Mengi yamesemwa katika miezi minane iliyopita juu ya mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Dk. John Pombe Magufuli (JPM) katika ukusanyaji wa kodi.

Mara tu baada ya JPM kuchukua hatamu za uongozi tulishuhudia hatua mbalimbali zikichukuliwa baada ya Serikali hiyo ‘kugundua’ maeneo yaliyokuwa yanasababisha au kuchangia katika uvujaji wa mapato ya Serikali. Ghafla tukaambiwa juu ya makontena lukuki ya bidhaa zilizokuwa zimeondolewa kutoka katika Bandari ya Dar es Salaam na maeneo mengine maalum ya kutunzia mizigo (ICDs) bila kulipiwa ushuru wa forodha na kodi nyingine.

Tuliambiwa pia juu ya meli nyingi zilizowahi kuwasili bandarini, zikateremsha mizigo na kuondoka bila kutozwa hata ‘ndululu’ na Mamlaka ya Bandari kama sheria na taratibu zinavyotaka. Viongozi wakuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Mamlaka ya Bandari (TPA) walivuliwa nyadhifa zao; na muda mfupi baadaye wengine kuteuliwa kushika nyadhifa hizo.

Baada ya hapo kuna kila dalili kwamba ufanisi wa taasisi hizo mbili umekuwa unaongezeka siku hadi siku. Kwa hiyo ni sahihi kabisa kupongeza hatua za awali zilizochukuliwa na Serikali na pia kupongeza viongozi wapya wa taasisi hizo. Hapo juu nimezungumzia juu ya Serikali ya JPM ‘kugundua’ maeneo yaliyokuwa yanasababisha au kuchangia uvujaji wa mapato. Si hilo tu. Serikali mpya ‘iligundua’ pia madudu mengi yaliyofanyika wakati wa Serikali zilizoongozwa na Jakaya Kikwete na watangulizi wake yaliyosababisha udumavu wa maendeleo ya nchi hii. Sina haja ya kuainisha hayo kwa kuwa yameandikwa sana.

Swali ambalo wengi wamejiuliza bila kupata majibu ni je, ni kweli kwamba Serikali iligundua hayo katika muda mfupi tangu iingie madarakani au JPM alipoingia ofisini alikuta majalada yenye taarifa mbalimbali za ‘madudu’ hayo, ambazo zilikuwa hazikufanyiwa kazi na mtangulizi wake na hivyo akaamua kuanza na kazi ya ‘kusafisha meza na makabati?

Au kwa kuwa JPM alikuwa kwenye serikali za awamu mbili zilizomtangulia alikuwa anafahamu ‘madudu’ hayo, lakini alishindwa kushawishi viongozi wa awamu hizo kuchukua hatua stahiki?

 Bahati mbaya hata mimi, kama wengine, sina majibu ya maswali hayo. Itoshe kusema kwamba hata kama tumechelewa miaka 10 au 20, hatuna budi kufarijika kwamba angalau hatua zimeanza kuchukuliwa.

Hata hivyo, kama wengi tunavyojua, HAPA KAZI BADO, tena sana! Maeneo mengi, ikiwa ni pamoja na kashfa mbalimbali zilizotikisa taifa hili wakati wa awamu zilizopita na bado hayajashughulikiwa. Vyombo vingi vya habari, hususan magazeti, havichoki kukumbusha viongozi (au watawala?) wetu juu ya ulazima wa kuchukua hatua stahiki juu ya maovu yote yaliyofanyika au yanayoendelea kufanyika, tena baadhi ya maovu hayo yakiwa mazito zaidi kuliko yale yaliyoshughulikiwa hadi sasa. Hiyo ni ‘selective justice’ kwa wananchi ambao ndio waathiriwa wa maovu hayo. Au labda ni vema tuanze mchakato wa kujitazama kama Taifa, tuzungumze kwa uwazi yote yaliyotokea ya kuteteresha uchumi na mustakabali wa Taifa hili na hatimaye tufanye maridhiano na kusameheana kama walivyofanya wenzetu wa Afrika Kusini?

