*Bunge, wabunge, vyombo vya habari, wananchi tujadili
Ninakumbuka baadhi ya michango ya mjadala juu ya bajeti ya mwaka 2012/2013 na jinsi ilivyokuwa ya kichama zaidi kuliko uhalisia. Wabunge wetu walisahau kabisa kusudi kubwa kati ya yaliyowaweka bungeni, yaani utashi wa nchi, kwa maana ya uwakilishi wa mamilioni ya Watanzania waliowaamini na badala yake kwa kiwango kikubwa wakatekeleza utashi wa sera za vyama vyao na utashi binafsi.
UTASHI WA NCHI
Binafsi sikuuona utashi huu ukitawala katika Bunge hili la bajeti kama ilivyotarajiwa na watu wengi ambao ndiyo waliowatuma wabunge, hawa kwa kuwapa madaraka pale walipowachagua na kuvishwa mamlaka mara tu baada ya kuapishwa kushika nafasi hizo nyeti katika ustawi wa Taifa.
Bado naona hakuna uelewa wa kutosha kwa wawakilishi wetu juu ya dhima yao kwa umma wa Watanzania. Kama wangejitambua nilitarajia kwamba wangebadilisha mifumo yao ya kujadili masuala nyeti kama haya ambayo ndiyo gurudumu kwa safari yetu ili, ama tufike salama, au kwa shaka.
UTASHI WA SERA ZA VYAMA
Utashi wa aina hii umegubika sana Bunge letu kwenye mijadala mbalimbali. Kila chama kinajaribu kwa gharama zozote zile kukubaliana na kutekeleza ile methali ya “kila mwamba ngoma ngozi huvutia kwake”.
Chadema walikuwapo bungeni kuhakikisha kwamba kile wanachokitaka juu ya bajeti ndiyo cha msingi na kitekelezwe. Wakajaribu kuwashawishi wengine. CCM walikuwapo bungeni kuhakikisha kwamba kile kilichowasilishwa bungeni hapo na Serikali kinapita jinsi kilivyo kwa gharama yoyote ile na wakajaribu kuwashawishi hata wengine pia.
CUF, NCCR-Mageuzi, TLP na UDP wao walikuwa njia panda maana kwa kuwa ni Bajeti ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, CUF walijikuta upande mmoja wanayo Serikali ya Mseto na upande mwingine ni Wapinzani.
NCCR-Mageuzi, TLP na UDP walijitoa kwa utashi binafsi zaidi pengine wengine wakiangalia kiundani uhalali wa kinachopingwa na kile kinacholazimishwa. Utashi huu wa hivi vyama vitatu ulisababisha kila mmoja wa wawakilishi hawa asimame upande aliouona unamfaa hata kama si kwa maslahi ya Taifa.
UTASHI BINAFSI
Hii iliwawia vigumu sana wabunge wengi kukataa au kukubali maana wanafungwa zaidi na utashi na mfumo wa kisiasa, kwamba mbunge atokane na chama cha siasa. Kwa hali hii basi yule anayeweza kukiuka msimamo wa chama chake, basi ajiandae kupambana na adhabu ya sirisiri yaani kunyimwa fursa ya kuwa mgombea uchaguzi ujao kwa kuwa ni “msaliti” kwa tafsiri hafifu ya vyama vyetu ambavyo bado demokrasia haijashika kasi ya vitendo zaidi ya nadharia.
Ili kuwa kinyume kabisa na utashi wa sera za vyama, mbunge huyu hana budi kujitoa mhanga kwamba liwalo na liwe, lakini utashi wa taifa kwanza na mengine yafuate. Nimpongeze sana Mheshimiwa Mpina katika hili bila chenga.
Katika hayo matatu kuelekea ukuaji wa demokrasia ya kweli ya nchini kivitendo, umekuwa ni mtihani mkubwa kwa CCM na hata vyama vya upinzani kwa kuwa kila mtu anahitaji kuwa “mmiliki” wa kiti cha ubunge na hivyo kufanya ukuaji wa demekrasia kwa maana halisi ya demokrasia kubaki kuwa nadharia sawa na nadharia ya mgawanyo wa madaraka katika mihimili mitatu ya Serikali, yaani Bunge, Mahakama na Serikali.
