Na Happy Lazaro, JamhuriMesia, Arusha
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha Ilvin Mugeta amesema kuwa taasisi za haki jinai na madai zinahitaji mabadiliko na mageuzi makubwa katika utekelezaji wa majukumu yao Ili kurudi katika misingi ya kusaidia wananchi katika upatikanaji wa haki bila vurugu.
Amesema kuwa taasisi hizo ni muhimu kuzingatia Sheria kanuni na taratibu za kisheria katika utekelezaji wa majukumu yao ya kuhakikisha upatikanaji wa haki bora na kwa wakati.
Jaji Mugeta ameyasema hayo leo, Februari 3,2025 kwenye kilele cha maadhimisho ya wiki ya Sheria nchini iliyofanyika kikanda Mkoani Arusha katika viwanja vya mahakama kuu Arusha.
Jaji Mugeta amesema, mabadiliko yanayohitajika, taasisi zinazohusika na haki ni kuvaa jukumu la kuelimisha jamii kuhusu haki zao pamoja na Sheria zinazowalinda Ili kuwapa uwezo wa kudai haki zao.
“Nikisema hivyo namaanisha, tuache tabia ya kuvizia wananchi wakosee Ili waadhibiwe bila kuelimishwa juu ya wajibu na haki zao kwani hazisaidii kujenga jamii inayojiheshimu” amesema.
Zaidi amezitaka taasisi hizo kuweka mifumo imara ya kisheria ya utoaji huduma ndani ya kila taasisi tena iliyo thabiti na wa haki kwa uwazi unaoeleweka ili kuepusha matumizi ya utashi kwenye kufanya maamuzi.
Haya ni mambo ya msingi katika maendeleo ya dira na kamwe tusiendelee kudhani utoaji wa haki si sehemu ya maendeleo endelevu
Kwani haki ndio msingi wa maendeleo” amesema na kuongeza;
“Haki inayopatikana kwa wakati hupunguza migogoro na kuachilia rasilimali zilizofungwa Ili ziingie kwenye mnyororo wa uzalishaji mali” .
Amesema kuwa katika rasimu ya dira ya taifa ya mwaka 2050 inataka kuwe na Taifa moja kama Jamhuri ya Muungano yenye jamii inayothamini utu, haki, Uhuru na Demokrasia na Taifa ambalo linasimamia rasilimali za nchi na kuimarisha utamaduni na tunu za Taifa.
“Katika kuyafikia haya, taasisi za haki madai zitahusika kusimamia eneo la utawala Bora, haki jamii, Uhuru na Demokrasia, tena wenye ufanisi katika kutazama haki za binadamu na usawa mbele za Sheria sambamba na usawa mbele ya utoaji haki madai kwa wananchi Ili kufikia jamii isiyo na vurugu wala ukatili” amesema na kuongeza;
“Ukimuuliza Mtanzania yoyote anataka nini kwenye taasisi za haki madai, atakuambia anataka huduma bora, ya haraka na kwa heshima, ndio hitaji lake na hapo ndio mtihani ulipo katika miaka 25 ijayo tutakidhi vipi mahitaji hayo mbele ya wananchi bila kubadilika?”amehoji Jaji Mugeta.
Awali Mwenyekiti wa Rais wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), Kanda ya Arusha George Njooka ameitaka Serikali kuendelea kujenga mahusiano mazuri na taasisi zake.
“Nimesema hivyo kwa sababu Ili kufikia dira yetu ya taifa lazima haki na wajibu viende pamoja na hii ni katika pande zote sio unakuta taasisi ya umma inadaiwa na mteja amekuja kulalamika lakini unaambiwa huruhusiwi kukamata mali fulani ni ya umma, hatuwezi kufikia huko tunakotaka” amesema.
Mmoja wa wananchi waliohudhuria katika maadhimisho hayo, Neema Andrew amesema kuwa maadhimisho hayo ni vema yangeenda sambamba na jukwaa la utoaji wa malalamiko kwa wananchi juu ya kuelezea matatizo yao wanayokutana nayo kwenye taasisi zilizoko kwenye mnyoroo utoaji haki.
“Yako mambo mengi tunakumbana nayo kwenye kusaka haki, ingefaa siku hii wale wakubwa waitishe jukwaa na wakae pale mbele wananchi ambao ni wateja wao waseme changamoto wanazokumbana nazo na wajue matatizo waliyonayo watendaji wao wa chini na wafanyie kazi kuhakikisha inajenga heshima ya sekta hii” amesema.