Kwa kuwa mada hii inajikita katika kuangalia machache ya hayo yaliyotokea katika TRA katika miaka 20 tangu ianze kufanya kazi Julai 1996 na uhusika wa viongozi katika kuathiri utendaji wake, nitaanza kwa kutoa mfano ‘ulio hai’ wa jipu ambalo nilitarajia kuwa miongoni mwa ‘majipu’ ya kwanza kutumbuliwa.

Kuna kampuni moja ambayo kwa takriban miaka 10 ilishikilia eneo moja nyeti la uchumi wa nchi yetu. Kampuni hiyo ilihodhi kwa kiasi cha kutisha biashara ya kuingiza bidhaa nchini kutoka nje bila kulipa kodi kwa thamani na viwango vinavyotakiwa. Si tu kwamba ilikuwa inaagiza bidhaa nyingi na kuziuza kwa bei nafuu, bali iliwalazimisha waagizaji wengine kupitisha bidhaa zao mikononi mwake kama walitaka kuendelea na biashara.

Wale waliokataa kutumia huduma ovu za kampuni hiyo walijikuta wakitozwa na TRA ushuru na kodi mbalimbali kwa viwango vinavyotakiwa au vya juu zaidi na hivyo kujikuta wakishindwa kuendelea na biashara.

Wale waliokubali kupitisha bidhaa zao kwenye kampuni hiyo, walifaidika na mtandao wake wa ufisadi kwa kulipa kodi kidogo au kutolipa kabisa na hivyo kuweza kuuza bidhaa zao sokoni kwa bei nafuu pia. Mengi yamesemwa na kuandikwa juu ya kampuni hiyo. Miongoni mwa hayo ni kwamba kampuni hiyo likuwa na mtandao mpana. Watumishi wa kampuni pamoja na viongozi wao walikuwa ‘hawagusiki’.

Aidha, kuna madai kwamba kampuni hiyo ilikuwa na ratiba maalumu ya kutembeza mgao wa fedha kwa wafadhili wake. Ilisemekana kwamba wale waliotaka mgao wao katika fedha za kigeni, kampuni ilitekeleza matakwa yao. Baadhi ya majengo mithili ya mahekalu na nyumba za kupanga, hususan ‘apartments’ tunazoona Dar es Salaam na kwingineko nchini yanasemekana kujengwa na fedha kutokana na bakhshish zilizolipwa na kampuni hiyo.

Mara tu baada ya Serikali ya Awamu ya Tano kuingia madarakani, kampuni hiyo ilitangaza kuwa imefilisika! Sina taarifa yoyote kwamba Serikali mpya ililifahamu au inalifahamu hili na iwapo kuna hatua zilizochukuliwa au zilizoko mbioni kuchukuliwa juu ya kampuni hiyo ‘mufilisi’ na wote; na nina maana ya wote, waliohusika katika kashfa hii ya kampuni binafsi kutoza waagizaji wa bidhaa kodi na kuamua ni kiasi gani kiingie kwenye mfuko wa Serikali huku sehemu kubwa ikibaki kwake na mafisadi wengine walioitwa viongozi wa umma!

Iwapo iliweza kupitisha bandarini mizigo ya watu wengine kwa kulipa kodi kiduchu, ni dhahiri kwamba mizigo yake yenyewe ilikuwa inapita bila kulipiwa na kama ililipiwa, ni wao walioamua kiasi cha kulipa.

Kama nilivyogusia hapo juu, Juni mwaka huu TRA ilitimiza miaka 20 tangu ianze kazi rasmi. Historia inaonesha kwamba mwaka 1995, Serikali ilifanya uamuzi wa kuanzisha TRA. Uamuzi huo ulitokana na mapendekezo ya Tume ya Rais ya Kuchambua Mfumo wa Mapato na Matumizi ya Serikali (MTEI COMMISSION) iliyoundwa na Mzee Mwinyi mwaka 1989.

