Banki Kuu ya Tanzania (BoT) imetoa tahadhari kwa raia wanaoshikilia pesa za kigeni hususani dola ya Marekani kuwa wapo katika hatari ya kupata hasara kubwa kutokana na uamuzi wao huo wa kuficha pesa hizo wakitegemea kupata faida katika soko la fedha.
Akizungumza leo Jumatatu Agosti 21 katika Kikao Kazi cha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi za Umma, Bw. Emmanuel Tutuba, Gavana wa Benki Kuu amesema Tanzania inatekeleza mikakati ya kuimarisha upatikanaji wa dola hivyo kuendelea kushikilia pesa hizo kuna athari ya kupata hasara badala ya faida.
“Niwaombe (wanaoshikilia dola) mziweke sokoni katika mfumo ulio rasmi. Tutawachukulia hatua za kisheria wale wote watakao bainika kujihusisha na biashara haramu ya soko la fedha (black market),” amesema Tutuba mjini Arusha.
Kwa sasa, Tutuba amesema Serikali inapata dola za Marekani kupitia utaratibu wa kawaida ukihusisha mikopo, misaada, mauzo ya nje na kwamba kunaongezeko la watalii ambao pia wamekuwa wakichangia katika upatikanaji wa dola.
Kwa mujibu wa Gavana, upungufu wa dola ni tatizo la kiduni lililochangiwa na wachapishaji wa fedha hiyo, Marekani, ambayo imeamua kudhibiti mfumuko wa bei kwa kupunguza usambazaji wa dola sokoni.
Marekani imepanga mpango huo utaendelea hadi Mwakani ili kuongeza thamani ya dola na kupunguza mfumuko wa bei ya bidhaa na huduma katika taifa hilo kubwa Duniani.
Katika hatua nyingine, Tutuba amesema Tanzania imetenga kiasi cha zaidi ya Sh bilioni 700 ikiwa ni mkakati wa kurejesha mpango wa Dhamana ya Kuuza Nje (Export Guarantee Scheme). Mpango huo unalenga kusaidia taasisi zinazotumia bidhaa nyingi za kuagiza nje kuongezewa uwezo wa kuzalisha ndani na kupunguza uagizaji wa bidhaa hizo nje.
Pia amesema wanakusudia kuboresha mpango wa kuuza nje kwa kutoa dhamana ya kibenki kwa wazalishaji wa ndani kuboresha ama kuongeza uzalishaji wa mauzo ya nje.