Na Benny Kingson, JamhuriMedia, Tabora
Milioni 25,600,000 zimetolewa kwa timu ya Tabora United ‘Nyuki wa Tabora – Wana Unyanyembe’ baada ya kuichapa Yanga mabao 3-1 wiki iliyopita kwenye mchezo wa Ligi Kuu uliochezwa kwenye uwanja wa Azam Complex Chamazi jijini Dar es Salaam.
Donge hilo nono lilitolewa kwa timu hiyo kwenye hafla maalum iliyoandaliwa na ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora iliyofanyika kwenye hoteli ya Tabora Orion mjini hapo mbapo pia ulifanyika uzinduzi wa jezi mpya za kisasa, basi jipya la kisasa lenye choo ndani pamoja na kufanyia maombi vifaa hivyo na timu nzima.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora Paul Chacha amekabidhi timu hiyo sh.milioni 20 taslimu na sh.milioni 5,600,00 zilikuwa ahadi ambapo kati yake sh. milioni 4, 200,000 zilitolewa na mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kutoka Mkoa wa Tabora MNEC Mohamed Naassoro na sh.milioni 1,400,000 zilitolewa na Meneja Biashara wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mkoa wa Tabora (TUWASA), Bernad Biswalo.
Mjumbe huyo wa CCM ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Mabasi NBS mjini Tabora maarufu kama ‘Meddy’ amesema atakuwa anatoa sh.600,000 kila mwezi kwa kipindi cha miezi saba kwa timu hiyo na Biswalo sh.200,000 kila mwezi ili kuisaidia na kuwapa molali wachezaji.
Meddy amesema nyuki hao kwa kuwashambulia Yanga na kuwaadhibu kumeleta heshima Tabora na hamasa kubwa kwa wadau wa maendeleo kutaka kuja Tabora kuwekeza na kwamba CCM imejipanga kuweka taa, nyasi bandia, vitega uchumi na kuukamilisha uwanja wa Ally Hassan Mwinyi kwa kuthamini mchango wa timu hiyo.
Mkuu wa Mkoa akitoa hotuba yake amesema wataendelea kutoa huduma bora kwa mashujaa hao na kwamba viongozi wa dini na wazee wa Tabora wataiombea zaidi dua iendelee kufanya vizuri zaidi katika michezo mingine inayofuata.
Chacha amewaasa wachezaji wa timu hiyo kutambua kuwa mpira ni ajira yao inayowapatia vipato halali na kwamna Serikali, wadau na wananchi watawaunga mkono kwa hali na mali kuhakikisha wanatimiza majukumu yao na kufanikisha malengo yaliyokusidiwa.
“Timu hii inaongozwa vema kwa nidhamu, heshima na kuhakikisha usalama wao popote watakapokuwa, nataka ulevi, jeuri na kiburi visiwepo kwenu, mfanye mazoezi na kutimiza majukumu yenu, tutawapatia stahiki zenu zote kwa wakati, chakula, posho na mengine”amesema.
Amewaahidi nyuki hao kuwapa sh.milioni 50 endapo timu hiyo itaifunga Simba na atatoa sh.miloni 200 wakifanikiwa kumaliza ligi na kushika nafasi ya tatu ambapo ataendelea kutoa sh milioni 10 kwa kila mchezo watakaoshinda ama kutoa sare.
Hafla ya kuipongeza timu hiyo ilitanguliwa na kufanyika kwa matendo ya huruma kwa jamii kwa kutoa na kuchangia damu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora Kitete, kutoa misaada ya vitu mbalimbali vikiwemo vyakula kwenye kituo cha watoto yatima cha Upendo cha Kanisa Katoliki na cha Igambilo cha akina mama wa Kiislamu.