Ni Tume hiyo hiyo liyopendekeza, pamoja na mambo mengine mengi, uanzishwaji wa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT). Nilibahatika kuwa kwenye Sekretariati ya Tume ile kama nilivyobahatika kuwa mtu wa kwanza kuteuliwa na Serikali kuandaa uanzishwaji rasmi wa TRA baada ya sheria husika kupitishwa na Bunge.

Uamuzi wa kuondoa utawala na ukusanyaji wa kodi kutoka kwenye mfumo wa utumishi wa umma (civil service) ulikuwa na sababu mbili kuu.

Mosi, kutokana na uwezo mdogo wa kulipa watumishi wa umma vizuri na kuwapatia vitendea kazi vya kutosha, Serikali ilikubali pendekezo la Tume ile kuanzisha mamlaka inayojitegemea na kuipatia nyenzo za kutosha na pia kuwalipa watumishi wake vizuri kwa matumaini kwamba kwa kufanya hivyo, mamlaka hiyo ingeweza kukusanya kodi kwa ufanisi zaidi ili kuiwezesha Serikali kukidhi kwa kiasi kikubwa, matumizi ya Serikali.

Ilitarajiwa pia kuwa kwa kufanya hivyo, watumishi waliobaki kwenye mfumo wa kawaida wa utumishi nao wangeweza kuongezewa mishahara kadri mapato yalivyoongezeka ili nao wafanye kazi kwa ufanisi zaidi. Aidha, Tume ya Rais ilikuwa imeshauri kwamba mamlaka hiyo ingekuwa na uhuru zaidi wa kuajiri wataalamu kwa ajili ya kuongeza ufanisi, huku ikiwa pia na uhuru wa kuondoa watumishi wasiofaa kwa urahisi zaidi tofauti na serikalini ambako kulikuwa na urasimu.

Mara baada ya sheria hiyo namba 11 ya mwaka 1995 kuridhiwa na Rais mnano Julai 31, 1995, Bodi ya Wakurugenzi ya kwanza chini ya Gavana wa sasa wa Benki Kuu (BoT), Profesa Benno Ndulu, iliundwa na kuanza kazi mara moja; mimi nikiwa Katibu wa Bodi hiyo. Miongoni mwa uamuzi muhimu wa kwanza wa Bodi ni ule wa kuacha, kwa kipindi cha mwaka wa kwanza, idara za kodi zilizokuwapo ziendelee na kazi chini ya mfumo na taratibu zilizokuwapo huku Bodi ikijikita kwenye kazi ya kuandaa mfumo na taratibu mpya ambazo zingeongoza chombo hicho kipya. Kwa maana nyingine, Bodi haikuona faida yoyote katika kurithi idara zilizokuwapo na taratibu na mifumo yake. Kufanya hivyo ingelikuwa ni sawa na kuweka mvinyo mpya katika chupa ya zamani. Kadri Bodi ilivyoendelea kutengeneza mifumo na taratibu mpya, ilifanya uamuzi muhimu ufuatayo:

Wafanyakazi wa chombo kipya (TRA) wangetokana na watumishi waliokuwa katika idara za kodi hizo hizo, yaani Idara ya Ushuru wa Forodha na Kodi ya Mauzo na Idara ya Kodi ya Mapato. Hata hivyo, iliamuriwa kuwa siyo wote wangechukuliwa. Ni wale tu ambao wangehakikiwa na kuonekana hawana matatizo ya kiutendaji na kimaadili ndio wangechukuliwa.

Kwa hiyo ulipofika wakati mwafaka na baada ya uchunguzi wa ndani, mamia ya watumishi katika idara hizo waliondolewa kazini kabla TRA haijazinduliwa rasmi. Kundi la pili la watumishi wa idara hizo liliondolewa baada ya uchunguzi wa kina uliofanywa na Bodi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya Serikali. Kwa maana hiyo, TRA ilipoanza kazi Julai mosi, 1996 ilianza kazi bila kuwa na ‘mzigo’ wa wafanyakazi ambao uadilifu wao ulikuwa wa shaka (doubtful integrity).

