Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imetoa wito kwa wananchi na wapiga kura wa mkoa wa Tabora kujitokeza kwa wingi kujiandikisha na kuboresha taarifa zao kwenye uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura unaotarajiwa kufanyika kwenye mikoa hiyo kuanzia Julai 20 hadi 26,2024.
Akifungua mkutano wa wadau wa uchaguzi mkoani Tabora, leo Julai 8, 2024, Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Jaji Jacobs Mwambegele amesema uboreshaji huO unamhusu kila mwananchi mwenye sifa ya kuandikishwa kuwa Mpiga Kura.
“Ni vyema mkatambua kuwa uboreshaji huu unamhusu kila mwananchi mwenye sifa ya kuandikishwa kuwa mpiga kura na anayeboresha taarifa zake. Hivyo, natoa rai kwenu kuwahimiza wananchi kupitia majukwaa yenu ya kisiasa, kijamii, kitamaduni, kiimani na kiuchumi wajitokeze kwa wingi kujiandikisha na kuboresha taarifa zao kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura,” amesema Jaji Mwambegele.
Pia amesema kila chama cha siasa kimepewa nakala ya orodha ya vituo vyote vya kuandikisha wapiga kura. Dhumuni la kuwapatia nakala hizo ni kuwawezesha kupanga na kuweka mawakala wa uandikishaji katika vituo vya kuandikisha wapiga kura.
“Kila chama kitaruhusiwa kuweka wakala mmoja kwenye kituo cha kuandikisha wapiga kura kwa lengo la kushuhudia utekelezaji wa zoezi la uboreshaji kituoni ikiwemo kuwatambua wale wanaokuja kituoni kama wana sifa za kuandikishwa,” amesema Jaji Mwambegele.
Jaji Mwambegele alitoa angalizo kwa wadau wa uchaguzi kwa umoja wao kuzingatia sheria za uchaguzi, kanuni za uboreshaji na maelekezo ya Tume kuhusu uboreshaji wa daftari, huku akisema Tume kwa upande wake itazingatia Katiba, sheria ya uchaguzi na kanuni zilizotungwa chini ya sheria katika uboreshaji.