkisi.

Ukimwongezea na Mwenyekiti wake, Anna Bayi, mchezo huo katika ujumla wake nchini umekosa mwelekeo. Unazidi kudidimia ukilinganishwa na miaka iliyopita hususan kipindi ambacho Chaneta ilikuwa chini ya uenyekiti wa Chiku Shomari.

Kupoteza michezo yote mitano ya mwisho ya kujipima nguvu kwa Taifa Queens, tena kwa kufungwa idadi kubwa ya mabao huku yenyewe ikifunga kidogo sana, ni kuelekea kufanana na timu ya taifa ya soka (Taifa Stars) ambayo imeua hadi ushabiki wa mchezo huo nchini.

Michuano hiyo ya Kombe la Afrika itakayoshirikisha nchi nane ingawa Namibia imesema haitashiriki kutokana na ukosefu wa fedha, ina heshima kubwa kimichezo.

Kwanza kufanyika kwake Tanzania kumetokana na uamuzi uliofanywa na Shirikisho la Netiboli Duniani (IFNA), hivyo litaifuatilia kwa karibu na viwango vyake havitakuwa vya Afrika peke yake.

Ndiyo maana miaka michache iliyopita, Taifa Queens ilishiriki michuano ya dunia ya netiboli huko Malaysia baada ya kufanya vizuri katika mashindano kadhaa ya kikanda. Lakini kwa kuanza kufanana na Stars, kunatia mashaka iwapo inastahili kuwamo katika mashindano muhimu yanayoanza leo jijini Dar es Salaam.

Watanzania wameziona na kuzifurahia juhudi zinazofanywa na mke wa Waziri Mkuu, Tunu Pinda akishirikiana na wake wa viongozi wengine wa nchi yetu, mmoja kati yao akiwa ni mke wa Rais mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Anna Mkapa, za kuitafutia ufadhili timu hiyo.

Mathalani, kufanikiwa kwao kukusanya shilingi 77, 800,000 taslimu na kuikabidhi zote, ni hatua ambayo haikutarajiwa na yeyote kuanzia wachezaji, kocha wa timu hiyo na viongozi wa Chaneta.

Kinachotia wasiwasi ni kupotea kwa juhudi hizo zote kutokana na timu hiyo kufanya vibaya katika maandalizi, jambo linaloweza kufanana kwa kiwango kikubwa na jinsi mamilioni ya fedha zinazotolewa na wafadhili wa Stars kuteketea bila faida yoyote.

Kama akina dada hao tayari wamekuwa wakiogelea kwenye bahari ya mabao kutoka timu za ndani tu ambazo si za taifa, itakuwa kazi ngumu kushinda mechi kubwa za kimataifa wakati wa michuano hiyo ya Kombe la Afrika inayoanza leo.

Kila nikiitazama Taifa Queens naiona ilivyo dhaifu dimbani kama Taifa Stars, lakini kwa kumlindia heshima Mama Pinda na jopo lake, nadhani sasa italazimika kufanya kila inavyoweza ili kulibakiza kombe hilo nyumbani.