LILONGWE

Na Mwandishi Maalumu

Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, amezitaka nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo  Kusini mwa Afrika (SADC) kufungamanisha sekta za kilimo na nishati kupitia mikakati  mbalimbali ya kukuza uchumi wanayoitekeleza.

 Akizungumza katika Mkutano Mkuu wa 51 wa  Jukwaa la Mabunge ya SADC uliofanyika jijini  Lilongwe nchini Malawi hivi karibuni, amesema kuna umuhimu wa kufungamanisha sekta hizo ili ziwezeshe ukuaji wa uchumi katika ukanda wa SADC.

“Endapo tunahitaji nchi zetu ziweze kujitegemea kwenye suala la usalama wa chakula, tunapaswa  kujifunza kupitia nchi zingine zilizofanikiwa  katika sekta hii kama zilivyoainishwa katika taarifa ya kamati ya chakula.

“Tunapaswa kuweka kipaumbele katika miundombinu wezeshi itakayosaidia kukuza sekta ya kilimo, kama ni sekta ya nishati basi twende pamoja kama jumuiya kuhakikisha inakuza kilimo chetu,” amesema.

Akitolea mfano wa nchi  ya Jamhuri ya   Kidemokrasia ya Congo (DRC), amesema: “Nakubaliana na wenzetu wa Kongo kuwa mradi wa umeme wa maji wa Inga unaweza kutoa umeme kwa nchi zote za SADC, hivyo kusaidia katika juhudi za kukuza sekta ya kilimo.”

Pia amewaomba  wajumbe wa mkutano huo  kuweka nguvu katika maeneo mengine ya kiuchumi yatakayofungamanishwa ili kukuza sekta ya kilimo kabla ya kufikiria kupata wawekezaji wakubwa watakaokuja kuwekeza katika sekta hiyo.

Amewashauri wajumbe hao kuzishauri nchi zao kuondoa vikwazo katika biashara ya mazao   mbalimbali yanayozalishwa kwa wingi kama sehemu ya juhudi za kukuza sekta ya kilimo.

Kadhalika, ameshauri kuimarishwa kwa  ushirikiano wa biashara baina ya nchi hizo ili kuhakikisha kunakuwapo na soko la uhakika kwa mazao yanayozalishwa na wakulima.

“Iwapo nchi mojawapo katika ukanda huu inazalisha kwa wingi zao fulani, kwa nini nchi zingine wanachama zisiiunge mkono kwa  kununua zao hilo badala ya kwenda kununua katika nchi zilizo nje ya SADC? Kwa kufanya hivyo tutatengeneza soko la ndani la bidhaa za kilimo,” amesema.

Awali, mjumbe wa Jukwaa hilo na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya SADC PF ya Chakula, Kilimo na Maliasili, Ishmael Onani, amewasilisha taarifa ya kamati hiyo na amesema pamoja na  ukweli kwamba kilimo ni kati ya sekta muhimu za kukuza uchumi na kupunguza umaskini lakini kumekuwa na uwekezaji mdogo.