Mkoa wa Tabora unaongoza mikoa ya kanda ya kati kwa Tanzania Bara kwa uwiano mkubwa kati ya wakazi wa mkoa huo na laini za simu zilizosajiliwa, kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni za mawasiliano nchini.
Meneja mkuu wa kanda ya kati, Boniface Shoo alitoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza katika kikao cha wadau wa sekta ya mawasiliano kilichofanyika katika ukumbi wa Isike Mwanakiyungi mkoani Tabora
Amesema kwamba hadi kufikia Juni 2022 laini 3,000,849 za simu zilikuwa zimesajiliwa mkoa wa Tabora, wenye wakazi wanaokadiriwa kuwa zaidi ya milioni mbili.
Shoo amesema kwamba takwimu hizo za kila robo ya mwaka zilizotolewa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), zinaonyesha kwamba Dodoma ni ya pili kwa wingi wa laini zilizosajiliwa kwa kanda ya kati ikiwa na laini 2,864,302.
Aidha takwimu hizo zinaonyesha kwamba jumla ya laini 56,153,097 zilikuwa zimesajiliwa hadi Juni 2022 kwa nchi nzima; huku mikoa 10 ikisajili zaidi ya laini milioni mbili kila mmoja.
Shoo amesema kwamba Idadi ya laini zilizosajiliwa katika mikoa hiyo ni Tabora 3,000,849, Kigoma 1,257,318, Singida 1,397,359 na Dodoma 2,864,302.
Hata hivyo amesema kwamba ni vyema ifahamike kwamba idadi ya laini zilizosajiliwa hailingani na idadi ya watumiaji, ambao ni wachache zaidi kwa kuwa kuna watu wenye laini zaidi ya moja.
Amesema kwamba kanuni zinaruhusu mtu kusajili hadi laini tano (5) kwa matumizi mbalimbali, kwa mfano intaneti.
Amesema kwamba kuna sababu nyingi zinazofanya watu kuwa na zaidi ya laini moja ,ikiwemo kutokupatikana huduma za mtandao husika eneo fulani au utaratibu wa baadhi ya ofisi ambamo watumishi wanapewa namba za kazini na wanakuwa na zao binafsi.