Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Arusha

MJUMBE wa Kamati ya Utendaji ya J⁸ukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Joseph Kulangwa, ametoa mwito kwa taasisi za habari kuimarisha ushirikiano na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kuhakikisha upatikanaji wa sheria bora za habari zitakazohakikisha uhuru wa vyombo vya habari nchini.

Ameyasema hayo wakati wa mkutano (side event) ulioandaliwa na TEF, LHRC na MCT katika siku ya ufunguzi ya maadhimisho ya siku ya uhuru duniani yaliyofanyika mjini Arusha leo.

Katika kuimarisha ushirikishwaji wa wadau, Kulangwa amezitaka kamati za Bunge kutoa notisi za muda mrefu kwa wadau kabla ya vikao vya kutoa maoni, ili kuwapa nafasi ya kutosha kujiandaa na kuwasilisha mapendekezo yao kwa ufanisi.

Kwa upande mwingine, Mhe. Neema Lugangira, Mbunge wa Viti Maalumu kupitia nafasi ya NGOs, amehimiza taasisi za habari kushirikiana na Serikali tangu hatua za awali za mchakato wa marekebisho ya sheria.

Amesisitiza kuwa ni muhimu kwa wadau kushirikiana na Serikali kuandaa mapendekezo ya maboresho ya sheria badala ya kuyatayarisha peke yao na kuyawasilisha mwishoni kwa ajili ya kufanyiwa kazi.

Dk. Kizito Mhagama naye amesisitiza umuhimu wa taasisi za habari kuendelea kushauri Bunge kwa kina na weledi, ili kuhakikisha zinapatikana sheria bora zinazokidhi mahitaji ya sekta ya habari na kulinda uhuru wa vyombo vya habari.