Taifa limepoteza mmoja wa wasomi, wanadiplomasia, na wanasiasa waliobeba mzigo wa matumaini ya Afrika Mashariki kwa mabega mawili bila kulalamika.

Balozi Juma Volter Mwapachu, aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa, amefariki dunia iana Ijumaa Machi 28, 2025 jijini Dar es Salaam akiwa na umri wa miaka 82.

Kuna watu huzaliwa na bahati. Wengine huzaliwa na akili. Lakini wachache sana huzaliwa na moto wa ndani – ile nguvu ya kimya inayowawezesha kuvuka milima ya maisha kwa utulivu, wakiwa wamebeba matumaini ya wengi mgongoni. Juma Mwapachu alikuwa mmoja wa hao wachache waliotuma maombi ya kazi kwa hatima, wakaajiriwa na historia.

Alizaliwa tarehe 27 Septemba, 1942 huko Mwanza – mji wa upepo mwanana wa Ziwa Victoria na mawimbi yaliyomlea kwa mafunzo ya kusimama imara. Baada ya kuhitimu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1969 kama mmoja wa wahitimu wa awamu ya mwanzo, Mwapachu alianza kazi kama askari polisi. Lakini haikuchukua muda – aliingia serikalini kupitia Wizara ya Serikali za Mitaa na Utawala wa Mikoa, ambako alianza kusoma siasa ya chini kwa chini. Ile siasa ya kuchochea harakati mtaani, si ya kutema hotuba majukwaani.

Akiwa huko, alianza kuandika mipango ya maendeleo kwa mkono mmoja huku mkono mwingine ukifuta jasho la changamoto — na hapa ndipo ndoto zake ziliota mbawa za chuma.

Miaka ya 2002 hadi 2006, alihudumu kama Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa na Mwakilishi wa Kudumu UNESCO. Katika kipindi hicho, Watanzania wachache walijua kuwa UNESCO haikuwa jina la bendi ya taarab kutoka Zanzibar — lakini kwa Mwapachu, ilikuwa jukwaa la kuunganisha dunia kwa njia ya elimu, sayansi, na utamaduni. Alikuwa balozi wa maono, si wa mialiko tu.

Aprili 4, 2006, Rais Jakaya Mrisho Kikwete alimpendekeza rasmi kuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Akapitishwa na wakuu wa nchi, na akachukua kijiti kutoka kwa Amanya Mushega. Mwapachu akawa Mtanzania wa kwanza kuiongoza EAC tangu ilipofufuliwa.

Kwa miaka mitano, alisimamia mikakati ya kuifanya Afrika Mashariki isibaki kuwa ndoto ya maofisini, bali iwe hali halisi kwa wananchi wa kawaida. Aliyavumilia makelele ya siasa, akachora ramani ya soko la pamoja, na akapigania umoja kama injini ya maendeleo.

Kama mtu ambaye hakupenda mapumziko ya kiakili, Mwapachu alikuwa na shahada tatu za heshima:
*Doctor of Literature – Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (2005),
*Doctor of Political Science – Chuo Kikuu cha Rwanda,
*Diploma ya Uzamili ya Sheria ya Kimataifa na Diplomasia – India.
Kwa hiyo, aliposema “elimu haina mwisho,” haikuwa methali — ilikuwa ni ratiba yake ya kila siku.

Mchango wake katika maendeleo ya taifa ni sawa na chemchemi isiyoishi. Alishika nafasi lukuki:
*Mwenyekiti, Bodi ya Shirika la Reli Tanzania (TRC),
*Mwenyekiti, Benki ya Uwekezaji Tanzania (TIB),
*Kamishna, Tume ya Mageuzi ya Mashirika ya Umma,
*Makamu Mwenyekiti, Baraza la Biashara ya Nje,
*Makamu Mwenyekiti wa Society for International Development (SID)
*Mwenyekiti, Baraza la Viwanda Tanzania (CTI),
*Mwenyekiti, Baraza la Biashara Afrika Mashariki,
*Mjumbe, Bodi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,
*Mwandishi na mshauri mkuu wa maandalizi ya Tanzania Development Vision 2025.

