Na Magrethy Katengu,JamuhuriMedia, Dar es Salaam


TAASISI ya Mama Ongea na Mwanao, imemaliza Mwaka 2024 na kuukaribisha Mwaka wa 2025 Kwa kutoa misaada mbalimbali Kwa watu wenye ulemavu na mahitaji Maalum.

Akizungumza jijini Dar es Salaam Desemba 31, 2024 hafla hiyo ya utoaji msaada huo iliyofanyika katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam, Meya wa Jiji hilo, Omari Kumbilamoto ametoa rai Kwa wadau mbalimbali kuunga mkono juhudi za Taasisi hiyo katika kuyashika mkono makundi ya watu wenye mahitaji maalum.

“Taasisi ya Mama Ongea na Mwanao ambapo Steve Mangele ni Mwenyekiti, inafaa kuigwa Kwa hayo inayoyafanya kwa kuwasapoti watu wenye ulemavu kwa kutoa zawadi mbalimbali,” amesema Kumbilamoto.

Aidha Kumbilamoto amesema kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imejipambanua kuhakikisha inatoa kiasi cha shilingi billion 5 kwa kundi la wenye ulemavu.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Taasisi hiyo hiyo, Steven Mengele ‘jina maarufu Steve Nyerere’, amesema kundi hilo ni muhimu sana na mwaka huu ni mwaka wa tatu toka kuazishwa Kwa utaratibu wa kulishika mkono kundi hilo.

“Rais wetu Mama Dkt. Samia ameamua kutushika mkono, hivyo tumekuwa tukitembea maeneo mbalimbali ya Tanzania kwa kila mkoa kuhakikisha tunakutana na watu wenye uhitaji kwa kuwapa zawadi mbalimbali ikiwemo viti mwendo 50, pamoja na kukarabati madarasa yao,” amesema Nyerere.

Amesema kuwa lengo la kulishika mkono kundi hili ni ili liweze kufurahia maisha kama watu wengine, ndiyo maana wanakutana nao na kula na kucheza nao.