Kadri siku zinavyosonga mbele ndivyo hii inavyoharibu ustawi wa Taifa kwa kuwa na migongano ya kimaslahi.
Mwanafalsafa Aristotle (384-322 BC) aliyeishi miaka ya nyuma kabla ya Kristo aliliona hii. Ndiyo maana alisisitiza uwepo wa utawala wa kikatiba na kuwapo na sheria zinazoiongoza jamii fulani katika utekelezaji wa shughuli zao, akipingana na falsafa ya mwalimu wake, Plato, kwamba kiongozi ni lazima awe msomi aliyefuzu ngazi mbalimbali kiutawala.
Aristotle anasema, “An ideal state is a constitutional based on law, any good state, law must be the ultimate sovereign and not any person” mwisho wa kumnukuu.
Hii inamaanisha kwamba katika sheria tunazoziweka zisimfanye mtu yeyote awe juu ya sheria, kwa maana ya kwamba sheria huwapo kwa ajili ya kutenda haki na hivyo kumuwajibisha mtu yeyote bila kujali nafasi yake. Kwa maana nyingine ni kwamba mwanadamu bila sheria anaweza kuwa mtu wa ajabu na kutenda mambo ya ajabu sana.
Hata Mungu pia alimpa Musa sheria (amri) 10 ambazo ndimo hasa hizi sheria za wanadamu zilimopatikana, sasa inapokuwa mmoja kati yetu anakuwa juu ya sheria maana yake ni kwamba si mwanadamu mwenzetu – sijui yupo fungu gani?
Nina wasiwasi kwamba tumefika hapa kwa sababu ya kutokuwa na utawala wa sheria na utawala bora katika uhalisia wake, zaidi ya kuwa nao kinadharia na kuwa na utekelezaji hafifu kabisa. Sipendi kurejea nyuma, lakini ningependa kukumbushia tu kwamba ili mtoto awe na tabia njema na maadili, basi ni dhima ya mzazi kuwa katika mfumo wa tabia njema katika maisha yake na maadili.
Waswahili walisema “mtoto umleavyo ndivyo akuavyo”. Mwanafalsafa St. Thomas Aquinas (1225-1274) alisema, “Morality is not an arbitrary set of rules to regulate human behaviour but rather is based on the very nature of human person”.
Anaendelea kwa kusema; “Moral truth is to do good and avoid evil”. Hawa ni wanafalsafa wa miaka mingi sana, lakini leo yale waliyoyasema yanajitokeza katika jamii zetu duniani na hatimaye tunapata mambo yasiyofaa.
Leo hii Taifa limeacha kuwa na utawala wa kisheria na badala yake tumetawaliwa zaidi na ushabiki wa kisiasa bila kujali unavunja Katiba kwa kiasi gani. Tumeacha misingi na kanuni za uongozi na tumegeukia fursa binafsi zaidi kwa kukidhi matakwa yetu binafsi.
Baba wa Taifa, Mwalimu julius Nyerere, alilalamika juu ya ukiukwaji wa Azimio la Arusha lililoweka misingi thabiti na imara, juu ya kiongozi anapaswa awe wa aina gani, lakini aliishia kwa kusema kwa uchungu “kulizungumzia Azimio la Arusha hadharani inabidi uwe na akili ya kiwendawazimu.”
Akaongeza kwamba yapo madhara makubwa kuwa na Taifa linalokumbatia walanguzi. Nakumbushia tu sote turejee kitabu chake cha “Uongozi wetu na Hatima ya Tanzania”. Tukikisoma vyema katu hatutashangaa tumefikaje hapa zaidi tutapata fursa ya kujitafakari na kujirekebisha.
