KILIMANJARO
Na Nassoro Kitunda
Baada ya hoja ya aliyekuwa Spika wa Bunge, Job Ndugai, au kama ilivyoitwa kauli aliyoitoa wakati anazungumza na Umoja wa Wagogo (Wanyasi) kuhusu mikopo na kwenda mbali kutaja deni lilivyokua kwamba tunadaiwa Sh trilioni 70 na tuna bajeti ya Sh trilioni 30 lakini katika fedha hizo, Sh trilioni 10 zinakwenda kulipa deni la taifa na alihoji hii ni sawa?
Kisha akatoa tahadhari kwa nchi. Hoja yake hiyo iliibua mjadala kwa wasomi na wanasiasa wa ndani na wa nje ya chama, na kupokewa tofauti. Kuna watu waliona alikuwa na hoja sahihi na alipaswa kuisimamia na wengine waliona amekosea na alipaswa kufanya kitendo alichokifanya cha kujiuzulu.
Lakini msimamo wake huo wa Ndugai baada ya mjadala kuibuka, naye aliibuka na kutolea ufafanuzi, akaomba msamaha kama alivyosema imetafsirika ndivyo sivyo. Mbali na msamaha huo, Rais Samia Suluhu Hassan na baadaye wanachama na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) walijitokeza na kumkosoa Ndugai.
Pia wanachama hao pamoja na wabunge walijitokeza na kumtaka ajiuzulu, na ndicho kilichotokea. Amejiuzulu na yeye mwenyewe amesema amefanya hivyo kwa masilahi mapana ya nchi.
Katika wazo hili sitajikita katika makundi mawili haya ya wanaompinga spika kwa kauli yake ama matendo yake aliyoyafanya nyuma au wale wanaoona angeendelea na msimamo wake na kuleta hoja ya mihimili ya dola.
Mimi nitachochea mjadala kwa hoja iliyoibuliwa na spika mwenyewe, lakini pia ni hoja ya muda mrefu juu ya masuala ya mikopo na madeni katika nchi zetu.
Hoja ni ipi?
Katika mjadala huu ambao pia umepanuka zaidi baada ya spika kujiuzulu, ni hoja iliyobakia, ya masuala ya nchi nyingi za Afrika kukopa. Kwa hiyo, hoja iliyopo ndiyo hii ya madeni na mwendelezo wa kukopa kwa nchi zetu.
Ingawa waliompinga spika walijaribu kujibu hoja hiyo, kwa baadhi yao kusema mikopo hii imekopwa muda mrefu na utamaduni huo upo wa kukopa, lakini wengine walisema kuwa hata nchi kubwa nazo zinakopa na zina madeni, sembuse Tanzania.
Lakini hoja hizi, ndiyo ni hoja lakini bado si sehemu ya kuondoa hoja ya wale wanaotia shaka juu ya mwenendo wa madeni katika nchi zetu na kutoa ushauri wa kutafuta namna ya kujitegemea hapa ndani.
Hii ndiyo hoja iliyobaki, spika aliyoisema, lakini yeye si wa kwanza, imekuwa ni sehemu ya mjadala katika historia ya Bara la Afrika na duniani kwa ujumla.
Mjadala wa madeni katika nchi za Afrika
Mjadala huu una historia yake katika Afrika, si hoja ambayo ameianzisha spika aliyejiuzulu, ni hoja ambayo tangu nchi za Afrika zinatafuta uhuru wake, mfano mzuri Tanzania, baada ya uhuru ilikuja na azimio la Arusha na kutangaza sera ya ujamaa na kujitegemea, kwa maana nchi kuwa na uwezo wa ndani wa kuamua na kuwa na uamuzi wa rasilimali zake na namna ya kuzitumia kwa manufaa ya watu wake.
Pia kujitegemea kulitazamwa kama sehemu ya kujiepusha na mikopo na misadaa iliyozua mjadala kwa wanasiasa na wasomi wakiwamo akina Dambisa Moyo katika kitabu chake cha ‘Dead Aid; Why Aid is not working and How There is better Way for Africa.’
Katika kitabu hiki, mwandishi anaibua hoja hiyo kuwa ndiyo tunapata misaada na mikopo lakini inaleta shida katika nchi za Afrika badala ya kuleta maendeleo.
