Na Lookman Miraji.l
Siku ya ukombozi wa nchi kusini mwa Afrika ni miongoni mwa siku muhimu zinazokumbukwa na jumuiya ya maendeleo ya nchi za kusini mwa Afrika SADC.
Siku hii inabaki kuwa kumbukumbu bora ya kudumu katika mapinduzi ya kisiasa barani Afrika. Maadhimisho ya siku hiyo hutajwa kama sehemu ya juhudi za kuenzi na kuhifadhi historia ya ukombozi wa mataifa ya kusini mwa Afrika.
Kufuatia mkutano mkuu wa 38 wa wakuu wa nchi na serikali wa SADC uliofanyika jijini Windhoek, Namibia mnamo mwezi Agosti 2018, tarehe ya Machi 23 ya kila mwaka iliidhinishwa kuwa siku rasmi ya kusherekea ukombozi wa nchi za kusini mwa Afrika.
Nini Kilitokea Mwaka 1988?
Ili kuijua vyema siku ya ukombozi wa nchi za kusini mwa Afrika basi turejee nyuma katika historia miongo kadhaa ambapo ilikuwa ni mwaka 1988 pale majeshi ya kiafrika yalipofanikiwa kuishinda vita ngumu dhidi ya majeshi mtawala wa Afrika Kusini na kuweka ukomo wa utawala wa kimabavu na ubaguzi wa rangi uliokuwa umekithiri kwa wakati huo hasa nchini Afrika Kusini.
Ilikuwa katika mji wa Cuito Cuanavale, kusini mwa nchi ya Angola ndipo ahadi ya ushindi wa vita hizo zilizokuwa zikiathiri maisha ya waafrika wengi ukanda wa kusini ilipopatikana. Kufuatia ushindi huo ulipelekea utawala wa ubaguzi wa rangi na washirika wake kukubali Azimio la baraza la usalama la Umoja wa mataifa (UNSCR) 435/78 azimio lililowezesha pia kupatikana kwa uhuru wa taifa la Namibia mnamo Machi 21 mwaka 1990.
Kwanini Siku ya Ukombozi ni Muhimu kwa Tanzania?
Maadhimisho ya siku siku ya ukombozi wa Afrika yamekuwa na yataendelea kuwa muhimu kwa Tanzania kutokana na mchango wake wa hali na mali katika kusaidia harakati za ukombozi wa bara la Afrika. Tanzania chini ya uongozi wa Baba wa taifa, Mwalimu Julius Nyerere ilishiriki kutoa misaada ya kidiplomasia, misaada ya kijeshi na rasilimali katika kusaidia vyama vya ukombozi hadi kufanikisha kupatikana kwa uhuru wa mataifa mengi ya Afrika. Itakumbukwa jina la Mwalimu Julius Nyerere si jina geni katika baadhi ya nchi za Afrika kama Afrika Kusini, Zimbabwe, Msumbiji, Namibia, Zambia, Angola za nyinginezo ambazo mchango wa Rais Nyerere ulisaidia kupatikana kwa uhuru wa kisiasa katika mataifa mengi barani Afrika.
Baadhi ya wanahistoria barani Afrika wanauelezea mchango wa Mwalimu Nyerere kwa baadhi ya mataifa kama sehemu muhimu ya kupatikana kwa Amani katika nchi nyingi jirani za Afrika. Ni kweli nami naungana na wasomi hao wa historia katika hoja hiyo kwani ni kweli yawezekana kama Mwalimu Nyerere na viongozi wengine wasingechangia kupatikana kwa uhuru katika baadhi ya mataifa mpaka hii leo hata baadhi ya nchi za Afrika zisingekuwa na amani.
Kupitia falsafa ya mfumo wa ujamaa wa Mwalimu Julius Nyerere ulisaidia kusimika mahusiano makubwa yanayotajwa kuwa ni zaidi ya diplomasia pamoja na nchi nyingi za Afrika. Kwa kulithibisha hilo naomba nielezee kwa uchache kuhusu matunda ya falsafa ya ujamaa chini ya Mwalimu Nyerere.
