”Kama mtu fulani angeniambia kuwa siku moja ntakuwa Papa, ningesoma kwa bidii”
Mtunga mashairi wa Uingereza George Gordon Byron Noel [1788-1824] alipata kuitumia kalamu yake kuandika hekima hii, ”Tone moja la wino wa kalamu linawafanya mamilioni ya watu kufikiri”. Ninaomba uisome makala hii kwa utulivu mwanana ilikusudi ikupatie tafakuri itakayobadilisha historia yako ya maisha kuanzia sasa.
Unapokuwa mvivu wa kusoma vitabu, magazeti na majarida mbalimbali yenye tafiti za kisomi haumkomoi jirani yako, haumkomoi ndugu yako wala haumkomoi mwajiri wako bali unayakomoa maisha yako binafsi.
Ngoja nikupe ushauri wa bure siku ya leo. Ushauri wangu kwako ni huu: ‘Soma vitabu ili usiwe mzigo kwa familia yako, jamii yako na taifa lako’. Mtu asiyesoma vitabu ni kama marehemu anayeishi, lakini asiyejifahamu kuwa ni marehemu anayeishi.
Toka kwenye kundi la marehemu wanaoishi kwa kusoma vitabu. Kama unapenda kuwa marehemu anayeishi: ”Acha kusoma vitabu”. Siku moja rafiki yangu alinitembea nyumbani kwangu, alipofika nilimkaribisha kwenye maktaba yangu ya vitabu.
Alishangaa sana kuona lundo la vitabu vya kila aina akasema, ”Mr. William, Vitabu vyote hivi unavisoma?”. Nikajibu, ‘Ndio navisoma vyote’. Akasema, ”Wewe na vitabu, vitabu na wewe”.
Padre Faustine Kamugisha anasema, ”Siwezi kuishi bila vitabu”. Utumie usemi huu wa Padre Faustine katika maisha yako. Hebu na wewe sema, ‘Siwezi kuisha bila vitabu’. Vitabu ni bustani ya hekima. Vitabu ni kisima cha maarifa. Vitabu ni taa ya maisha. Vitabu ni kioo cha kuyatazama maisha.
Vitabu ni mwalimu, rafiki, mshauri na mhubiri. Nyumba iliyo na wapumbavu wengi ni nyumba isiyo na utamaduni wa kusoma vitabu. Nyumba ambayo haina vitabu inakosa marafiki wa zamani. Nyumba ambayo haina vitabu ni kama nyumba ambayo haina madirisha. Nyumba isiyo na vitabu ni kama kiota cha ndege.
Mtume Paulo alimshauri Timotheo kwa maneno haya, ”Ufanye bidii katika kusoma” [1Timotheo 4:13]. Tuusambaze utamaduni wa kusoma vitabu, magazeti na majarida kwenye familia zetu. Ukiweza kuwarithisha watoto wako utamaduni wa kusoma vitabu utakuwa umewawashia mshumaa usioweza kuzimwa na upepo wala mvua.
Ukiweza kuifundisha jamii yako utamaduni wa kusoma vitabu utakuwa umeifunulia siri ya kujitambua. Ifundishe familia yako umhimu wa kusoma vitabu. Mfundishe rafiki yako umuhimu wa kusoma vitabu. Wafundishe wafanyakazi wenzako umhimu wa kusoma vitabu.
Ifundishe jamii yako umhimu wa kusoma vitabu. Mfundishe mwanafunzi wako umhimu wa kusoma vitabu. Wewe Askofu, Padre, Katakista, Mchungaji, na Shehe wafundishe waamini wako umhimu wa kusoma vitabu.
Mwandishi Albert Bartholin alipata kuandika hivi, ”Bila vitabu Mungu yuko kimya, haki inalala, sayansi ya asili inasimama, falsafa inachechemea, herufi zinakuwa bubu na mambo yote yaliyo magumu yanakuwa giza”.
Na mwandishi Henry Miller anathibitisha hivi, ”Kitabu si tu rafiki. Kinakufanyia marafiki. Unapomiliki kitabu kwa akili yako na roho yako unatajirishwa. Lakini unapompatia na mwingine unatajirishwa mara tatu”.
