Ni kosa kubwa kwa mtoto wa Kizanaki kumtamkia mtu aliyemzidi umri neno ‘mwongo’. Hawa ni tofauti na makabila mengine, mathalani Wajita. Wao mtoto ana uhuru na haki ya kumtamkia mzazi au mtu aliyemzidi umri neno ‘mwongo’. Wakati Mzanaki atapambana kumnasa vibao mtoto anayeamini kamtukana, mzazi wa Kijita atafanya juhudi za kupambana kwa hoja kumthibitishia mtoto yule kwamba yeye (mkubwa) si mwongo. Hizo ni tofauti za wazi kwa makabila hayo mawili.
Vivyo hivyo, tumezoea kuwasikia wananchi wakiisema mihimili ya Serikali na Bunge kwa uwazi kabisa. Serikali inakosolewa kwa matukio ya rushwa, ajali barabarani, ujambazi, ukosefu wa elimu bora, uduni wa huduma za kijamii kama afya, tiba, maji, nk.
Bunge linakosolewa kwa kupitisha miswada isiyo na manufaa kwa wananchi, utoro wa wabunge, matumizi ya fedha nyingi, marupurupu manono, n.k. Kwa namna mihimili hii miwili inavyosemwa, unaweza kuifananisha na mzazi wa Kijita.
Mahakama ni tofauti. Kuambiwa ukweli maana yake ni kuikosea adabu. Ni kama mzazi wa Kizanaki, Mahakama imejiweka katika mazingira ya kutaka iaminiwe kwa utakatifu. Haitaki iambiwe kuwa ndani yake kuna wasio waadilifu. Mbunge Tundu Lissu alianika udhaifu wake. Akachukiwa na wachache, lakini wengi walikubaliana naye. Hadi leo si Mahakama wala Bunge waliokuwa na ujasiri wa kujitokeza kukanusha alichokisema Lissu.
Ni rahisi zaidi kumsema Rais au Spika, lakini ni vigumu sana kumsema Jaji Mkuu hata kama ana kasoro. Mahakama imejiwekea kinga ya kutotaka kuguswa kwa kigezo kwamba kufanya hivyo ni kuingilia uhuru wake! Ngao hiyo imeifanya Mahakama ivurunde mambo mengi, lakini iachwe kwa sababu kuisema ni kuikosea adabu.
Sisi JAMHURI tupo, si kwa ajili ya kupambana na mihimili ya dola, yaani Serikali, Bunge na Mahakama. Hatuna ubavu wa kupambana na Mahakama. Tunatambua kuwa kwa nia njema au kwa hila Mahakama inaweza kutuweka kwenye wakati mgumu. Inaweza kututoa kwenye ramani ya dunia.
Tunayasema haya tukirejea kauli ya Jaji Kiongozi ya kwamba ametuchoka. Hili neno ‘tumewachoka JAMHURI’ ni neno kali sana. Hatujui baada ya kauli hiyo kitu gani kitafuata, lakini ni dhahiri kuwa kitakacholetwa kwetu si kitu cha heri. Tunauacha umma uamue ni nani mkweli kwenye suala la uadilifu miongoni mwa baadhi (tunasema baadhi) ya mahakimu na majaji wetu.
Tumeingia kwenye mapambano dhidi ya wauza na wasafirisha dawa za kulevya. Hawa wanawaumiza sana vijana wetu. Wapo walioachiwa na mahakimu au majaji kwa sababu mtuhumiwa mwanamke alikamatwa na polisi mwanamume! Kwa maneno mengine, akitokea mtuhumiwa wa ujambazi mwanamke, polisi mwanamume asimkamate maana akimkamata atakuwa amemdhalilisha! Haya ndiyo Jaji Kiongozi wetu anayotaka kuwaambia Watanzania.
Dawa za kulevya zimewafanya vijana wengi wawe mazezeta na wahalifu. Tumeingia kwenye mapambano dhidi ya wezi wa mali za umma. Mfano mzuri ni wa Mkutano wa Smart Partnership ambao ulitumiwa kutafuna mabilioni ya shilingi.
Tumeingia kwenye mapambano dhidi ya matapeli nguli wa madini hapa nchini. Hawa wanawaliza walimwengu wengi. Wanawatapeli mabilioni ya shilingi. Jina la Tanzania linanuka kwa sababu ya watu hawa. Wana fedha nyingi. Wanahonga kila wanapoweza. Baada ya kuwaandika wamekutana katika kikao cha dharura. Wamechangisha fedha kwa lengo moja kuu la kuhujumu JAMHURI, waandishi na wahariri wake. Tumeandika habari zilizofanikisha kusafishwa kwa baadhi ya mashirika ya umma, ikiwamo Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL).
Yote haya, na mengine yanayowagusa mahakimu na majaji, tunajua yana athari kubwa kwetu. Lakini tufanye nini? Hatuwezi kurudi nyuma. Tunaifanya kazi hii kwa kumtanguliza Mungu mbele. Haiwezekani katika nchi hii kila mtu awe mwoga. Woga ndiyo silaha dhaifu kuliko zote.
Hatuna nguvu za kidola wala kifedha. Tunajua tunaweza kufungwa, kuuawa au kuzuiwa kuifanya kazi hii. Kitu kimoja kitaendelea kubaki kwenye historia ya Taifa letu; nacho si kingine bali tumethubutu kusema yasiyosemwa. Tumesema ukweli. Tunamtanguliza Mungu mbele na kuomba Watanzania wenzetu watuunge mkono.