Nikirudi katika hoja yangu ya msingi, tunawezaje kuwa na Taifa la waadilifu ambao hawapaswi kusemwa hadharani wanapenda na kufurahia wakisemwa sirini na hadharani washangiliwe na kusifiwa?
Tunawezaje kuwa na Taifa lenye maadili kama kwa makusudi kabisa watawala waliona Azimio la Arusha linawabana wakatengeneza azimio lao? Tunawezaje kuwa na Taifa la maadili kama wabunge hawajiamini, wanafanya kazi na kutoa mamlaka kwa wachache katika misingi ya “fear of force, personal agreement na strategic compliance?”
Binafsi nilidhani kwamba lugha za kejeli na matusi ziliishia kwenye uchaguzi mdogo wa Arumeru Mashariki, nikidhani kama viongozi ndani ya vyama vyetu vya siasa tulijifunza kitu au pengine tulichojifunza ni kwamba lugha zile zinajenga Taifa? Wasiwasi wangu mkubwa ni jinsi gani dhihaka hizo kwa Watanzania zimehamishiwa katika chombo kilichopewa dhamana kubwa ya kutunga sheria na kusimamia maslahi ya walio wengi.
Kejeli, ngonjera na malumbano yasiyo na msingi vimepewa fursa kubwa sana bungeni kuliko jambo la msingi, huku kila mtu akidhani akisema kwa mfumo huo ndiyo wapiga kura wake watamwona anastahili kurejea kwa kipindi kijacho.
Moja kati ya dhihaka ni pale mtu anapofahamu fika matatizo ya wapiga kura wake, lakini hayupo tayari kutetea na kusimamia kuondoka kwa tatizo walilonalo. Kwa mfano, mbunge anajua kwamba kwa sababu ya shida ya maji wapiga kura wake wanadiriki kubadilishana debe moja la mahindi kwa ndoo moja ya maji – uwiano ambao haupo popote pale hata kwa sisi ambao hatujui hesabu.
Lakini kama mwakilishi tayari ameona wazi kwamba bajeti iliyotengwa kwa ajili ya kushughulikia tatizo hilo haikidhi haja, lakini bado anathubutu tena kwa mbwemwe kabisa kwamba “naunga mkono hoja mia kwa mia” yaani bila kuacha hata chembe ya shaka (beyond reasonable doubt).
Tumtafsirije mbunge huyu si tu juu ya uwezo wake wa kufikiri, lakini je, ni kweli anawakilisha wananchi? Ama ni ile dhana ya kuvaa ngozi ya kondoo kumbe ni mbwa mwitu?
Napata shida sana kwa sababu tu pengine sijabobea katika Kiswahili, lakini tafsiri yangu isiyo rasmi kwa maneno yaliyotamkwa na Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (Chadema), bungeni iliyosababisha kutolewa nje ya ukumbi wa Bunge kwa amri ya Naibu Spika “wa ukweli” Mheshimiwa Job Ndugai na kutekelezwa na askari wa Bunge ni hii:-
UDHAIFU: Ni kushuka kwa uwezo wa kawaida wa kitu au mtu. Mfano mtu kushindwa kutambua wajibu wake kama baba katika familia, mwalimu shuleni, dereva barabarani, mchezaji uwanjani, hakimu mahakamani nk.
UZEMBE: Ni utendaji wa jambo au mambo bila kufikiri na hivyo kupelekea madhara fulani ambayo yangeweza kuepukwa. Kwa mfano kunywa pombe na kulewa halafu unaendesha gari.
UPUUZI: Ni uhayawani wa kutenda kitu kwa makusudi pamoja na kujua athari zake lakini ukabadilisha kwa makusudi ukidhani tu kwamba matokeo yake hayatakuwa hayo. Mfano ni kuchukua chemli au yai na kulibwaga kwa kishindo kabisa sakafuni ukitarajia kupata majibu tofauti na yale ya kuvunjika kwa chemli au yai hilo.
Sitaki kuwa upande wowote katika hili, lakini pia nikiri kwamba inawezekana Mheshimiwa Mnyika alikuwa na maana tofauti na yangu silazimishi kwamba hii ndiyo iwe tafsiri halisi.
