Tafiti zilizofanywa na taasisi mbalimbali siku chache zilizopita kuhusu kukubalika kwa wagombea wa nafasi ya Rais zinaonesha Tanzania imejaa baadhi ya wasomi “wapuuzi”.

Hii ni kutokana na kuweweseka kwa chama kinachotakiwa kuondoka madarakani na kupisha fikra mpya kutawala na kuleta matumaini ya kweli kwa Watanzania waliolizwa kwa miaka zaidi ya 50 iliyopita.

Wameibuka baadhi ya wasomi ambao mimi naona ni wahuni walioamua kwa akili zao kwa lengo la kupofusha macho watu ama kwa kushawishi kwa kuibua matokeo ya tafiti za ulaghai kwa wananchi.

Taasisi ya Twaweza walikuwa wa kwanza kuwahadaa Watanzania kwa utafiti wao ulioleta fedheha kubwa kwa wasomi wetu ambao wanaonekana elimu zao ziko kwa ajili ya kueneza ujinga kwa wananchi na kuganga njaa tu. Hii ni hatari kubwa na aibu kwa wasomi tulionao.

Wakafuata watafiti wengine ambao ni umoja wa katiba ya wananchi (Ukawa) wao wakampa ushindi Mgombea wa Chadema, Edward Lowassa kwamba anaongoza kwa asilimia 76 wakati ule wa Taasisi ya Twaweza ikimpa ushindi mgombea wa CCM Dk. John Magufuli kwa asilimia 65.

Ukaibuliwa utafiti mwingine wa taasisi Tanzania Development Initiatives Program (TADIP) uliompa ushindi wa asilimia 54.5 Lowassa dhidi ya Dk. Magufuli wa CCM aliyeambulia asilimia 40.

Tafiti zote hizi na zingine zinazokuja zikiwahusisha wapiga ramli wasomi zina lengo moja tu la kuwahadaa wananchi wanaotarajia kuwachagua viongozi watakaoleta matumaini ya kweli kwa watanzania kuondokana na umaskini unaoendelea kukua mwaka hadi mwaka.

Ukizingatia tafiti hizi zinaendeshwa na wasomi wetu ambao wanaonekana kutumika kisiasa zaidi na kuganga njaa wao na familia zao na wale wanaowatumia kwa matakwa ya kisiasa. Watanzania wenzangu “wapumbavu na malofa” naomba tupuuze tafiti hizi na kusubiri utafiti wa kweli ndani ya boksi la kura.

Lakini ninachoweza kuwaeleza enyi wapumbavu na malofa ni kwamba utafiti ambao si wa mafichoni uliofanywa pale kwenye soko la Kariakoo jijini Dar es Salaam kwa kura za wazi ambazo hazikuwa na wachakachuaji zilionesha mgombea wa Chadema aliongoza kwa asilimia 90.

Wananchi walishiriki kupiga kura wakiwa kwenye foleni na baada ya matokeo yao kutangazwa walijikuta mikononi mwa polisi kwa kufanya kazi ya NEC. Huu nao ni upuuzi uleule ulioasisiwa na wasomi wetu.

Wasomi wa Tanzania wakiwemo wenye vyeo vya Uprofessa na Udaktari wamekuwa wakitumiwa na viongozi waliojaa hila kutulaghai wananchi na matunda ya upuuzi wao sasa yanaonekana.

Serikali kwa kuwatumia wasomi hawa hawa ilithibitisha kuwa dawa iliyokuwa ikitolewa na babu wa Loliondo, Mchungaji Ambilikile Mwasapile, aliyodai kuoteshwa na Mungu kuwa inatibu magonjwa yote na wananchi kuuamini uongo.

Ni Maprofesa na Madaktari wetu hawakuweza kutumia utashi wao na taaluma zao kuwaeleza ukweli wapumbavu na malofa walioshindwa kupata tiba bora katika hospitali zetu na kuaminishwa babu wa Loliondo ndio kimbilio lao.

Viongozi waandamizi wa Serikali hii bila aibu waliongoza msafara mrefu wa malofa kwenda kupiga kikombe kwa babu wa Loliondo, lakini hakuna aliyetupa majibu ya kweli juu ya uponyaji wa dawa hiyo.

Wananchi waliominishwa upuuzi huo na Serikali na kuacha kutumia dawa zilizotolewa na wataalamu wetu hawahawa na kuaminishwa kupiga kikombe cha babu walipoteza maisha kwa maelfu yao na waliotuaminisha tiba hiyo wamekaa kimya kama hawaelewi kilichotokea.

Kwa mujibu wa aliyekuwa Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hussein Mwinyi, utafiti wa kulinganisha wagonjwa wa Ukimwi na kisukari waliokunywa dawa hiyo na wale ambao hawakunywa, umebaini kwamba hakuna utofauti wa afya ya mgonjwa.

utafiti huo uliofanywa na Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), ulihusisha wagonjwa 200 waliofuatiliwa kwa kupimwa damu, kinga ya mwili (CD4) na uzito wa mgonjwa, ambao ulifanyika tangu mgonjwa alipokunywa kikombe cha babu na kubaini hakukuwa na tofauti kati mgonjwa aliyepiga kikombe na yule asiyepiga kikombe.

Kwa ufupi yatosha kueleza kwamba wasomi wetu wanajitia doa. Kuna baadhi ya viongozi wa Serikali walihusika kulaghai Watanzania kwa kuishabikia na kuitangaza dawa ya Loliondo kwamba ni miongoni mwa tunu za taifa huku akina William Lukuvi wakapeleka umeme wa jua na Magufuli akihakikisha barabara zinapitika ili malofa wakapige kikombe bila shida.

Ulaghai huu wa Babu wa Loliondo hauna tofauti na watafiti wetu wa kura waliojitokeza kwa upuuzi ule ule na ramli chonganishi ile ile yenye nia ya kutowesha amani ya nchi yetu.

Wanaotafuta kuharibu amani ya nchi yetu ni wasomi hawa ambao wameamua kutumika kwa tafiti za kipuuzi na NEC ambayo imeshindwa kukemea ujinga huu na mwingine unaofanywa majukwaani na baadhi ya wagombea.