Ningekuwa mbunifu mahiri wa kuandika hadithi, ningeandika hadithi ya vyura wa Kihansi kushangaa ni kwa kiasi gani binadamu wajinga mpaka kuwasafirisha vyura wenzao kwenda kuishi Marekani kwa muda.
Mradi wa kuzalisha umeme wa Kihansi ulipoanza, mwaka 2000, ulipunguza kiwango cha maji yaliyokuwa yakitiririka kwenye eneo walipokuwa wanapatikana vyura ambao uhai wao ulitegemea sana mvuke wa maji yaliyotokana na maporomoko ya Kihansi. Mvuke ulipopungua, vyura wakaanza kutoweka.
Lakini kabla hawajaisha wote, Serikali ya Tanzania iliwapa kazi wanasayansi ya kupendekeza hatua za kuwaokoa vyura hao. Ni kutokana na hayo mapendekezo vyura hao 499 wakapandishwa ndege na kupelekwa uhamishoni Marekani na kupokelewa na hifadhi ya wanyama ya Bronx katika jiji la New York.
Maisha kwa vyura nchini Marekani yalikuwa mazuri sana, vyura 499 wakazaliana hadi kufikia vyura 5,000 kwa taarifa za mwaka 2015. Suala la uzazi wa mpango halikuzingatiwa kabisa kwa sababu lengo lilikuwa kuongeza idadi ili kuhakikisha uwepo wao.
Walianza kurudishwa Tanzania mwaka 2010 na mfumo maalum ulibuniwa kwenye eneo lao la zamani ili kuweka mazingira yale yale yanayohitajika ili warudie maisha yao ya kawaida.
Gharama ya kuokoa vyura haikuwa ndogo. Ulibuniwa mradi na Benki ya Dunia ikaidhinisha mkopo kwa serikali ya Tanzania wa kiasi cha dola milioni 5.98 za Marekani kati ya mwaka 2013 mpaka mwishoni mwa mwaka huu.
Unapotafakari gharama kubwa ya kuhifahdi hawa viumbehai wa Kihansi, tafakari pia inakadiriwa kuwa watu sitini wanapoteza maisha duniani kila dakika kutokana na njaa. Hao ni watu zaidi ya milioni 30 kwa mwaka.
Somo dogo la kujifunza hapa ni kuwa uhifadhi una gharama kubwa sana.
Kwa wanasayansi na baadhi ya wasomi kisa cha vyura wa Tanzania kuishi kwa muda nchini Marekani, kwa gharama kubwa, siyo la kuandikiwa makala. Ni suala la wajibu tu. Tanzania imeridhia mikataba ya kimataifa ya kutunza na kuhifadhi mazingira ambayo inaongozwa na misingi mikuu miwili: kwanza, kwamba kila bayoanuwai (au uwepo wa wingi wa viumbehai kutoka kila eneo, kama ardhini na kwenye maji) inapaswa kuhifadhiwa na kulindwa ili isitoweke na; pili, inapotokea hali ya kuhatarisha kupunguka au kuwapo kwa bayoanuwai, kukosekana kwa uhakika wa kisayansi kusichukuliwe kama sababu ya kutochukua hatua za kuepuka au kupunguza athari hizo.
Maana yake ni wazi: kuelewa au kutokuelewa kwako umuhimu wa kuendelea kuwapo kwa chura wa Kihansi hakufuti jukumu la Serikali ya Tanzania ya kulinda uhai wao.
Tukifika hapo, somo la utunzaji wa mazingira na viumbe vyake linaanza kuwa gumu kuelewa. Ukizingatia kuwa mradi wa kuzalisha umeme wa Kihansi ungeweza kusitishwa bila kuwepo mikakati ya uhakika ya kuokoa vyura wa Kihansi, basi somo linazidi kuwa gumu.
Yapo masomo ambayo ni rahisi sana kuyaelewajuu ya utunzaji wa mazingira na yasiyohitaji hata kwenda shule kujifunza. Ni rahisi kufundisha athari za kutohifadhi mazingira kwa anayekata miti ovyo kwa matumizi ya kuni, na akaacha kupanda miti upya. Miaka inavyozidi kupita atalazimika kwenda mbali zaidi kutafuta kuni.
