DAR ES SALAAM
Na Mfaume Seha, TUDARco
Timu ya taifa, Taifa Stars, imejiweka katika nafasi nzuri kuwania kufuzu kucheza michuano ya Kombe la Dunia itakayofanyika nchini Qatar mwakani.
Stars inaongoza Kundi ‘J’ lenye mataifa ya DRC, Benin na Madagascar, ikiwa na alama nne baada ya mechi mbili za kwanza.
Akizungumza na JAMHURI, shabiki mmoja wa soka jijini Dar es Salaam, Abuu Abdallah, anasema kikosi cha sasa cha timu ya taifa ni imara.
“Kikosi kimebadilika, hasa jinsi wanavyocheza inaonyesha wachezaji wanamsikiliza na kumuelewa mwalimu, hivyo kutimiza majukumu yao uwanjani,” anasema.
Anataja dosari ya safu ya ulinzi kupiga pasi ndefu sizizokuwa na msaada mkubwa, kuwa moja ya mambo yanayopaswa kufanyiwa kazi.
“Wakati timu ikiwa inashambuliwa, pasi fupi fupi ndizo huwa zina manufaa zaidi. Wachezaji wa kiungo nao kwa namna fulani wamekosa ubunifu, hasa wa kuipandisha timu mbele. Pasi zao nyingi ni za kurudisha nyuma,” anasema.
Abdallah anashauri safu ya ushambuliaji ya Taifa Stars kuongeza umakini na kushirikiana kwa kuwa: “Kuna muda wanaonekana kama wanategeana ndiyo maana japokuwa mabao yanapatikana, huwa si ya ufundi!”
Katika mahojiano na waandishi wa habari baada ya mechi zote mbili; ile dhidi ya DRC jijini Kinshasa na dhidi ya Madagascar, Dar es Salaam, Kocha wa Stars, Kim Paulsen, anasema kuna nyakati wachezaji wake hujisahau na kucheza nje ya maelekezo.
Kwa kauli hiyo, benchi la ufundi la Stars lina kazi kubwa ya kujenga timu imara zaidi ndani na nje ya uwanja, na Abdallah anasema:
“Kuna suala la saikolojia. Hili ni muhimu kwa mchezaji ili kumuweka sawa kiakili aweze kuzingatia maelekezo ya mwalimu na kuyafanyia kazi kwa vitendo.”
Kwa sasa wachezaji wanarejea katika klabu zao kujiandaa kuhusu mechi za kimataifa, hivyo kuwapa nafasi ya kujiandaa na kujifunza kutoka kwa wenzao.
Stars inaundwa na nyota wengi wanaocheza soka lao nchini, mbali na Nahodha Mbwana Samatta anayecheza nchini Ubelgiji na Simon Msuva aliyepo Morocco.
Stars inatarajia kutupa karata yake nyingine mwezi ujao kwa kuchuana na Benin, mchezo wenye nafasi ya kuonyesha mwelekeo wa Tanzania katika kufuzu kwa Kombe la Dunia la Qatar 2022.
Mechi hiyo inapigwa Dar es Salaam na ni faida kwa wachezaji kuitumia vizuri.
Kwa upande mwingine, mashabiki wanapaswa kuiunga mkono Stars kwa kujitokeza kwa wingi uwanjani.