Lakini kwa tafsiri yangu ni kwamba sijaona ubaya wa hoja yake na pengine alipaswa kuachwa aendelee, ili baada ya kumaliza tafsiri yake ndiyo ingetupeleka kwenye adhabu gani anapaswa kuchukuliwa kwa labda kukiuka vipengele vya kanuni za Bunge kama ilivyopendekezwa na Mheshimiwa Lukuvi na kutafsiriwa na Naibu Spika.
Sina hakika sana na kwa nini kanuni ilisema kwa msisitizo, “hasa kwa kumtaja jina lake” wengine wanisaidie kwamba je, angeishia tu kusema “rais” isingemgharimu hivyo? Mheshimiwa Mnyika ni mbunge na sijaona kosa lake kwa kusema uzembe wa Bunge na wabunge ikimjumuisha na yeye pia.
Hii ni kwa maana moja kubwa; kwa mfano baada ya bajeti kupitishwa bungeni Ijumaa siku hiyo hiyo, vyombo vya habari vya kielektroniki yaani runinga na radio viliripoti kwamba “Bunge limepitisha bajeti” na kesho yake magazeti nayo yaliandikwa kwa vichwa vya habari vikubwa kwamba “Bunge lapitisha bajeti”.
Taarifa hii kwa umma haiwatenganishi waliokataa na waliokubali kwa sababu inahitaji uchambuzi wa kina kujua kulikuwa na pande mbili zilizovutana bungeni juu ya suala hilo, kinyume cha hapo ni kwamba wananchi walio wengi hasa wale ambao hawakupata fursa ya kusikiliza na kusoma mijadala hiyo wanabaki na taswira ya Bunge zembe kuwafikisha pahala ambako wao wanaona hapakustahili.
Wabunge wote wataambiwa ni wazembe kwa sababu wameshiriki katika vikao na hawakuchukua uamuzi kama ulipaswa kuchukuliwa. Na hili ndilo kwa upande mwingine linaloibua juhudi za wabunge binafsi kama kina Mheshimiwa Luhaga Mpina. Upuuzi alioumaanisha pengine Mheshimiwa Mnyika ni ile hali ya kujua ubovu wa bajeti, lakini kwa kukikomoa tu chama fulani, tunaamua kuungana kuipitisha ili wapinzani wetu wasije wakajichukulia umaarufu.
Tunakubaliana kumlinda mvunja yai au chemli kwa kusema ni ndugu yetu. Tunasema hili yai au chemli havikupaswa kuvunjika kwa kubamizwa tu chini na wala hakuna sababu ya kumsema chochote mtenda kosa. Wabunge watambue kwamba hii ni dhana ya mafahali wawili wapiganapo ziumiazo ni nyasi.
Wakati wao wakiendelea kuhakikisha kwamba wanalinda kila kitu kama mafahali, basi wajue kwamba sisi nyasi si tu tunaumia, bali tunaangamia kabisa. Wapi dhana ya uwajibikaji wa pamoja?
MAADILI NA CHIMBUKO LAKE
Zamani kidogo nakumbuka mtoto alikuwa ni wa jamii nzima kwa maana ukifanya kosa kama mtoto, mzazi yeyote anaweza kukukanya na au kukuadhibu ikibidi. Jamii ya wakati huu ilikuwa na maadili mazuri sana na heshima ilijengeka katika jamii yetu.
Baadaye hali ikaanza kubadilika kila mtu na mtoto wake, ni marufuku kumkanya au kumuadhibu mtoto ambaye hukumzaa wewe kwa sababu ukifanya hayo tarajia matusi kutoka kwa mtoto mwenyewe na pia kwa wazazi wa mtoto au hata kufikishwa kwenye vyombo vya sheria kwa kisingizio cha kuvunja haki za mtoto. Sipati picha tunakoelekea.
