Mchezaji wa Uruguay, Luis Suarez (31), amesema kamwe hawezi kuomba msamaha kwa kushika kwa mkono mpira uliokuwa unaingia golini kwao katika mechi yao ya Kombe la Dunia dhidi ya Ghana mwaka 2010 nchini Afrika Kusini.
Watu wengi wamekuwa wakimtaka Suarez kuomba msamaha kwa kitendo chake hicho ambacho kiliinyima Ghana nafasi ya kutinga hatua ya robo fainali ya michuano ya Kombe la Dunia baada ya kudaka mpira huo ambao ulikuwa ukielekea wavuni na kuipa Ghana goli muhimu.
Suarez amesema yeye hastahili lawama na hawezi kuomba msamaha kwa kuwa alishapewa kadi nyekundu kwa kosa hilo na penati ilitolewa hivyo hahitaji kuomba msamaha kwa sababu ya jambo hilo.
Suarez anasema angekuwa tayari kuomba msamaha iwapo kadi yake nyekundu ingetokana na rafu mbaya ambayo angekuwa amemfanyia mchezaji wa timu pinzani ya Ghana.
Suarez amenukuliwa akisema, “Sihitaji kuomba msamaha [kwa kuzuia mpira usiingie golini kwetu kwa mkono]. Hilo sio kosa langu kwa sababu mimi siye niliyekosa penati”.
Katika mechi hiyo Ghana walikosa penati baada ya Asamoah Gyan kugongesha mpira katika mwamba wa juu wa goli na kuinyima Ghana fursa ya kutinga hatua ya robo fainali ya Michuano ya Kombe la Dunia.