Dambisa anaonyesha nchi nyingi za Afrika zinatumia mapato yake ya ndani kulipa mikopo badala ya maendeleo yake. Kwa hiyo, naye kitabu chake kinajaribu kushauri namna ya nchi za Afrika kusonga mbele na kuwa na tahadhari juu ya misaada na mikopo.
Hata Profesa Issa Shivji katika baadhi ya maandiko yake, hasa kwenye andiko lake la ‘Accumulation in an African Periphery; A Theoretical Framework’ aliwahi kujadili suala la mikopo, namna nchi zilizoendelea zinavyotumia dhana ya mikopo kama sehemu ya kutafuta faida (biashara) na si kusaidia nchi hizi za Afrika kuendelea.
Alionyesha wanachokopeshwa na kuwapa Waafrika kama misaada ni kidogo kuliko wao wanachokichukua barani Afrika. Alitolea mfano, katika kipindi hicho, ndani ya miaka 18, Nigeria ilikopa mkopo wa thamani ya dola bilioni 13.5 za Marekani lakini ikalipa deni hilo kwa dola bilioni 42 za Marekani, ikiwa ni mara nne ya mkopo waliokopa awali.
Tuendelee kuijadili hoja hii?
Kama nilivyo sema awali, spika kama mtu ameondoka katika kiti, lakini kuna hoja imebaki mezani. Ndiyo, hakuna nchi isiyo kopa lakini ni muhimu kuendelea kujadili namna ya kutafuta sababu za ndani za kujitegemea kama Mwalimu Julius Nyerere alivyosimama katika kuhakikisha tunajitegemea na hadi anaondoka aliona hakukuwa na shida yoyote katika Azimio la Arusha lililokuwa ni kiini cha dhana ya kujitegemea.
Hivyo, tunapaswa kuipa nafasi hoja hii, si hoja ya spika bali ni hoja ya waasisi wetu waliopigania nchi hizi na hata kuja na dhana ya Umajumui wa Afrika (Pan Africanism) kwa maana ya kutaka kuifanya Afrika kuwa moja na kupambana na ubeberu na kuweza kujitegemea yenyewe.
Kwa sababu madeni haya kwa nchi hizi zilizoendelea zinatumia kama biashara, si kama zina lengo pana la kutaka kusaidia nchi zetu za Afrika. Haya ndiyo yalikuwa maono na ndoto za waasisi wetu akina Kwame Nkrumah, Mwalimu Nyerere na wengine. Kuona Afrika ikijitegemea na kupambana na ubeberu ulimwenguni.
Hivyo, naheshimu hoja zote mbili; wale wanaoona tunapaswa kukopa lakini tuangalie mikopo ya riba nafuu na wale wanaohimiza kuwe na namna ya kujiondoa katika mikopo hiyo na kutafuta vyanzo vya ndani na kuendeleza nchi. Hoja zote hizi zinapaswa kujadiliwa kwa kina na tusijadili haiba ya mtu, tukiendelea kujadili mtu, huyu mtu ameondoka tayari, amejiuzulu, lakini hoja imebaki na bado tunayo.
Kwa hiyo, tujadili hoja hii kwa kina, maana katika mjadala kama asemavyo Profesa Shivji ndipo mahali panapopatikana mwafaka.
Rai yangu ni kwamba katika mjadala huu, wa kujiuzulu kwa spika, ni muhimu tukajadli sera badala ya haiba za watu. Tujikite kwa kile kilichobaki baada ya spika kujiuzulu.
Kilichopo tukijadli kwa hoja ili tupate mwafaka kama nchi. Tufanye nini katika mikopo hii? Mikopo ya aina gani tuchukue? Lakini hadi lini tutachukua mikopo hii? Pia tutaiendeleza vipi dhana ya kujitegemea? Maswali haya yanapaswa kuongoza mjadala wa hoja tuliyokuwa nayo.
Mwandishi wa makala hii ni Mhadhiri Msaidizi wa Idara ya Sosholojia na Ustawi wa Jamii katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Mwenge (MWECAU).
0659-639808/0683-961891