Oktoba 2015, Mzee Mwapachu alijitoa CCM na kumuunga mkono Hayati Edward Lowassa. Lakini mwaka mmoja baadaye, alirudi CCM kimyakimya. Wakati wengine wakibadilisha namba za magari kila Ijumaa, Mzee huyu alihama kwa msimamo, si kwa selfie.

Labda kilichomtofautisha zaidi ni ule moyo wa Afrika Mashariki alioubeba bila kujigamba. Alielewa kuwa maendeleo ya Mwanza hayawezekani bila utulivu wa Kampala, au kahawa ya Kigali kusafirishwa kwa urahisi kutoka Mombasa. Moyo wake ulikuwa na kipimo cha Mwalimu Nyerere — si kwa kumbukumbu, bali kwa matendo.

Familia ya Mwapachu ni kati ya zile zinazochora historia ya taifa. Baba yake, Mzee Hamza Kibwana Bakari Mwapachu (1913–1984), alikuwa kiongozi wa mwanzo katika harakati za uhuru wa Tanganyika. Akiwa Rais wa TAA, tawi la Tabora mwaka 1947, alifanya kazi bega kwa bega na Mwalimu Julius Nyerere, aliyekuwa Katibu Mkuu.

Hamza alifunga ndoa na Juliana Volter mwaka 1938, na walibarikiwa kupata watoto sita:

  • Harith Bakari Mwapachu: Alizaliwa Julai 25, 1939, na alikuwa mtoto wa kwanza wa Hamza na Juliana. Alipanda ngazi katika utumishi wa umma hadi kufikia nafasi ya Meneja Mkuu wa Shirika la Ndege Tanzania (ATC). Pia alihudumu kama Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mbunge, na Waziri wa Katiba na Sheria katika Serikali ya Awamu ya Tatu chini ya Rais Benjamin Mkapa. Alifariki dunia Februari 12, 2021, akiwa na umri wa miaka 81.
  • Rahma Mark Bomani: Aliolewa na Jaji Mark Bomani, Mwanasheria Mkuu wa kwanza mzawa wa Tanzania, na hivyo kuwa sehemu ya familia yenye mchango mkubwa katika sekta ya sheria nchini.
  • Juma Volter Mwapachu: Alizaliwa Septemba 27, 1942, huko Mwanza. Ni mwanasiasa na mwanadiplomasia maarufu wa Tanzania. Amehudumu kama Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa na pia alikuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuanzia Aprili 4, 2006, hadi Aprili 19, 2011.

Wengine ni Wendo Mtega Mwapachu, Tunu Mwapachu na Jabe Jabir Mwapachu

Mchango wa familia ya Mwapachu katika maendeleo ya Tanzania ni mkubwa, hasa katika nyanja za siasa, diplomasia, na utumishi wa umma. Historia yao inaonyesha dhamira yao ya kujenga taifa imara na lenye maendeleo.

Katika zama hizi ambapo umaarufu unapimwa kwa likes na retweets, maisha ya Mwapachu ni somo. Alikuwa icon aliyepita kimya kimya, bila kashfa, bila mabishano ya magazetini, na bila kufuatwa na kamera hadi grocery. Alikuwa boss wa maboss, lakini aliweza kukumbuka ladha ya maharage ya Bukoba na samaki wa Mwanza, hata alipokuwa akisaini mikataba ya mamilioni Ulaya.

Juma Volter Mwapachu ameondoka, lakini urithi wake unabaki. Kwa viongozi wanaotaka kujua maana ya kujitolea kwa taifa, kwa vijana wanaotaka kuandika historia bila kutegemea TikTok, na kwa taifa linalotafuta dira ya kweli — wasifu wake unapaswa kufundishwa, kusomwa, na kuheshimiwa.

Alikuwa si tu mjenzi wa taifa, bali pia mwanga wa kuangazia njia ya Afrika Mashariki. Na kama alivyoamini, maendeleo si ya mtu mmoja, ni safari ya wote. Na safari hiyo, aliianza na kuikamilisha kwa heshima ya juu kabisa.

Inna Lillahi wa inna ilayhi raji’un