Na Allan Vicent, JamhuriMedia,Tabora  

TIMU ya soka ya Tabora United ya Mkoani Tabora imezawadiwa kitita cha sh mil 50 baada ya kufanikiwa kubakia Ligi Kuu ya NBC msimu huu kama motisha kwa wachezaji na walimu wao.

Kitita hicho kimekabidhiwa jana na Mkuu wa Mkoa huo Paul Matiko Chacha kwa wachezaji na viongozi wa timu hiyo ikiwa ni utekelezaji wa ahadi aliyotoa kwa timu hiyo kama itafanya vizuri katika michezo ya mtoano na kubakia ligi kuu.

Alisema kuwa katika mchezo wa awali Tabora United ilifungwa goli 1-0 na Biashara United lakini katika mchezo wa marudiano ikashinda 2-0 hivyo kurejesha furaha na shangwe kwa wakazi wa Tabora baada ya kufanikiwa kubakia ligi kuu.

Akizungumza katika hafla hiyo RC Chacha amewapongeza Viongozi, Kocha na Wachezaji kwa kushikamana na kupambana ipasavyo katika michezo yao na hatimaye kufanya vizuri.

‘Fedha hizi zimetolewa na mashabiki na wadau mbalimbali wa soka ndani na nje ya Mkoa kama motisha kwa wachezaji na viongozi na kubainisha kuwa msimu ujao timu hiyo anataka timu hiyo iwe moto wa kuotea mbali’, alisema.

Kuelekea msimu mpya wa ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara itakayoanza kutimua vumbo mwishoni mwa mwezi Agosti, RC Chacha aliwataka wachezaji wa timu hiyo kubadilika kiuchezaji na kuwa na nidhamu ya hali ya juu ili wafanye vizuri.

Naye Mwenyekiti wa Timu ambaye ni Kamanda wa Polisi Mkoani hapa Richard Abwao alimshukuru Mkuu wa Mkoa kwa hamasa yake kubwa ambayo imewezesha timu hiyo kubakia ligi kuu.

Alimhakikishia kuwa msimu ujao timu yao itakuwa na mabadiliko makubwa na itakuwa miongoni mwa timu bora na tishio za ligi kuu.

Nahodha wa timu hiyo Saidi Mbatty alishukuru serikali ya Mkoa, wadau na mashabiki wote kwa kuipigania timu hiyo ili isishuke daraja, alibainisha kuwa kama sio wao kamwe wasingerudi ligi kuu.

Mstahiki Meya wa halmashauri ya manispaa ya Tabora Ramadhan Kapela alimhakikishia Mkuu wa Mkoa kuwa kikosi chao msimu ujao hakitakuwa cha kitoto, watafanya usajili wa nguvu utakaozitetemesha hata  Simba na Yanga.

Please follow and like us:
Pin Share