Waziri Wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira amesema yeye ni mtu safi asiye na kasfa ya ufisadi tangu kuzaliwa kwake.
Akzungumza katika Ukumbi wa BoT, jijini Mwanza alipokuwa akitangaza nia ya kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 25, mwaka huu.
Wasira anasema kuwa ameitumikia nchi ya Tanzania katika Serikali zote nne na hana rekodi ya kupokea rushwa katika utendaji wake tangu kashfa zote zilizowahi kutokea nchini kuanzia sakata la kuchotwa kwa fedaha benki kuu EPA na Escrow.
Anasema kuwa yeye binafsi pamoja na kutokuwa katika kashfa za uchotwaji huo wa fedha ambao umekuwa ukiwahusisha vigogo serikalini sio kwamba hafanyi kazi za madaraka makubwa bali ni kutokana na uadilifu wake na kujiamini.
Anaeleza kuwa amekaa Ikulu ya Rais Jakaya Kikwete kwa miaka minne, lakini kila siku alikuwa akijiuliza, “Kuna biashara gani pale kiasi cha kuwafanya baadhi ya watu kutumia nguvu kubwa kutaka kwenda huko ambako kila siku alikuwa akiona wafanya usafi na wamwagilia maua.”
Wasira amewataka viongozi wa CCM kupima na wagombea wote watakaojitokeza kuwania nafasi hiyo ili kupata mtu safi maana Ikulu hawezi kukaa mla rushwa ambaye atauza nchi.
“Ikulu hatuwezi kuweka mla rushwa, mkiweka mla rushwa atauza Ikulu yenu, rais wa Tanzania ni mtu mmoja tu, hatuwezi kumkosa mtu mwadilifu katika watu milioni 44, yupo na atapatikana,” anasema Wasira.
Anabainisha kuwa Baba wa Taifa Mwalimu Julius K. Nyerere aliwahi kumwambia kuwa kama anataka kuwatumikia Watanzania basi awatumikie kwa uadilifu, lakini kama anataka utajiri basi akafanye biashara.
“Nilichagua kuwatumikia Watanzania, na kama utatajirika ukiwa waziri basi wewe ni mwizi, ukitajirika kwa mshahara nawe ni mwizi lazima tukutilie shaka, ukitaka kutajirika unakuwa mfanyabiashara, huko ndiko kuna kununua kwa urahisi na kuuza ghari,” anasema.
Akijibu swali kuhusiana na kifo cha lililokuwa Azimio la Arusha, Wasira anasema kuwa Azimia la Arusha lilikuwa linasisitiza ujamaa ambao hata hivyo anaamini ya kuwa bado upo ila kila kitu kinabadilika kutokana na wakati.
“Naamini mpaka sasa ujamaa bado upo, ndio maana tunasema wazee tutatibiwa bure, tutaendelea kutekeleza uchumi wa soko bila kusahau misingi ya soko, sio lazima watu walime shamba moja kama awali, hatuwezi kusema turudi tusiwe na nyumba ya kupangisha, kila kitu kinabadilika kutokana na wakati,” anasema Wasira.
Akifafanua kuhusiana na kukwama kwa mchakato wa kura ya maoni ya Katiba Mpya, Wasira anasema: “Katiba ni suala la mchakato ambalo halijakwama kama ambavyo inaelezwa na baadhi ya watu bali limesimamishwa kutokana na kuwepo kwa uchaguzi mkuu.”
Anasema kuwa katiba ni suala la muda haijakwama bali upo Uchaguzi Mkuu hivyo Rais ajaye anaweza kuangalia nini afanye na kama itapigiwa kura na kuona kama itapita basi falsafa ya wengi wape itatumika maana hiyo ndiyo demokrasia ya kweli.