Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) inapendekeza kuwapo kwa kanuni kadhaa zinazolenga kupunguza ajali nchini. Katika mapendekezo hayo, Sumatra wanataka umri wa madereva wa magari ya abiria uwe kati ya miaka 30 hadi 60. Wamejikita kwenye hoja hiyo dhaifu kwa imani kwamba vijana chini ya umri wa miaka 30 ndiyo chanzo kikuu cha ajali za mabasi nchini!
Bila kumung’unya maneno, tunasema wazi kwamba Sumatra wanataka kuuhadaa umma wa Watanzania. Wanauhadaa umma kwa sababu inaelekea kwamba ni jambo la kawaida Mamlaka za aina hii zinapotaka kujulikana kwamba zipo, basi lazima ziibuke na matamko au mapendekezo ya ajabu ajabu. Ukweli kwamba Sumatra wameshindwa kabisa kupunguza au kuzuia ajali za barabarani na majini, si jambo la mjadala.
Tujuavyo sisi ni kwamba kuna sababu nyingi mno zinazoleta ajali hizi. Kwa mfano, ubovu wa magari, ujuzi hafifu wa madereva, rushwa ya upatikanaji leseni, adhabu ndogo kwa madereva wazembe, uzembe wa watumiaji wengine wa barabara, wembamba wa barabara, hujuma za alama za barabarani na kadhalika.
Sumatra wanatambua kuwa kanuni wanayopendekeza haiwezi kuwagusa wanaoendesha magari madogo na yasiyo ya abiria. Wanatambua kuwa si ajali zote za mabasi, kwa mfano, zinazosababishwa na madereva wa mabasi. Nyingine zinasababishwa na madereva wa magari madogo, madereva wa matrekta, waenda kwa miguu na kadhalika. Hata kama dereva akiwa na umri wa miaka 50, ghafla likakatiza mbele yake gari bila kuzingatia sheria za usalama barabarani, lazima ajali itatokea na hata kusababisha maafa.
Sumatra hawa hawa wanatambua kuwa tuna idadi kubwa ya madereva wenye umri wa miaka wanayoitaka wao wanaoendesha bila kuzingatia sheria za usalama barabarani. Hawa ndiyo wale wanaopita magari kwenye kona na sehemu zisizoruhusiwa kisheria. Hakuna ushahidi wa wazi kwamba wanaofanya makosa hayo ni wenye umri unaoishia miaka 29 pekee.
Sumatra wanatambua kuwa wana sheria inayotaka gari linaloharibikia barabarani kuondolewa baada ya muda fulani ili kuondoa msongamano na hatari ya kutokea ajali. Sheria hiyo wameiweka kapuni, badala yake wanakuja na porojo zisizokuwa na maana. Mara zote wamekuwa wakisafiri huku na kule nchini. Wanashuhudia mamia ya malori yaliyoegeshwa katikati ya barabara yakifanyiwa matengenezo makubwa yakiwamo ya “gear box”. Hatujasikia mahali popote wakiwaadabisha kisheria wavunjaji hao wa sheria. Matokeo yake ajali nyingi zimekuwa zikitokea kwa magari kuyagonga malori yaliyoegeshwa holela.
Kana kwamba hayo hawayaoni, juzi Waziri wa Uchukuzi kapiga marufuku “kuchimba dawa” holela. Sumatra wakitambua kuwa suala hili linawahusu, kwa miaka yote wamekaa kimya. Walipomsikia Waziri nao wamezomoka na kutoa orodha ya vituo kwa abiria kujisaidia. Tunajiuliza, muda wote walikuwa wapi? Kwanini waendelee kufanya kazi kwa mazoea? Abiria wanajazwa kwenye daladala na mabasi makubwa kana kwamba nchi hii haina utawala. Kenya, Uganda, Zambia na kwingineko kwenye “Sumatra” zenye watu makini wamedhibiti hali hiyo. Hapa kwetu wamebaki kwenye usingizi wa pono. Hawa wanastahili kubanwa. Kasi hii hawaimudu.