Zebaki katika maeneo yenye uchimbaji mdogo wa dhahabu si msamiati unaotaka kamsi ya Kiswahili sanifu kujua ni nini na inafanya kazi gani.
Katika migodi midogo iliyopo mkoani Geita, hususan machimbo ya Nyarugusu, Makurugusi, Lwamugasa na Mugusu, wachimbaji wadogo wameizoea zebaki kiasi kwamba wanaitegemea kama zinavyotegemewa kuni au mkaa kupika chakula.
JAMHURI limefanya uchunguzi katika migodi hiyo (Nyarugusu, Makurugusi, Lwamugasa na Mugusu) mwanzoni mwa mwezi Februari mwaka huu na kubaini matumizi holela pamoja na udhibiti hafifu wa kemikali hiyo inayosifika kwa kunasa dhahabu.
Kemikali hiyo hutumika wakati wa kuchenjua mchanga na kukamata dhahabu, ambayo huwekwa kwenye karai lenye mchanga pamoja na maji kwa ajili ya kukorogwa kwa mikono ili kemikali hiyo iweze kuenea kwenye udongo huo.
Pamoja na kemikali hiyo kuwa muhimu katika kukamilisha zoezi zima la upatikanaji wa dhahabu katika migodi ya wachimbaji wadogo, kitaalamu inaelezwa kwamba ni kemikali hatari kwa afya ya binadamu na mazingira.
Katika migodi iliyopo Lwamugasa (Bingwareef, Miyombo na Isenyi), Gazeti la JAMHURI lilishuhudia vijana wakiwa wametumbukiza mikono yao bila kuvaa glovu, katika makarai yenye zebaki wakiendelea na kazi ya kuchenjua mchanga wenye dhahabu.
Wengine walionekana wakichoma kwenye moto dhahabu iliyopatikana huku moshi uliochanganyika na mvuke wa zebaki ukifuka moja kwa moja kuelekea usoni mwao, ilhali hawana kitu chochote cha kujikinga na mvuke huo unaotajwa kuwa hatari kwa afya zao, kwa sababu mvuke huo una hewa ya ukaa ndani yake.
Hata hivyo, machimbo ya Musasa yaliyopo wilayani Chato, nako Gazeti la JAMHURI lilishuhudia vyombo vinavyohifadhi zebaki yakiwemo makopo, pamoja na vyombo vingine kama ndoo na makarai yanayotumika kwenye uchenjuaji yakitumika tena kuchotea maji ya kunywa katika vyanzo vya maji vilivyopo hapo.
Hata katika machimbo ya Nyarugusu, mwandishi wa Gazeti la JAMHURI aliwashuhudia wanawake wakifua magunia yaliyotumika kuosha mchanga pamoja na nguo zao wanazovaa wakivifua karibu na vyanzo vya maji, hali inayoashiria mabaki ya zebaki huenda yakawa yanaingia katika vyanzo hivyo ambayo hutegemewa kwa matumizi mbalimbali ya watu na wanyama.
Gazeti la JAMHURI liliwahoji baadhi ya wakazi ya Nyarugusu kuhusu zebaki na athari zake, lakini wengi walionekana kuichukulia kawaida huku wengine wakionyesha kukosa uelewa juu ya madhara ya kiafya yanayoweza kuwapata kutokana na kemikali hiyo.
Ofisa madini mkazi wa Mkoa wa Geita, Ali Maganga, amesema kuwa wachimbaji wadogo mkoani humo wemeelimishwa kuhusu athari za zebaki na kupewa mbinu za kuitumia zebaki hiyo bila kuleta athari kwa afya zao wala kwa mazingira.
Lakini anasema kutoka na ukaidi wa wachimbaji hao huwa hawazingatii usalama wa afya zao, hivyo hufanya makusudi kuitumia kiholela.
Akaongeza kuwa taasisi binafsi na mashirika yasiyo ya kiserikali kama vile Shirika la Plan International wamejitahidi kutoa semina elekezi kuhusu matumizi sahihi ya zebaki bila kuleta madhara lakini wachimbaji hawazingatii.
