Kampuni ya kuchakata gesi asilia na kuzalisha umeme ya Songas inapanga kuongeza kiasi cha umeme inachozalisha nchini kwa asilimia 33 ili kuliwezesha taifa kuwa na nishati ya kutosha kwa ajili ya shughuli za kiuchumi, mkurugenzi mtendaji wake amesema.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji huyo, Nigel Whittaker (pichani), ili kufanikisha mpango huo zinahitaji dola milioni 60 za Marekani (sawa na Sh bilioni 138.5) ambazo kampuni hiyo iko tayari kutumia kama itakubaliana na serikali kufanya uwekezaji huo.

Kwa sasa kampuni hiyo inazalisha asilimia 25 ya umeme wote unaoingizwa kwenye gridi ya taifa.

“Tayari tumeandaa mpango kabambe wa kupanua na kuongeza uzalishaji wa umeme kwenye mitambo yetu ya Ubungo ambayo hivi sasa inazalisha megawati 180. Kama serikali itaridhia mpango wetu, tutaongeza kiwango cha umeme tunachozalisha hadi megawati 240 ambalo litakuwa jambo zuri kwa uchumi na maendeleo ya nchi,” Whittaker aliliambia JAMHURI wiki iliyopita katika mahojiano maalumu.

Mkurugenzi huyo ambaye uongozi wake unakwisha mwishoni mwa mwezi huu baada ya kuitumikia kampuni hiyo kwa miaka minne na nusu, anasema uwekezaji mpya katika mradi huo ni muhimu kwa sasa wakati Tanzania iko kwenye mchakato wa kujenga uchumi wa viwanda.

Whittaker pia alitanabainisha kuwa nchi inakuwa salama zaidi kinishati inapokuwa na vyanzo mbalimbali vya umeme na kuongeza kwamba hili ni suala la msingi katika uchumi wowote wa kisasa. Kupitia uchumi wa viwanda, Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kuifanya Tanzania nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

“Serikali ikikubali kuongeza mkataba wetu wa mauzo ya umeme (power purchasing agreement) na Tanesco tuko tayari kuwekeza dola milioni 60 zaidi kwenye mitambo ya Ubungo kwa ajili ya kuongeza uzalishaji,” raia huyo wa Uingereza anafafanua.

Kwa mujibu wa Whittaker, Mkataba wa Mauzo ya Umeme (PPA) wa hivi sasa utamalizika mwaka 2024, na ili uwekezaji mpya wa Songas uwe na tija, mkataba mpya inabidi uwe wa kati ya miaka 10 na 15 na bei ya umeme kwa Tanesco ibaki ileile ya senti sita za dola ya Marekani kwa kila uniti ambazo ni sawa na Sh 138.3.

Kiongozi huyo anayeondoka, anasema Tanesco huwauzia wateja wake umeme wa Songas senti 12 za dola ya Marekani kwa kila uniti ambazo ni sawa na Sh 276.6, kiasi ambacho kinaliwezesha shirika hilo la umma kupata faida kubwa.

“Tangu tuingie Mkataba wa Mauzo ya Umeme mwaka 2004, Tanesco imeweza kuzalisha mapato ya takriban dola milioni 500 za Marekani kutokana na umeme tunaowauzia,” Whittaker ameliambia JAMHURI na kuongeza kwamba gharama ya kuanzisha mradi huo ilikuwa dola milioni 320.

Kampuni ya Songas ambayo ilianzisha shughuli zake za biashara Julai 2004, inamilikiwa na wanahisa wanne ambao ni Kampuni ya Globeleg ya Uingereza yenye hisa asilimia 54.1, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) asilimia 28.69, Tanzania Development Finance Company Ltd (TDFL) asilimia 7.65 na Tanesco asilimia 9.56.

Kwa hivi sasa kampuni hiyo inaajiri watu 73 moja kwa moja na wengine zaidi ya 100 kupitia makandarasi inaofanya nao kazi. Mwaka jana Songas ilipata tuzo ya mwajiri bora kwa upande wa kampuni za kati kutoka kwa Chama cha Waajiri nchini (ATE) na kutangazwa kuwa mwajiri bora wa mwaka 2019 na TUICO.

Kuhusu mafanikio yake makubwa akiwa Tanzania, Whittaker anasema: “Ni kuwafahamisha Watanzania kuwa Songas ni rasilimali kubwa kwa taifa ambayo mchango wake madhubuti kwenye maendeleo ya nchi ulikuwa hautambuliki.”