Wakuu wa idara zote katika TRA pamoja na manaibu wao, ikiwa ni pamoja na wale wa idara mpya za sheria, utumishi na fedha, ukaguzi wa ndani, utafiti na sera, n.k wangeajiriwa baada ya kudahiliwa na kuonekana wanafaa siyo tu katika utendaji kazi, bali pia kwa upande wa maadili.

Ili kuhakikisha kwamba chombo hicho kingeongozwa na watumishi wenye sifa hizo, iliamuriwa kwamba nafasi zote za wakuu wa idara na manaibu wao zingetangazwa na wale ambao wangefaulu wangefanya kazi kwa mkataba wa miaka mitatu mitatu ili kuhakikisha kwamba wanaendelea na sifa zilizowawezesha kuajiriwa.

Uamuzi mwingine muhimu uliofanywa na bodi kabla ya TRA kuanza kazi rasmi ni ule wa kuweka MASHARTI YA MAADILI (Code of Conduct) yaliyombana kila mfanyakazi. Kila mmoja alitakiwa kujaza fomu na kuorodhesha mali zake zote wakati wa kuingia TRA na kila mwaka baada ya hapo. Hii ilikuwa nguzo muhimu kuliko zote katika utendaji kazi wa watumishi wote. Nakumbuka kwamba kati ya mwaka 1996 na 2003 watumishi walio wengi waliheshimu na kufuata maadili ya kazi na hicho ndicho kilikuwa chanzo cha mafanikio tuliyoyashuhudia katika ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali.

Hata hivyo, kama nilivyowahi kuandika mwaka 2006, nakisi katika maadili ya utumishi wa umma kwa ngazi zote iliwafanya watumishi wa TRA kuanza kulegea na hatimaye ‘kuanguka’ kwani katika mazingira kama hayo wasingeweza kuwa ‘watakatifu kumzidi Papa’.

Pamoja na hayo ni lazima nikiri kwamba hata kufifia kwa maadili ya watumishi wa umma katika Serikali nzima haukutokana na kukosa ‘code of conduct’.  Viongozi wa juu hasa wale wa kisiasa walikuwa chanzo kikuu cha uozo katika utumishi wa umma. Nitatoa mifano michache ya mambo niliyoyashuhudia mimi binafsi.

Mwaka 1992 nikiwa Mkuu wa Kitengo cha Kuzuia Dawa za Kulevya katika Idara ya Forodha tulifanikiwa kukamata kontena la futi 20 lililojaa dawa za kulevya. Enzi hizo kazi hiyo ilikuwa jukumu la Idara ya Forodha ingawa tulishirikiana na Jeshi la Polisi katika operesheni kubwa. Baada ya kukamatwa katika Bandari ya Dar es Salaam, kontena hilo lilihifadhiwa kwenye bohari la Mamlaka ya Tumbaku Kurasini. Bohari lilifungwa na funguo kuwekwa katika mikono salama huku askari wa FFU wakililinda.

Siku konteina lilipofunguliwa kwa ajili ya Jaji aliyekuwa anasikiliza kesi dhidi ya watuhumiwa wa kuliingiza nchini ili kuona vielelezo, iligundulika kwamba kontena lilikuwa limekatwa sehemu ya juu na dawa kuondolewa. Baada ya dawa kutolewa, sehemu iliyokatwa bati lake lilichomelewa upya. Hadi leo hakuna mtu yeyote aliyewahi kukamatwa kwa uhalifu huo uliofanyika ‘chini ya ulinzi wa FFU’.

Wakati tunapeleleza jinsi kontena hilo lilivyoingia nchini tulipata taarifa za kuaminika kuwa kontena la pili lilikuwa limeteremshwa kwenye Bandari ya Zanzibar.