Hata hivyo ameongeza kuwa umaskini nao unachangia wachimbaji wadogo kuitumia zebaki katika shughuli zao kwani hawawezi kuimudu teknolojia ya kutumia kemikali ya ‘Cynide’ ambayo ni nzuri kwa uzalishaji wa dhahabu.
“Hatuna mbadala wa zebaki, kwa watu wa kiwango cha chini zebaki ndiyo mkombozi wao, wao wanaona ni bora kuitumia kujipatia ridhiki hata kama itasababisha madhara ya kiafya katika miili yao,” alisema mmoja wa wakazi wa Nyarugusu.
James Luhilabake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Musasa ambaye pia anajishughulisha na shughuli za uchimbaji katika mgodi wa Musasa, anaeleza kuwa hajawahi kumshuhudia mwathirika wa zebaki lakini anaamini kwa vyovyote vile kemikali hiyo ina madhara kwa binadamu.
Masunga Magembe, ni mkazi wa Katoro wilayani Geita, anayefanya shughuli za uchimbaji katika mgodi wa Musasa uliopo wilayani Chato, yeye anasema zebaki haina madhara kwani ameitumia kwa zaidi ya miaka 25 bila kupata madhara ya zebaki wala kumshuhudia mtu aliyeathirika kwa sababu ya zebaki.
Anaamini zebaki ina tatizo kwa mtu mwenye kidonda au michubuko kwenye mikono. “Kama hauna kidonda kwenye mwili wako zebaki haiwezi kukufanya chochote, ila ukiigusa ukiwa na kidonda hapo inaweza kukusababishia matatizo,” anasema Magembe.
Hata hivyo baadhi ya machapisho ya wataalamu wa afya yanaonyesha athari za zebaki ni pamoja na kuathiri ubongo, kubadili mfumo wa kawaida wa vinasaba vya binadamu, kuharibu figo, kusababisha upungufu wa nguvu za kiume, magonjwa ya ngozi pamoja na kuharibu mimba kwa wajawazito.
Pia inatajwa kusabaisha uchovu mwilini na kumfanya mtu ambaye ameathirika kuwa na usingizi wa mara kwa mara, kuwa na kichefuchefu pamoja na kusababisha upofu huku kemikali hii ikiwekewa tahadhari kwamba inasababisha ulemavu wa kudumu kwenye viungo vya mwili na kansa.
Meneja wa usajili wa kemikali kutoka Ofisi ya Mkemia Mkuu, Gerald Mollel, ameielezea zebaki kuwa kemikali hatari kwa afya ya binadamu, wanyama na mazingira kwa jumla.
Anasema zebaki inapatikana kutokana na kemikali iliyopo kwenye mwamba ulioko chini ya ardhi unaofahamika kitaalamu kama ‘Cnnabar Ore’.
Anaeleza kuwa kemikali inayotokana na mwamba huo (Cnnabar Ore) ina uwezo wa kujitengeneza yenyewe ikiwa chini ya ardhi au ikachimbwa na kuzalishwa viwandani kwa njia za kitaalamu.
Zebaki inayotumiwa na wachimbaji katika maeneo mengi nchini yenye shughuli za uchimbaji mdogo wa dhahabu ikiwemo inayotumiwa na wachimbaji wadogo mkoani Geita anaitaja kuwa ile inayotengenezwa viwandani.
Vilevile anasema kwamba kwa mjibu wa sheria ya uingizaji wa kemikali nchini, zebaki ya aina hiyo imezuiliwa kuingia nchini lakini kutokana na Tanzania kuzungukwa na mipaka ya nchi jirani, huenda kemikali ya zebaki ikawa inaingizwa kwa njia za magendo kupitia mipaka hiyo.
Akielezea zebaki inavyotengenezwa viwandani, amesema hupatikana baada ya miamba ya ‘Cnnabar Ore’ kuchimbwa na kusagwa kwenye mashine halafu unga wake kuchemshwa kwenye maji na kwamba mvuke unaopatikana unakingwa kwenye kifaa maalumu ambacho hupoza mvuke huo hadi unageuka kuwa zebaki.
“Hii ndiyo wanatumia wachimbaji kukamatia madini ya dhahabu inaitwa ‘Metal Mercury’ rangi yake ni ya fedha na inakuwa nzito.