Wazazi huweka kipaumbele kikubwa katika kuhakikisha wanalitetea kwa hali na mali tatizo alilotenda mtoto wao na kulihalalisha kwa wingi wa kejeli, nahau, methali na misemo. Ushabiki na ule tunaouita uchungu wa mwana aujua mzazi vimetufikisha hapa tulipo leo.
Majambazi wanajulikana wazi na familia zao, lakini wakisikia tu kakamatwa kwa kosa la kuua hata watu 10 tunajidai tunaongozwa na “uchungu wa mwana” kuuza hata mali ili tumuwekee dhamana kama sheria inaruhusu kwa kosa alilotenda.
Tunahangaika usiku na mchana kwa kupishana kwa waganga wa kienyeji wafanye viinimacho ili ashinde kesi, kuwahonga mahakimu na majaji ili wapindishe misingi ya kisheria au ikibidi hata polisi kabla hawajamfikisha mtuhumiwa sehemu ya mbali zaidi.
Yote haya yanafanyika kwa makusudi zaidi baada ya kuona wengi wetu kwanza hawajui haki zao za msingi, au wamekuwa wakitishwa kwa muda mrefu na vyombo vya dola na hivyo wangali na hofu mioyoni mwao juu ya kudai haki zao na hivyo uoga wao kutumiwa kama mwanya.
Wazee wamekuwa wakitembea na watoto wao au wakati mwingine hata wajukuu zao kiumri, lakini wamejiingiza kwenye uhusiano nao wa kimapenzi na hivyo kumomonyoa maadili ya jamii. Watoto hawaheshimu tena watu wazima kwa sababu anaona ni kama mnalingana. Kama ungekuwa mkubwa kiasi hicho unachodhani unastahili heshima, uliwezaje kujifunika naye shuka moja tena mkiwa watupu?
Haya yote ndiyo yaliyofanya jamii yetu iwe hivi leo hii kama tutawarejea wanafalsafa wetu Aristotle na St. Thomas Aquianas.
Naliona tatizo kubwa la Watanzania katika kujua nini kinapaswa kujadiliwa na kwa wakati gani. Nadhani huu ulikuwa wakati mwafaka wa kujadili kwa kuinyambua bajeti yetu kwa mujibu wa vipengele, ili kujua nini kingekuwa mbadala wake kama si hiki kilichopo.
Kwa mfano, wale wanaobadilishana maji kwa debe la mahindi tunawezaje kuwanusuru kwa sababu tabu aliyoipata mkulima huyu kulihangaikia debe hilo moja la mahindi ni kubwa sana ikilinganishwa na linavyobadilishwa kirahisi kabisa kwa ndoo ya maji?
Tunapaswa kujaribu kuangalia na kuchambua kunahitajika bajeti kiasi gani katika majimbo yetu ili kufanikisha miundombinu na maendeleo ya jimbo. Tuweke uchambuzi huo kwenye mipango thabiti ya kimkakati ya utekelezaji wake. Tufanye hivi kwenye barabara, elimu, afya, kilimo na mambo kama hayo.
Nina wasiwasi mkubwa wabunge wengine hata hawajui majimboni mwao wanakabiliwa na matatizo gani. Hii ni hatari, tunazidi kuijenga jamii ambayo inachoka zaidi kimtazamo, kimawazo na kiuamuzi ambayo kesho tutaivuna kwa uchungu mkubwa.
Yaliyoandikwa juu ya bajeti kwa mfumo uleule tuliouzoea hayatoshi kumhakikishia mwananchi uhalisia wa bajeti kwa uwiano wa maendeleo yao, na kodi zao na rasilimali zao. Vyombo vya habari viende mbali zaidi kupeleka hili kwa wananchi badala ya kuishia hapo ambako wala si robo ya walichopaswa kukijua wananchi.
Tatizo kubwa ni kwamba wasomi na baadhi ya vyombo vya habari wamekuwa wakiegemea upande mmoja. Uzito wa kujadili kauli za Mheshimiwa Mnyika kwangu mimi haubebi mzigo wowote juu ya dhambi inayofanywa na jitihada za kumkwamua Mtanzania katika lindi la umasikini linalomzunguka. Tunakwenda wapi?