Baba wa Taifa la Tanzania, Mwalimu Julius K. Nyerere alikuwa msomaji mzuri wa vitabu. Alikuwa anasoma vitabu na alikuwa mwandishi mahiri wa vitabu na makala. Unapokuwa mvivu wa kusoma vitabu unawahi kufa, na unapokuwa msomaji mzuri wa vitabu unachelewa kufa. Hapa nazungumzia kifo cha akili na sio kifo cha mwili. Soma vitabu akili yako ibaki inaishi milele. Andika vitabu hekima yako ibaki inaishi milele.
Kusoma vitabu ni kuzungumza na waandishi mashuri wa zamani na wa sasa. Mfano: Unapoisoma makala hii unazungumza na mimi [William Bhoke]. Unaposoma vitabu unakuwa na mazungumzo na watakatifu, watu wenye hekima, marais mashuhuri wa zamani, waandishi mashuhuri, watetezi wa haki za binadamu, waalimu bora, wafanyabiashara mashuhuri na wanasiasa wazalendo wa zamani.
Unazungumza na wapigania uhuru, wanateolojia mashuhuri, wanafalsafa mashuhuri na wanasayansi mashuhuri, kutaja machache. Kwa mantiki hiyo, ni kwamba unaposoma vitabu unazungumza na waandishi mashuri duniani kama Mwalim Nyerere, Plato, Hegel, St. Thomas Aquinas, Fulton J. Sheen, St. Jerome, St. Heronimo, Tertulian, Ben Carson, Robert Kiyosaki, Hellen Keller, Yohane Paulo II, Charles Darwin na wengine wengi.
Ukibahatika kuniona na kuniuliza maisha ni nini, nitakujibu; ‘Maisha ni vitabu’. Ukiuliza siri ya mafanikio yangu ni nini, ntakujibu; ‘Siri ya mafanikio yangu ni vitabu’. Soma vitabu ili uwe miongoni mwa binadamu wanaojitambua. Vitabu vinamsaidia mtu kufikiri na kufanikiwa.
Maisha yamejaa maswali tata ambayo hayajibiwi kwa hisia na vionjo vya mwili bali kwa kusoma vitabu na kutafakari. Maendeleo na maana ya maisha hupimwa kutokana na yale mawazo yaliyomo ndani ya vichwa vya watu. Tunawasifia sana Wazungu kwamba wanaweza kuishi mazingira ya aina yoyote.
Ukweli ni kwamba wanaweza kuisha mazingira ya aina yoyote kwa sababu wanapata hekima ya kuishi katika mazingira ya aina yoyote kutoka kwenye vitabu. Wanasoma sana na kufanya tafiti za kisomi ili kufahamu ni aina gani ya mazingira wanayoishi.
Mwanateolojia wa Kiangalikani, William Barclay anasema, ”Hakuna mazingira yasiyo na matumaini, ila kuna watu ambao hawana matumaini na mazingira yao”. Kwa mantiki hiyo ni kwamba hata ukiishi Ikulu kama hauna matumaini na mazingira ya Ikulu bado mazingira ya Ikulu yatakushinda.
Wenzetu wana matumaini na mazingira yao wanayoishi, ndio sababu wanamwagiwa sifa za kuishi na kustahimili hata kipindi cha baridi kali. Tunapashwa kuwa na matumaini na mazingira yetu tunayoishi. Hakuna tatizo linalokosa jibu katika jamii ya watu wanaotumia akili.
Ukweli ni kwamba jamii ya Kiafrika ina ugonjwa wa kutokusoma vitabu, magazeti na majarida mbalimbali. Huu ni ugonjwa mbaya sana na ndio ugonjwa unaomtambulisha Mwafrika kwa walimwengu wenzake. Mwafrika anasoma lakini elimu yake inaonekana kama ‘Ujinga ulioboreshwa’.
Mfano: Hapa kwetu Tanzania kuna wasomi wengi sana, lakini mchango wao kwa jamii hauonekani. Ni kama wana faida ya kuzaliwa na siyo faida ya kuishi. Kwa mwonekano mayai yote ya kuku wa kienyeji yanafanana, lakini mayai mengine ni mayai vinza.