“Ipo nyingine inaitwa ‘Methylmercury’ hii ni kemikali hatari, hii mara nyingi hujitengeneza yenyewe chini ya ardhi, hii ina uwezo wa kuua haraka sana kwa sababu kiwango chake cha hewa ukaa (Carbon monoxide) ni kikubwa,” anasema Mollel.
Hata hivyo anasema zebaki ya aina hii kuwa inaweza kutengenezwa viwandani pia na kwamba mazingira ya kutengenezwa kwa kemikali ya ‘Methylmercury’ kwa njia za asili hutokea kwa nadra.
Anasema zebaki ya aina yoyote ile inakuwa na kiwango cha hewa ya ukaa (Carbon monoxide) na kwamba zebaki zamani ilikuwa ikitumika kama dawa ya kuua wadudu majumbani na nyingine ikitumiwa hospitalini kuziba meno na kupima joto la binadamu kwa njia ya thermometer.
Anasema kuwa zebaki inao uwezo wa kusababisha wanawake wajawazito kuzaa watoto vilema. Vilevile anasema ikiwa mbegu za kiume na za kike zitakuwa zimeathiriwa na zebaki zinapokutana na kutengeneza mtoto zinakuwa na upungufu wa kimfumo katika vinasaba.
“Kama unavyoelewa mwanaume anatakiwa awe na gameti 23 na mwanamke awe nazo 23 ili watengeneze jumla ya gameti 46 ambazo ndizo hutengeneza mtoto.
“Sasa mbegu zinapokuwa na gameti pungufu kwa sababu ya madhara ya zebaki husababisha mtoto anayetengenezwa kuzaliwa akiwa na upungufu, anaweza kuwa kilema au akawa na upungufu wa akili,” anasema Mollel.
Akifafanua zaidi kwanini zebaki ina madhara katika mwili wa binadamu, amesema kwa kawaida binadamu ameundwa kwa kemikali za madini ya aina mbalimbali, huku akizitaja baadhi ya kemikali hizo kuwa ni zile zinazozalishwa kwenye madini ya vyakula tunavyokula kama vile kalishamu, chuma, fosfolasi (phosphorous), madini ya zinki, potasiamu na magnesiamu.
Madini mengine ni ayodini, kopa, potasiamu, sodiamu pamoja na krolini na krolaidi ambayo hutakiwa mwilini kwa kiwango cha wastani.
“Mwili wa binadamu kuna vitu vinne vinahitajika ambavyo ni hewa ya Oksijeni kwa wingi, Hydrojeni, hawa ya Karboni pamoja na Naitrojeni ambavyo vyote hupatikana kwa wingi katika damu na maji yaliyomo katika mwili wa binadamu.
“Sasa kwenye zebaki kuna hewa chafu, hewa ya ukaa, (Carbon monoxide) hii inapoingia mwilini huvuruga utaratibu wa mwili kwa kuziba njia za damu zinazosafirisha hewa safi (oksijeni), hivyo huzuia damu kusambaa mwilini na kusababisha mwili kuanza kupata maradhi,” anaeleza.
Hata hivyo anaieleza hali hiyo kuchukua muda mrefu kuanza kuonyesha dalili katika mwili wa binadamu, na kwamba hadi matokeo yaanze kuonekana inaweza kuchukua hadi miaka 20.
Naye, Mkurugenzi wa Kitengo cha Uchunguzi wa Saratani, Taasisi ya Uchunguzi wa Saratani na Tiba ya Ocean Road (ORCI), Dk. Maguha Stephano, amesema hakuna ushahidi wa moja kwa moja kwamba zebaki inasababisha ugonjwa huo.
Anasema ni kutokana na kukosekana kwa tafiti za kiafya ambazo zimefanyika nchini na kuonyesha madhara ya zebaki, hivyo ni vigumu kuwabaini wagonjwa ambao wamepata saratani iliyotokana na zebaki.
“Hakuna jibu la moja kwa moja kwamba kansa au saratani inaletwa na vimelea vya zebaki,” amesema.
Ameongeza kuwa ugonjwa wa saratani unasababishwa na mabadiliko ya umbo la chembechembe hai zilizomo mwilini.