Niliamua kwenda mwenyewe kufuatilia taarifa hizo. Baada ya kufanya kazi hiyo kwa siku kadhaa huku nikichunguza pia juu ya upatikanaji na matumizi ya dawa za kulevya Kisiwani humo, ilitolewa amri ‘kutoka juu’ kwamba niondoke Zanzibar katika muda wa saa tatu na nisirudi wakati wowote ‘bila kuomba na kupata kibali kutoka juu’.

Aliyenijulisha uamuzi huo wa Serikali alikuwa ni Waziri wa Fedha wa wakati huo. Ilikuja kufahamika kuwa ni vinara wa uingizaji wa dawa za kulevya ndio walijenga hoja iliyosababisha nifukuzwe mithili ya prohibited immigrant!

Mwaka 1993 nikiwa Kaimu Kamishna wa Upelelezi na Uzuiaji wa Magendo katika Idara hiyo hiyo niliamua kukagua viwanda vya wafanyabiashara waliokuwa wanaingiza walichoita mafuta ghafi ya kula ili kuhakiki iwapo walikuwa na mitambo ya kusindika mafuta hayo.

Nilitaka kufanya hivyo ili kulinda mapato ya Serikali kwa vile kwa muda mrefu mafuta ghafi yalikuwa hayatozwi ushuru wa forodha wala kodi ya mauzo. Tuliamini kuwa wafanyabiashara hao walikuwa wanaingiza mafuta yaliyokuwa yamesindikwa, lakini ili kukwepa kulipa kodi waliamua kuyaingiza kama mafuta ghafi. Siku tulipokwenda kukagua kiwanda cha kwanza, tulicheleweshwa mlangoni wakati walinzi wakiwasiliana na wenye kiwanda.

Baada ya muda kupita huku tukisubiri, tuliitwa sehemu ya mapokezi ambako niliombwa kuzungumza na mtu aliyekuwa anasubiri kwenye ‘line’. Huyo hakuwa mwingine, bali Kamishna wangu ambaye aliniamuru kusitisha zoezi hilo (kazi hiyo) baada ya kupokea maelekezo kutoka ofisi ya Waziri Mkuu.

Tukio lingine katika mwaka huo huo ni pale nilipoamuriwa na kiongozi mwandamizi katika Wizara ya Fedha kuacha kufuatilia ulipwaji wa kodi kwenye kiasi kikubwa cha bia aina ya Stella Artois iliyokuwa imeingia nchini; na Waziri wa Fedha kuamua kwamba waingizaji wangelipa kodi husika kwa awamu (installments); uamuzi ambao ulikuwa kinyume cha sheria.

Kila mzigo mpya ulipofika nchini, kilitoka kibali kipya chenye masharti yale yale hata kama hakuna kodi iliyokwishakulipwa kwa mzigo uliotangulia. Nilipomwambia kiongozi huyo kuwa kufuatilia ulipwaji wa kodi hizo lilikuwa ni jukumu langu, alinitajia jina la mke wa kiongozi serikalini kuwa ndiye alikuwa anahusika na uingizwaji wa bidhaa hiyo. Nilipodadisi zaidi sababu za kunitaka nisitekeleze wajibu wangu, nilifukuzwa ofisini kwake na baada ya muda mfupi nilijikuta nashushwa cheo na kuhamishiwa mkoani Mwanza!

Hayo ni ya huko nyuma, lakini ni vielelezo vinavyothibitisha uhusika wa viongozi wa ngazi za juu serikalini na hata kwenye chama tawala katika kushuka kwa maadili ya watumishi wanaohusika na ukusanyaji kodi na wale wa umma kwa ujumla wao.

