Ligi mbalimbali duniani zimemalizika katika msimu wa 2018/2019. Fainali ya Europa na UEFA nazo zimemalizika, hicho kikiwa ni kiashiria kwamba wachezaji wanakwenda katika mapumziko na kuanza maandalizi ya msimu mwingine wa ligi.
Pazia la Ligi ya Mabingwa barani Ulaya limefungwa Jumamosi iliyopita kwa fainali baina ya Tottenham na Liverpool.
Mchezo huo ulipigwa katika dimba la Wanda Metropolitano (uwanja wa Atletico Madrid), mechi ambayo majogoo wa Merseyside, Liverpool walitawazwa mabigwa wa UEFA kwa ushindi wa 2-0, jijini Madrid, Hispania.
Mashabiki wa soka duniani sasa wanaelekeza macho na masikio nchini Misri, ambako fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika zitachezwa mwezi huu, timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, inashiriki mashindano hayo baada ya kutofanikiwa kufuzu kwa miaka 39.
Taifa Stars imepangwa katika kundi C, ambalo washindani wengine ni Kenya, Algeria na Senegal. Taifa Stars imepangwa kwenye kundi lenye ushindani wa hali ya juu, huku Senegal na Algeria wakiwa na uzoefu wa kushiriki fainali za Kombe la Dunia mara kadhaa.
Wafuatao ni wachezaji wa kuchungwa na wachezaji wa Taifa Stars katika kundi hilo ili wasilete madhara watakapochuana nao.
Sadio Mane, Senegal; ni mchezaji hatari anapokuwa na mpira, katika msimu huu katika Ligi Kuu ya Uingereza amefunga magoli 22, akifungana na mshambuliaji wa Arsenal, Pierre Aubemayang pamoja na Mohamed Salah wa Liverpool.
Liverpool wameshika nafasi ya pili katika msimu huu wa ligi na ndio mabingwa wa UEFA.
Kocha wa Senegal, Aliou Cisse, anamtegemea Mane kama shujaa ambaye atashirikiana vizuri na wenzake ili kutwaa Kombe la Mataifa ya Afrika kwa mara ya kwanza tangu nchi hiyo ianze kushiriki fainali hizo. Safu ya ulinzi inahitaji kuwa na umakini ili kumdhibiti mshambuliaji huyu.
Mchezaji mwingine hatari ni kiungo mkabaji, Idrisa Gueye, ambaye ni beki wa Klabu ya Everton. Lakini wakati ligi inakwisha tayari Manchester United wamevutiwa na kiwango chake, inawezekana msimu ujao akavaa jezi ya Man United.
Mchezaji mwingine wa kuangaliwa kwa karibu ni winga wa Algeria na Klabu ya Manchester City, Riyad Mahrez.
Umaarufu wake ulianza mwaka 2016, baada ya kuchaguliwa kuwa mchezaji bora wa Ligi Kuu ya Uingereza, baada ya kuisaidia Klabu yake ya Leicester City kutwaa ubingwa.
Mahrez ameiwezesha timu yake kutwaa vikombe ambavyo ilikuwa ikishiriki ndani ya Uingereza. Vikombe hivyo ni ubingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza, Ngao ya Jamii, Kombe la FA na fainali ya Kombe la Carabao.
Taifa Stars inakwenda kwenye mashindano hayo kifua mbele, hasa kutokana na umahiri wa mshambuliaji wa KRC Genk, Mbwana Samatta. Mshambuliaji huyo ndiye amechukua kiatu cha dhahabu cha mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Ubelgiji.
Samatta amefunga magoli 20, na kuwa mfungaji bora katika Ligi Kuu ya Ubelgiji pamoja na kuchaguliwa kuwa mchezaji bora mwenye asili ya Afrika.
Mbali na Samatta, mshambuliaji wa Difaa El Jadidi ya Morocco, Simon Msuva, pia anatarajiwa kung’ara katika mashindano hayo.
Kiungo wa Harambee Stars na Tottenham ya Uingereza, Victor ‘Mugabe’ Wanyama, anabaki kuwa kiungo bora zaidi katika ukanda wa Afrika baada ya viungo kama Yaya Toure, kuyapa kisogo mashindano ya kimataifa.
Uwepo wa Wanyama katika nafasi ya kiungo mkabaji, umekuwa wa faida kubwa kwa Tottenham hadi kufikia fainali ya UEFA, ambayo hata wakati wanapoteza 2-0 kwa Liverpool, hakucheza na badala yake nafasi yake ilizibwa na Harry Winks.
Katika kundi hili Sadio Mane na Victor Wanyama watachuana tena katika timu zao za taifa baada ya kukutana katika Ligi ya Mabingwa barani Ulaya.