Zile athari za jumla na za muda mrefu za kuteketea kwa misitu hazimuathiri kwa haraka zaidi kama adha ya kutembea mwendo mrefu zaidi kusaka kuni. Hili somo rahisi sana kuelewa.
Hali kadhalika ni rahisi kumshirikisha binadamu anayepata magonjwa ya kupumua kwa sababu ya uchafuzi wa mazingira yanayoharibu hewa anayovuta. Atakuwa wa kwanza kujitokeza kuunga mkono jitihada za kulinda hewa ibaki safi.
Mvuvi anayebaini kupunguka kwa samaki anaovua kwenye ziwa kutokana na uchafuzi wa mazingira naye atakuwa mdau mzuri wa kutunza mazingira kwa sababu maisha yake yanahitaji kuwepo samaki.
Kipengele cha mikataba ya kimataifa kinachohimiza kutozingatia sana uwepo wa uhakika wa kisayansi kinaacha nafasi pana ya wadau na wanaharakati wa kutetea uwepo wa bayoanuwai kupinga kila hatua inayokisiwa kuathiri uwepo huo.
Katika jitihada hizi za kutunza mazingira lipo kundi la tatu la watu ambao wanaamini kuwa hatua za kulinda mazingira zinapaswa kuzingatia pia mahitaji halali ya maendeleo ya binadamu. Wengi wa wanaokata miti ovyo kwa matumizi ya kuni hawana nishati mbadala ya kutumia. Suluhisho la kupunguza kuteketea kwa misitu kunahitaji kuwapo kwa mbadala wa kuni.
Na ni hivyo kwa masuala mengi ya yale masuala ambayo ni dhahiri kabisa huathiri mazingira na hayahitaji uthibitisho wa kisayansi kuyatetea.
Mfumo muafaka wa utunzaji wa mazingira ungekuwa ni ule unaopima kwenye mizani mahitaji ya sasa na yale yajayo, bila kuathiri sana tunaoishi leo na wale watakaofuata.
Nina wasiwasi kuwa wakati mwingine tunalazimika kuathiri maendeleo yetu kwa sababu ya kulazimika kutimiza masharti ya kuridhia kwetu kwa ile mikataba ya kimataifa ya kuhifadhi mazingira.
Naamini katika kura ya maoni inayotaka Watanzania wachague kati ya uhai wa chura wa Kihansi na uwepo wa umeme wa uhakika, wengi wangeamua wanataka umeme wa uhakika.
Ukimuuliza msafiri wa basi kutoka Musoma kwenda Arusha kupitia Serengeti achague kati ya barabara ya lami na ile ya vumbi iliyopo, wengi watachagua ya lami. Lakini pamoja na kuwapenda sana Watanzania Serikali iliheshimu misingi ya uhifadhi na kuamua kuwa itajenga barabara hiyo kwa lami mpaka kwenye mipaka ya hifadhi na kutotandaza lami kwenye kipande cha barabara inayopita mbugani.
Lakini hata uamuzi huo wa serikali haukuwafurahisha wadau wa mazingira ambao wameendelea kushinikiza isiwekwe hata hiyo ya lami nje ya mipaka ya hifadhi kwa sababu wanaamini itaathiri maisha ya wanyamapori ndani ya hifadhi. Lakini wanafanya hivyo kwa sababu ya kuwepo kile kipengele kwenye mikataba ya kimataifa kinachosema hata inapokosekana sayansi ya uhakika, basi jitihada ziegemee kwenye kuhifadhi na si vinginevyo.
Mtaalamu mmoja wa wanyamapori aliniambia kuwa kelele za baadhi ya hawa wadau ni “siasa” zaidi, kwamba hakuna uthibitisho wa kisayansi kuwa nyumbu wa Serengeti watashindwa kuvuka barabara na Mto Mara kila mwaka kuelekea Kenya eti kwa sababu ipo barabara ya lami imejengwa nje ya mipaka ya hifadhi.
Leo tunapoadhimisha Siku ya Mazingira Duniani upo umuhimu wa kuunga mkono jitihada zote za dhati za kuhifadhi mazingira zinazolenga kutimiza malengo ya dhati ya utunzaji wa mazingira na siyo yale ya kufanikisha malengo mengine yaliyojificha nyuma ya harakati za kuhifadhi mazingira.
Hatimaye, tutashinda vita ya kuhifadhi mazingira kama wote tunakubaliana juu ya maudhui ya somo la mazingira.