Serikali ya Marekani imepongeza hatua ya makubaliano yaliyofikiwa na Somalia na Ethiopia ya kumaliza mivutano ya kikanda, iliyochochewa na shinikizo la Ethiopia la ufikiaji salama wa baharini.

Katika taarifa maalum iliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken, amesema Marekani imepongeza kwa  azimio hilo la Desemba 11 kati ya Somalia na Ethiopia linalothibitisha tena uhuru wa kila nchi, umoja, na uadilifu wa kimaeneo.

Blinken ameongeza kuwa Marekani ilikuwa inatazamia mazungumzo ambayo yangeelezea ufikiaji wa bahari wa Ethiopia huku ikiheshimu uadilifu wa eneo la Somalia.

Blinken amezihimiza nchi hizo mbili kuimarisha ushirikiano kwa maslahi ya usalama wa pande zote mbili hasa  mapambano dhidi ya kundi la al-Shabaab.

Waziri huyo pia ameishukuru Uturuki kwa kusimamia makubaliano hayo mapya.

Taarifa hiyo imetolewa wakati Blinken alipokuwa katika mazungumzo na rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan mjini Ankara kuhusu hali nchini Syria.

Hatahivyo, Umoja wa Afrika umezihimiza nchi hizo  kutekeleza bila kuchelewa  kwa makubaliano hayo muhimu yaliyofikiwa Desemba 11 yenye lengo la kumaliza mvutano kati ya mataifa hayo majirani.

Nchi hizo mbili zimekuwa na mzozo tangu Ethiopia isiyo na bandari ilipofikia makubaliano mwezi Januari na eneo lililojitenga na Somalia la Somaliland, kukodisha eneo la pwani kwa ajili ya ujenzi wa bandari na kambi ya kijeshi kitendo ambacho kilizua taharuki kubwa kwa Somalia na hivyo kuzusha hofu ya kuzuka kwa mzozo wa kikanda.