Kuna baadhi ya wasomi wetu ni mayai vinza ya taifa. Usomi wao hauwasadii wao wenyewe na wala hausaidii jamii wanayoishi. Naishauri selikari yangu ya Tanzania itenge siku Maalumu ya kusoma vitabu, magazeti na majarida ili jamii yetu ijenge utamaduni wa kusoma.
Usipigepige mabawa kama kuku hali unaweza kuruka hewani kama tai. Kuna watu wanasema, ‘Mimi siwezi kusoma kwa sababu mimi sio mwanafunzi wala mwalimu’. Hizi ni sababu ‘bubu’. Hauwezi ukawa kiongozi mzuri kama hausomi vitabu. Hauwezi ukawa mshauri mzuri katika jamii kama hausomi vitabu.
Hauwezi ukawa na mtazamo chanya katika maisha kama hausomi vitabu. Hauwezi ukawa na moyo wa kuvumilia magumu katika maisha kama hausomi vitabu. Jibu la maisha lipo kwenye vitabu. Fungua kurasa za vitabu mbalimbali, utakutana na hekima, tiba na furaha. Tumtafute Mungu moyoni akikosa tumtafute kwenye vitabu atapatikana.
Mwandishi Michael de Montaigne alipata kusema hivi, ”Ninaposhambuliwa na mawazo ya kuleta huzuni, hakuna kitu kinachonisaidia sana kama vitabu. Vinanishughulisha kwa haraka sana na kuondoa mawingu katika akili yangu”. Vitabu ni tiba ya msongo wa mawazo.
Mtazamo sahihi ni sifa inayopatikana kwa njia ya kusoma vitabu. Naomba ujulikane, upendwe na uheshimiwe kwa kusoma vitabu. Hekima inayopatikana nje ya vitabu hiyo sio hekima.
Hauwezi kufika mbali pasipo kufunua mawazo ya waliokutangulia. Mawazo ya waliokutangulia unayapata katika vitabu. Unaposafiri, safiri na vitabu. Unapolala, lala na vitabu. Unapoamka, amka na vitabu. Unaposhauri, shauri na vitabu. Unapofundisha, fundisha na vitabu. Unapocheka, cheka na vitabu.
Soma sana vitabu. Vitabu vinabadili sumu kuwa dawa. Vitabu vinabadili chuki kuwa upendo. Vitabu vinabadili majivuno kuwa unyenyekevu. Vitabu vinabadili jangwa kuwa msitu. Vitabu vinabadili mlima kuwa tambarare. Vitabu vinabadili huzuni kuwa faraja. Kuna nyakati ngumu sana katika maisha ya binadamu. Nyakati zinazomuumiza zaidi mwanadamu ni zile nyakati ambazo anazotafuta hekima nje ya vitabu.
Mwanafalsafa Socrates alimzungumzia mtu anayesoma vitabu kwa maneno haya. Alisema: ”Mtu msomi ni mwenye sifa zifuatazo. Mosi, ni mtu anayeweza kuyatawala mazingira yake, badala ya mazingira kumtawala yeye. Pili, anakabiliana na hali zote kwa ujasiri. Tatu, anayashughulikia mambo yote kwa uadilifu. Nne, anadhibiti starehe zake na wala haharibiwi na mafanikio yake”.
Tukutane kwenye vitabu. Tufahamiane kwenye vitabu. Unaposoma vitabu unaona makosa yako ya jana na kubaini fursa za kesho. Unaposoma vitabu ni kwamba unayatazama maisha. Unaposoma vitabu unafuta historia ya kushindwa katika maisha yako. Unaposoma vitabu unaponya historia iliyokuumiza katika maisha yako. Unaposoma vitabu unaitazama kesho yako kwa matumaini.
Soma vitabu vina elimu ya kutosha juu ya jambo lolote jema unalopenda kulijua. Haijalishi ulikomea darasa la ngapi au una shahada ngapi, kujisomea ni wajibu mhimu kwa kila mtu. Watu wanaojisomea wana hekima na maarifa. Ikiwa una nafasi ya kwenda kuongeza elimu yako shuleni au chuoni, nenda bila kusita. Ukishindwa jinoe ukiwa nyumbani kwa kusoma vitabu mbalimbali. Hudhuria pia kwenye semina mbalimbali za kiroho, ujasiriamali na uongozi. Tukutane wiki ijayo.