Tuache kutafuta muonekano wa jinsi gani tumemtetea aliyeguswa na kauli za mbunge – tutawajadili wangapi? Ni kweli hayo ndiyo ya msingi tunayopaswa kuyajadili leo na hatuna mengine? Mheshimiwa Livingstone Lusinde na wengine wa aina yake kwa kauli kama walizotoa hadharani Arumeru Mashariki tumewajadili kiasi gani?
Hatuwezi kuwa na kauli mbovu majukwaani halafu tukadhani tutakuwa na kauli nzuri bungeni kwani tofauti ya “moral behaviour” ya mgombea na mshindi wa uchaguzi ni nini? Tujiulize zaidi nini makuzi yao katika nyanja hii ya siasa? Nini “moral” yao katika nyanja hii ya siasa? Tunatarajia kuvuna nini kwao? Kubwa zaidi najiuliza wapi utawala wa kisheria na dhana ya uwajibikaji? Nani katengeneza kizazi hiki cha wanasiasa?
UZOEFU KWA SIASA ZETU
Tunashindwa kabisa kutambua kwamba kama taifa tunalo tatizo la msingi la kulazimisha kutetea hata mambo yasiyofaa ili kulindana. Kama Bunge letu halipaswi kuwa wazi, tunawezaje kuwa na uwazi katika uwajibikaji wa Serikali? Nani anaisimamia Serikali kutekeleza dhima zake kwa uwazi na ufanisi?
Sipendi kurudi nyuma, lakini mada inanilazimisha kufanya hivyo, Bunge lilisimama kidete kabisa kukataa uwepo wa rushwa katika zabuni iliyowezesha kununuliwa kwa rada, lilitetea kwa nguvu zote na kupinga kwamba hakuna ubadhirifu katika akaunti ya EPA, mabishano makali yaliibuka juu ya ubovu wa mikataba ya madini.
Ukiukwaji wa zabuni zilizoipa ushindi kampuni ya Richmond kuhusu umeme wa dharura, ubadhirifu wa wazi wazi juu ya aliyekuwa katibu Mkuu wa Nishati, David Jairo, yaliyojiri na yaliyosababisha kuundwa upya kwa Baraza la Mawaziri na mengine mengi.
Haya yote pamoja na kejeli nyingi, hatimaye yalijidhihirisha na Taifa likajiingiza katika migogoro mikubwa. Suala la mgodi wa North Mara na athari wazipatazo wakazi wa huko. Mheshimiwa Balozi Kagasheki alijionea mwenyewe, lakini sijaona jinsi lilivyopewa kipaumbele na kulitokomeza. Je, ni kweli tuamini kwamba tunalo Bunge makini?
MGAWANYO WA MADARAKA
Napata ugumu wa kutafakari katika dhana nzima ya mgawanyo wa madaraka kwamba ni jinsi gani unatekelezwa kwa vitendo. Mbunge ambaye ni waziri anamwakilisha nani katika Bunge? Jibu rahisi zaidi litakuwa ni Serikali. Sasa kuna haki yoyote kweli imetendeka juu ya wananchi anaowawakilisha jimboni kwake?
Kwa mfano, kuna shida ya maji jimboni kwake na ni kilio cha muda mrefu, lakini mbunge wao huyo ndiye anayepaswa kujibu hoja hiyo bungeni, hapo atasimama upande gani wa hoja hiyo? Ni kweli hakuna mfumo mbadala wa kufanya waziri awakilishe Serikali peke yake, mbunge awakilishe wananchi na mahakama iwe peke yake ili kuweka dhana ya mgawanyo wa madaraka na uwajibikaji katika uhalisia? Haya nadhani yalipaswa kuwa mambo ya msingi ya kuyajadili.