Mmomonyoko wa uadilifu katika utendaji kazi ndani ya TRA ulishika kasi baada ya Kamishna Mkuu wa kwanza kuondolewa kwa manufaa ya walafi. Hiyo ilikuwa mwaka 2003. Hata hivyo, mbegu za mmomonyoko huo zilianza kupandwa baada ya ujio wa Mwenyekiti wa Pili wa Bodi ya Wakurugenzi uliofuatiwa kwa karibu na mabadiliko ya mawaziri katika Wizara ya Fedha. Wote wawili walianza kukiuka misingi ya kazi iliyokuwa imewekwa na Bodi ya kwanza.

Misingi hiyo ndiyo ilikuwa nguzo ya ufanisi katika utendaji wa TRA kati ya mwaka 1996 na 2003. Pamoja na kwamba sheria iliyoanzisha TRA ilikuwa inatambua madaraka ya Waziri wa Fedha juu ya Bodi na watendaji wakuu wa TRA, mawaziri wa fedha waliokuwapo wakati TRA inaanzishwa hadi kuanza kufanya kazi waliheshimu mipaka ya kazi iliyokuwa imeainishwa kwa kuwa walikuwa wameidhinisha wenyewe. Mwenyekiti wa Bodi aliyeingia madarakani mwaka 1998 alitoka serikalini na alianza kulazimisha Bodi kubadili baadhi ya uamuzi wa Bodi ya kwanza. Alikuja na hoja za usawa wa jinsia na hata ukabila katika ajira bila kujali uwezo – na hilo lilianza kuathiri utendaji katika ukusanyaji mapato ya Serikali.

Aidha, alikiuka baadhi ya taratibu za kiutendaji kwa kushughulika na walipa kodi yeye mwenyewe huku akitoa maelekezo kwa Kamishna Mkuu juu ya viwango vya kodi vya kutoza wafanyabiashara hao. Kwa kufanya hivyo alikuwa anakiuka sheria ya TRA ambayo inakataza Bodi kuingilia kazi za ukadiriaji na ukusanyaji kodi.

Hakuishia hapo. Ilifika wakati akaanza kuongoza timu za wapelelezi wa kodi kufanya doria mchana na usiku ili kukamata bidhaa za magendo au wakwepakodi. Tuliomuonya juu ya ukiukwaji huo wa sheria ‘tulilipwa’ kama alivyoona inafaa.

Kwa ujumla, Mwenyekiti huyo alishirikiana na Waziri wa Fedha wa wakati huo katika kukanyaga msingi imara uliokuwa umejengwa na Bodi ya kwanza pamoja na Waziri aliyekuwapo wakati huo. Wote wawili walishirikiana kuweka viongozi waliotaka na ambao wangetii maagizo yao bila kuhoji. Wigo wa fungate hilo la viongozi wapya wa TRA na wale wa wizara liliendelea kupanuka hadi kwenye ngazi za juu za uongozi wa nchi, huku wakiingiza pia viongozi wa idara nyeti kama Takukuru na Usalama wa Taifa.

Kutokana hali hiyo, ilifika wakati ambako viongozi wa TRA walifanya wanalotaka wakijua kuwa hakuna mamlaka yoyote inayoweza kuwauliza; achilia mbali kuwawajibisha. Matunda ya hali hiyo ni pamoja na madudu machache sana yaliyoibuliwa na Serikali mwanzo kabisa wa Awamu hii ya uongozi wa nchi hii.

Kwa hiyoTRA chini ya uongozi wake mpya inaposherehekea(?) kutimiza miaka 20 tangu ianze kazi rasmi inahitajika kuangalia misingi na sababu za mafanikio yake katika miaka ya kwanza ya uhai wake na kuiboresha kwa ajili ya kupata ufanisi zaidi.

 

Mushengezi Nyambele, kitaaluma ni Mwanasheria na Mtaalamu wa Kodi. Alishiriki kuanzisha Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mwaka 1996 na kushika wadhifa wa Katibu wa Bodi na Mshauri Mkuu wa Sheria. Anapatikana kupitia simu: 0764 501 264