Waziri-Mkuu-Mstaafu Fredrick-SumayeWaziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye, ameibua upya sakata la uchotwaji mabilioni ya shilingi kutoka kwa Mmiliki wa Kampuni ya Kufua Umeme ya IPTL, Habirnder Singh Seth.

Kampuni hiyo ilikuwa mbia wa VIP Engineering ya James Rugemarila ambao kwa pamoja walikuwa na fedha katika akaunti ya Tegeta Escrow kwenye Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

IPTL ambayo kwa sasa inamilikiwa na Habirnder Singh Seth, ilipata mgawo wake na sehemu kubwa ya fedha zake zilihifadhiwa kwenye Benki ya Stanbic, Dar es Salaam.

Sumaye kwa upande wake, ametaka wote waliochota fedha hizo wawekwe hadharani kama walivyotajwa wengine wanaodaiwa kupata mgawo kutoka Rugemarila.

Sumaye amesema hayo hivi karibuni katika viwanja vya Jangwani jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa Kampeni za mgombea urais kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa. 

Waziri Mkuu huyo mstaafu ambaye amekihama chama tawala na kujiunga na chama cha NCCR-Mageuzi ambacho pia kinaunda Ukawa ameeleza kwamba haingiingii akilini watuhumiwa waliodaiwa kupewa fedha na Rugemalira wakifahamika huku waliopata mgao huo kutoka kwa Seth wakiwekwa kapuni.

Wakati Sumaye akilipua bomu hilo, zipo habari kwamba miongoni mwa wanaodaiwa kuchota mabilioni ya fedha hizo kutoka kwa Singh ni vigogo wa juu wa serikalini. 

“Je, wamelamba Escrow Lowassa alikuwepo? Waliolamba fedha kutoka kwa Rugemalira walijulikana je, kipande cha Seth alilamba nani?”. Alihoji Sumaye huku akishangiliwa na maelfu ya wananchi waliokuwepo Jangwani.

Katika maazimio yake Bunge liliazimia kuwajibishwa kwa mawaziri Profesa Sospeter Muhongo, Profesa Anna Tibaijuka, Mwanasheria Mkuu wa Serikali Jaji Frederick Werema, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi na Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).

Vigogo wengine wa serikali waliotajwa kuhusika na sakata hilo ni Mwanasheria wa zamani Andrew Chenge, Waziri wa zamani wa Nishati na Madini, William Ngeleja na watumishi wengine wa serikali.   

Akiwa Jangwani Sumaye ambaye alikuwa kivutio kikubwa kwa wananchi kutokana na namna alivyopangilia yale aliyotaka alitumia wasaa huo kujibu tuhuma mbalimbali zinazoelekezwa kwa Lowassa.

Kwa mujibu wa Sumaye, Lowassa amekuwa akielekezewa tuhuma za ufisadi, mla rushwa na nyingine lakini akahoji kwamba kama Lowassa ni mla rushwa alitoka madarakani mwaka 2008 wakati huo akiwa na wadhifa wa Waziri Mkuu akahoji kama alikuwa mkosefu kwa nini asiwajibishwe na vyombo vya dola.

“Lowassa alitoka madarakani mwaka 2008, kama alikuwa mla rushwa mbona hakushtakiwa? Kama Lowassa alikuwa mla rushwa alikimbia hii nchi? Lowassa alichukua jukumu la kujiwajibisha kwa makosa ya wengine, lakini leo hii mnamhukumu.

Je, angekuwa mla rushwa leo hii wananchi wote hawa wangekuja kufanya nini hapa?… Wale twiga waliopandishwa ndege Lowassa alikuwepo? Mbona haya hamyasemi…?”, amehoji Sumaye huku akishangiliwa na umati wa watu waliofurika katika viwanja vya Jangwani.

Hali kadhalika Sumaye ameeleza kwamba badala ya kujali wananchi, hivi sasa watawala wamejaa kiburi hivyo amewaasa wananchi kutumia fursa hiyo kukubali kuonja mabadiliko nje ya CCM kwa kumpigia kura Lowassa.

Naye, mgombea mwenza wa Chadema kupitia Ukawa, Juma Duni Haji anasema kuwa katika kipindi cha miaka 50 ya uhuru wa nchi Watanzania wamekuwa wakiishi maisha duni kutokana na kutosekana kwa huduma muhimu.

Duni anasema kuwa uonevu nchini Tanzania umekuwa sehemu ya maisha yao ambako chuki imeongezeka kutokana na kukithiri kwa uonevu katika jamii.

Pamoja na nchi kusifiwa kuwa ina amani ni jambo la kujidanganya maana wenye amani ni wanyonge kwa sababu ya uvumilivu wao ambao sasa umefika kikomo.

Anasema kuwa iwapo atapewa ridhaa katika uchaguzi mkuu atahakikisha anaondoa manyanyaso ya muda mrefu kwa wanawake na watoto ambao wamekuwa wakikosa huduma ya afya inayohitajika.

“Hakuna mtu hata mmoja aliyezaliwa na mwanamume, ni lazima tuwaheshimu kina mama, mama ni mlezi wa watoto wala halipwi, mama hapewi likizo wala kiinua mgongo pamoja na kuzaa idadi kubwa ya watoto,” anasema Duni.

Anaeleza kuwa atahakikisha analinda heshima ya wanawake wananyaonyasika hospitali ambapo hulazimika kulala wanne kitanda kimoja huku wengine wakijifungulia chini huku wakilazimishwa kwenda na vifaa vya kujifungulia hospitali.

“Duniani vimetokea vita vingi lakini hakuna vita vigumu kama vile vya chumba cha uzazi, tunawaahidi kuwaheshimu na kuwaboreshea huduma za afya ili kuokoa maisha ya mwanamke na mtoto ambao wamesahaulika.Tutahakikisha mnapata haki zenu za msingi hata mkienda kupatiwa matibabu hospital mheshimiwe sio kudharaulika kama ilivyo sasa,” anasema Duni.