MATUNDA YA USIRI
Matatizo ya Muungano tunayoyaona sasa ya kuibuka kwa vikundi kama Uamsho, ni matokeo ya kuzibwa midomo kwa muda mrefu kwa wananchi au wabunge kulizungumzia suala hilo kwa uwazi kwa dhana ile ile kwamba kwa kufanya hivyo ni kukiuka kanuni zilizowekwa ili kuulinda Muungano.
Wakati lile kundi la vijana waliojitokeza na kuandika barua kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa juu ya kuukataa Muungano sikuona juhudi za makusudi za kuwaita watu hawa ili wasikilizwe mawazo na kutoa maoni yao kwa haki na demokrasia juu ya Muungano, badala yake tuliwaona wendawazimu.
Tukirudi nyuma waliopendekeza mifumo tofauti ya Muungano ama kuusema wazi kwamba una kasoro walichukuliwa kama wahaini. Sina maana ya kuupinga Muungano lakini hapa tulipofika ni matunda ya usiri wetu juu ya suala hilo kwa hirizi ya unyeti wake. Haya tunayoyaona bungeni kwa sasa ni matokeo ya kunyimwa fursa ya kuhoji na kusema waziwazi yasiyofaa kwa muda mrefu sana kwa wale waliokuwa na mawazo mbadala juu ya yale yaliyowasilishwa na Serikali.
Nasikitika kwamba bado hatujifunzi tu. Huwa tunajisikia fahari sana kupiga kelele mtu akiwa amemaliza muda wake madarakani na katu hatuwezi kumrekebisha akiwa madarakani.
Hii ni sawa kabisa na kumuonya mtu aache matendo mabaya akiwa tayari ni maiti, kitu ambacho hakisaidii kwa hali yoyote. Kama Katiba yetu hairuhusu kwa sasa, basi mimi naomba kutoa mapendekezo ya kuongezwa kwa kipengele hicho kwamba hatua zichukuliwe kwa yeyote hata kama yu madarakani tena kwa uwazi na kuvunja uzio uliojengwa kwenye ibara ya 46 ya Katiba yetu ya sasa.
Hii itarudisha nidhamu na uwajibikaji kwa watawala wetu kinyume cha hapo ni ngonjera na mashairi yaliyokosa vina na vibwagizo. Tusiendelee kutenda mambo yaleyale huku tukitarajia matokeo tofauti, tunapanda maharage halafu matarajio yetu ni kuvuna mpunga – katu haiwezekani.
Zaidi sisi tunaona kujiuzulu au kuondolewa katika nafasi za kazi ndiyo adhabu pekee kwa wasiowajibika na wafujaji wa mali za umma. Wataendelea kufanya hivyo kwa kuwa sasa wamejua kwamba kuna kuondolewa na hakuna hatua zaidi. “No matter” wakirudi majimboni mwao wanapokewa kifalme maana wananchi hawaoni hatia zaidi ya unafiki na kujipendekeza kwa baadhi ya wanasiasa.
Hii inajenga matabaka na inakuza uhasama baina ya walio na hoja za maslahi ya Taifa na walio na hoja za maslahi binafsi. Tunakumbuka dada yetu Beatrice Shelukindo alivyoanza kumiminiwa meseji za vitisho baada ya kusimama imara kuweka hadharani uozo ndani ya Wizara ya Nishati na madini.
TUFUNGUKE ZAIDI YA HAPA TULIPO SASA TUMHOJI MTU BILA KUJALI NAFASI YAKE, ATAWAJIBIKAJE BILA KUHOJIWA NA KUAMBIWA UKWELI? TUJADILI YA MSINGI TUACHE KUWA WALINZI WASIOJUA WANACHOKILINDA. DEMOKRASIA NI NINI?
Tujibu hili swali kwanza kwa mapana yake na tusikimbilie tu moja kwa moja kuangalia mipaka ya demokrasia. TUWE JASIRI, WAKAKAMAVU na WENYE KUJENGA NGUVU ZA HOJA ili zitawale HOJA ZA NGUVU.
TUNATAKA TANZANIA MOJA YENYE AMANI NA MAENDELEO na si UTULIVU NA UMASIKINI.