Amesema chembechembe hizo zinapopata umbo tofauti na umbo la awali husababisha kushindwa kukaa mahali pake, hivyo kusababisha uvimbe wa eneo husika mwilini.
Dk. Stephano amesema hali hiyo ndiyo hupewa jina la saratani, na kwamba hupewa jina hilo kulingana na eneo ilipo.
“Kuna saratani ya damu, saratani ya ubongo, saratani ya shingo ya kizazi, majina hayo yote hutokana na sehemu chembe chembe hizo zinapokuwa zimekosa umbo sahihi hivyo kusababisha eneo hilo kuanza kulika,” anasema.
Ameyaeleza magonjwa ya saratani kusababishwa na vitu vingi, huku akisisitiza kuwa hakuna tafiti zimefanyika kuonyesha kuwa zebaki ina madhara, hivyo ni vigumu kutoa jibu la moja kwa moja.
“Matokeo ya kupata saratani mara nyingi nayo huchukua muda mrefu kuonekana, inaweza kuchukua hadi miaka 20 na kuendelea hadi dalili zake zianze kuonekana,” anaeleza Stephano.
Methylmecury ilivyoua watu nchini Japan
Nchini Japan kwenye ghuba inayofahamika kama Kyushu, ulizuka ugonjwa uliopewa jina la Minamata. Ugonjwa huo uliua watu takriban 900 na kuacha wengine zaidi ya 2,265 wakiwa na ulemavu wa kudumu katika miili yao.
Ilikuwa mwaka 1956, ambapo wananchi wa mji wa Minamata walishuhudia wagonjwa wanne wakipatwa na malaria kali, kifafa pamoja na kupoteza kumbukumbu kwa haraka, hali iliyosababisha wagonjwa hao kupoteza maisha kwa muda mfupi.
Ugonjwa huo pia uliwapata paka, ambao nao walikuwa wakipata vichaa hadi kufa kila walipokuwa wakila samaki waliovuliwa katika maji ya ghuba ya Kyushu.
Baada ya tukio hilo, ilibainika kuwa chanzo cha ugonjwa huo ni samaki waliokuwa wakivuliwa katika maji ya ghuba hiyo, kwani baada ya kula samaki hao wavuvi wengine 13 wa mji wa Minamata walikufa kwa dalili zilezile.
Hata hivyo, wagonjwa wengine walizidi kuugua, baadaye uchunguzi ulipofanyika wa kubaini chanzo cha vifo hivyo, ilibainika kuwa zebaki aina ya ‘Methylmercury’ iliyokuwa ikimwagwa katika maji ya ghuba hiyo kutoka kwenye kiwanda kilichokuwa kikizalisha kemikali zitokanazo na mimea ndizo zilileta athari hiyo.
Uchunguzi wa kina ulionyesha kuwa zebaki iliyokuwa ikizalishwa kwenye kiwanda hicho baada ya kutupwa kwenye maji iliathiri samaki, ambapo watu wote waliokula samaki hao walipata madhara na wengine kufa.
Kwa mjibu wa ripoti mbalimbali zinazochambua tukio hilo zinaonyesha kuwa hadi sasa athari hizo bado zinawakumba watu wa ghuba hiyo na kwamba tukio hilo limeacha alama inayoonyesha madhara ya zebaki kwa dunia nzima.
Kutokana na athari hizo, kemikali ya zebaki inapigwa vita duniani kote kutumiwa katika matumizi ya kawaida ya kibinadamu.
Ni kutokana na ukweli kwamba zebaki inaathiri afya za watu bila wao kujua madhara yake yanayoweza kudumu kizazi hadi kizazi, kwani baada ya kuingia mwilini hubadili vinasaba vya mwathirika na kuyageuza madhara yake kuwa ya kurithishana.
Zebaki pia ina uwezo wa kuathiri mazingira na viumbe wengine wanayopatikana katika mazingira hayo kama ng’ombe, mbuzi na wanyama wengine. Binadamu akila nyama ya wanyama hao huweza kupata madhara ya zebaki inayokuwa ndani ya nyama ya wanyama hao.
Makala hii imetayarishwa kwa msaada wa Wakfu wa Vyombo vya Habari (TMF).