Rejea katika kipindi ambacho nchi nyingi za kiafrika zilikuwa zikipambana kusaka uhuru wake, hali ilikuwa si nzuri kabisa katika baadhi ya nchi pindi linapokuja suala la amani na usalama, hali iliyopelekea hata baadhi ya wanasiasa kuzikimbia nchi zao ili tu kupata hifadhi ya nafsi zao. Kwa wakati huo wanasiasa wengi walichagua Tanzania kama kituo cha amani huku wakiamini ndipo watakapopata msaada na kuungwa mkono katika harakati za uhuru. Wanasiasa kama Nelson Mandela, Sam Nujoma, Samora Machel miongoni mwa wachache waliowahi kufaidika na amani ya Tanzania.
Bila kujali tofauti za ukabila, udini na unchi wanasiasa hao wengi walipata hifadhi nchini na mahitaji mengine na zaidi mpaka kupewa hati ya kusafiria ya kitanzania ili kufanikisha safari zao.
Kwa uchache tu niangazie maeneo mbalimbali yenye historia kubwa kati ya wapigania uhuru waliowahi kupita nchini wakati vuguvugu la utafutaji uhuru likiendelea wakati huo.
Mwalimu Julius Nyerere na Hayati Nelson Mandela ambae baadae alikuja kuwa Rais wa kwanza wa taifa la Afrika Kusini walikuwa na uswahiba mkubwa ulioshibana kiasi cha kuitwa ndugu. Kwa wakati huo chama kisiasa cha Afrika Kusini cha (ANC) kikiwa kinakabiliana vikali na ubaguzi wa rangi uliokuwa umekithiri nchini humo kiliichagua Tanzania kuwa sehemu salama zaidi kwao kujipanga upya na kuleta mageuzi katika mfumo wa kisiasa nchini humo.
Kwa hapa nchini yako maeneo baadhi ambayo wapigania uhuru wa chama cha ANC walipata kukita kambi na hata wengine kuanza maisha mapya wakiwa bado wako hapa nchini.
Eneo kama Dakawa mjini Morogoro lilikuwa likitumika kama makazi ya wapigania uhuru wa chama cha ANC ambapo pia kunapatikana makaburi 50 ya wapigania uhuru wa chama cha ANC waliopoteza maisha wakati wa harakati za uhuru.
Huko Morogoro pia liko eneo la Mazimbu ambapo pia ilikuwa sehemu ya makazi ya wapigania uhuru hao wa chama cha ANC huku kukiwa na makaburi 98 ya wapiganaji wa chama cha ANC ambao walipoteza maisha walihifadhiwa hapo.
Eneo la Mkuyu Handeni mkoani Tanga pia lilikuwa eneo maarufu ambapo kulikuwepo na kituo cha mafunzo ya kijeshi yaliyokuwa yakitolewa kwa wapigania uhuru wa chama cha ANC.
Maeneo hayo machache kati ya mengi yanadhihirisha uswahiba na umoja wa kati ya wanasiasa wa Afrika Kusini na Tanzania.
Hata hivyo pia ukiachana hayo unaweza kuona matunda mbegu za ushirikiano na umoja zilizopandwa wakati huo na waasisi wa vyama na serikali yamekuwa yakifazidisha hata jamii ya sasa.
Mfano, Kufuatia matukio ya majanga yasiyokuwa yakupangwa(Natural disasters) ambayo yalitokea nchini Tanzania miaka kadhaa nyuma serikali ya Afrika Kusini ilisimama kidete na kutoa baadhi ya misaada kwa Tanzania kukabiliana na changamoto hizo.
Hivyo basi maadhimisho ya siku ya ukombozi wa nchi za Afrika ya Kusini ni muhimu kwa Tanzania kwakuwa ni njia ya kuenzi mchango wa mataifa ya SADC katika ukombozi wa bara la Afrika.
Leo Machi 23 ni kumbukizi ya siku ya ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika ambapo nchi jumuiya zinaadhimisha miaka saba tangu jumuiya ya SADC ilipoipitisha siku hiyo kuwa siku rasmi ya kuadhimishwa na nchi jumuiya ya maendeleo Kusini mwa Afrika.
Nihitimishe kwa kuwatakia waafrika wote Kheri ya siku ya ukombozi.
