Desemba mwaka jana baadhi ya wapenzi na mashabiki wa wanamuziki Tabu Ley na Pepe Kalle walifanya kumbukizi ya wanamuziki hao.
Ikumbukwe kuwa kifo cha Pepe Kalle kilitokea Novemba, 1998 wakati Tabu Ley alifariki dunia Desemba 2013, kutokana na mshtuko wa moyo kwenye Hospitali ya Ngaliema jijini Kinshasa.
Kwakuwa wasifu wa nguli hawa ni mrefu sana, safu hii leo inamzungumzia marehemu Pepe Kalle, aliyezaliwa Novemba 30, 1951. Alikuwa mwimbaji wa Soukous, mwanamuziki na kiongozi wa bendi kutoka nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Pepe Kalle mara baada ya kuzaliwa katika mji mkuu wa Kinshasa (wakati huo mji huu ulikuwa unajulikana kama Léopoldville), alipewa majina ya Kabasele Yampanya. Lakini baadaye aliamua kulichukua jina la mshauri wake, Grand Pepe Kalle. Mwanamuziki huyu (Pepe Kalle) alikuwa jitu la miraba minne.
Pepe Kalle alikuwa na uwezo wa kuimba kwa sauti ya juu zaidi pamoja na sauti ya chini zaidi ambayo kwa lugha ya ‘kimombo’ inaitwa ‘Multi-Octave range’.
Alikuwa mtunzi, mwimbaji wa muziki wa Soukous na kiongozi wa bendi ya Empire Bakuba. Umbo lake kubwa lilikuwa limebeba uzito wa kilo 136 na urefu wake ulikuwa sentimeta 190, ambazo ni sawa na futi sita na inchi tatu.
Pepe Kalle alikuwa bingwa wa miondoko ya Soukous na kiongozi wa bendi ya Empire Bakuba, ambayo ilikuwa maarufu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Sauti yake nyembamba iliyokuwa na uwezo mkubwa wa kughani, alikuwa ana uwezo mkubwa wa kucheza jukwaani akitikisa umbo lake licha ya kuwa na uzito mkubwa.
Watanzania wengi tutaendelea kumkumbuka mwanamuziki huyu hasa wakati alipokuja nchini mwetu na kutikisa majiji ya Arusha, Dar es Salaam na Mbeya.
Wakati wa ujio wake hapa Tanzania, Pepe Kalle ambaye sauti yake ilikuwa nyembamba na nyororo, alifuatana na wanamuziki wengine akiwemo mpiga gitaa la besi, Lofombo na waimbaji kina Papy Tax, Dilu Dilumona na Djo Djo Ikomo.
Rapa wake mahiri na kiongozi wa wacheza shoo, Bileku Mpasi na mbilikimo wawili, Emoro na Jolly Bebbe, walitoa burudani tosha kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam mwaka 1991. Mwaka uliofuata wa 1992, Emoro alifariki dunia akiwa na bendi yake nje ya nchi kwa safari ya kikazi ya muziki.
‘Kizuri huigwa’, usemi huo ulijionyesha dhahiri baada ya msanii mmoja aliyejulikana kwa jina la Kokoriko, kuweza kuiga miondoko ya uchezaji wa Bileku Mpasi. Msanii huyo alipachikwa jina la Bileku Mpasi wa Tanzania.
Pepe wakati wa uhai wake alirekodi nyimbo zaidi ya 300 na kufyatua albamu 20 katika miongo miwili ya muziki wake na alijulikana kama ‘Tembo wa Afrika’.
Historia yake katika muziki inaeleza kwamba alianza muziki rasmi katika bendi ya Afrikan Jazz ya baba yake mzazi, Joseph Kabasele ‘Grand Kalle’ aliyemtengeneza mwanaye huyo.
Baada ya kukomaa kimuziki akatimka na kwenda kujiunga na bendi ya Lipua Lipua iliyokuwa ikimilikiwa na Kiamunagana Mateta Wanzo la Mbonga ‘Verkeis’, alipotua Lipua Lipua, haikuchukua kipindi kirefu akafanywa kuwa mwimbaji kiongozi akishirikiana na mwimbaji mwingine Nyboma Mwandido.
Safari yake katika muziki haikuishia hapo kwani mwaka 1973 Pepe Kalle akiwa na Dilu Dilumona na Papy Tax waliondoka katika bendi hiyo na kuunda bendi yao iliyopewa jina la Empire Bakuba.
Jina la Empire Bakuba lilitokana na mashujaa wapiganaji wa makabila ya Kongo.
Kama wanamuziki wengine, Pepe Kalle aliwashirikisha wanamuziki wengine wakongwe katika tasnia ya muziki kina Simaro Lutumba na Nyoka Longo.
Bendi hiyo ya Empire Bakuba ilitoweka katika sura ya muziki baada ya kifo cha kiongozi wake Pepe Kalle.
Watanzania tutaendelea kumkumbuka Pepe Kalle ambaye alipotua Tanzania alitunga nyimbo kupitia lugha ya Kiswahili, za Yanga Afrika, akiisifia Klabu ya Yanga, wimbo uliokuwa ukimtaja mfadhili wa klabu hiyo, Abbas Gulamali.
Vilevile aliimba wimbo wa ‘Hidaya’, alioimba akilalamika kupoteza mkanda wake wa kiuno na wimbo wa ‘Mpenzi Bupe’, alioutunga alipotoka jijini Mbeya kufanya onyesho.