Na Mwandishi Wetu
Taasi ya Jakaya Mrisho Kikwete Foundation (JMKF) na Kampuni ya wanasheria NEXLAW Advocates ya Dar es Salaam wamesaini rasmi makubaliano ya ushirikiano (MoU) yenye lengo la kuimarisha na kukuza ujasiriamali wa vijana nchini Tanzania kupitia Mpango wa JMKF wa Kuharakisha Wavumbuzi wa Kijamii wa Kijana Leo (Kijana Leo Social Innovator Accelerator).
Hafla ya kusaini makubaliano hayo imefanyika leo Aprili 28, 2025, katika ofisi za makao makuu ya JMKF zilizopo Masaki, Dar es Salaam, ikishuhudiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa JMKF, Bi. Vanessa Anyoti, na Mshirika Mwandamizi wa NEXLAW, Profesa Saudin Mwakaje.

Ushirikiano huu wa kihistoria unalenga kuwawezesha vijana wajasiriamali wa kijamii kwa kuwapatia maarifa muhimu kuhusu masuala ya kisheria, rasilimali za kufanikisha uzingatiaji wa sheria na zana za uongozi — ambazo ni msingi muhimu kwa ujenzi wa biashara endelevu na zinazovutia wawekezaji.
“Hili ni tukio kubwa sana,” alisema Prof. Mwakaje. “Tuna furaha kubwa kusaini rasmi makubaliano haya na JMKF. Vijana wengi wana mawazo bora na yenye nguvu ya mabadiliko — lakini mara nyingi hukosa mwongozo wa namna ya kulinda, kurasimisha au kupanua mawazo yao kwa njia ya kisheria. Ushirikiano huu utaleta suluhisho.”
Kupitia makubaliano haya, wataalam wa NEXLAW Advocates waliobobea katika elimu ya kisheria na uzingatiaji wa sheria kwa sekta ya kuanzisha biashara na SME, wataendesha moduli muhimu ndani ya Accelerator iitwayo Sheria, Uzingatiaji, Elimu ya Fedha na Ushirikiano na Mamlaka za Udhibiti.
Moduli hii itawapatia vijana msaada wa kitaalam wa masuala ya kisheria, msaada wa usajili wa hati miliki, na mbinu bora za kupita katika mifumo ya udhibiti.

Kwa mujibu wa Bi. Anyoti, mpango huu umejikita moja kwa moja katika utekelezaji wa Mpango Mkakati wa JMKF wa 2023–2030, ambao umebaini changamoto kubwa kwa vijana kupata huduma za kisheria na maandalizi ya kupokea uwekezaji.
“Ushirikiano huu wa kwanza wa aina yake tunaamini utazaa matunda,” alisema Bi. Anyoti. “Huduma za ulinzi na ushauri wa kisheria zinazotolewa na NEXLAW zitakamilisha juhudi zetu za kuwawezesha vijana na SMEs Tanzania. Tunataka vijana wetu wasiwe tu waotaji, bali wachukua hatua — wenye nguvu ya kufanikisha ndoto zao.”
Programu ya Kijana Leo ilianzishwa mwaka 2021 kwa ushirikiano na Ofisi ya Waziri Mkuu – Idara ya Maendeleo ya Vijana (PMO-LYED) na inarushwa kupitia AZAM TV kwa lugha ya Kiswahili.

Tangu kuanzishwa kwake, programu hii imekuwa nembo ya kitaifa ya ujenzi wa uwezo kwa vijana, ikigusa sekta kama vile kilimo kinachozingatia mabadiliko ya tabianchi, elimu na uvumbuzi wa kidijitali.
Kijana Leo imepata mafanikio makubwa kitaifa kwa wastani wa watazamaji zaidi ya milioni 4 kwa kila kipindi na kushinda Tuzo mbili za Umahiri katika Uandishi wa Habari Tanzania (EJAT).
Kuanzisha na kudumisha biashara changa ni safari ngumu. Kupitia makubaliano haya mapya, JMKF na NEXLAW wamejipanga kuhakikisha kuwa biashara za vijana zinakuwa na uimara wa kisheria, udhibiti na fedha tangu hatua za awali — jambo ambalo litasaidia kuimarisha mfumo wa ujasiriamali Tanzania na kuufanya kuvutia zaidi kwa uwekezaji.
Mbali na malengo ya ndani ya nchi, washirika hawa wawili pia wana ndoto ya kupanua wigo wao kikanda, wakilenga kuendeleza modeli ya Kijana Leo Accelerator kote Afrika Mashariki, huku wakijenga mfumo mpana wa maendeleo ya vijana unaojumuisha uwezeshaji wa kisheria.
“Nina shauku kubwa ya kuona mustakabali ambapo vijana wavumbuzi hawatatiwa moyo tu kuanza safari zao, bali pia kupewa vifaa sahihi vya kuvumilia na kustawi,” alisisitiza Bi. Anyoti. “Mustakabali huo unaanza leo — kwa kutumia vifaa sahihi, ushirikiano sahihi, na maono sahihi.”
JMKF na NEXLAW walitoa shukrani za dhati kwa washirika wote, wadau na wafuasi wanaoendelea kuunga mkono dhamira ya kuwawezesha vijana, wakieleza kuwa makubaliano haya ni zaidi ya hati tu — ni ahadi ya kulinda, kukuza na kusimama bega kwa bega na waanzilishi wapya wa Tanzania katika safari yao ya mafanikio.
