Katika kikao cha Desemba 17-18, 2016 mjini Mpanda, Mkuu wa Mkoa Katavi alipiga marufuku ukataji miti katika maeneo muhimu kwa maisha ya Sokwemtu.
Binafsi nakubaliana na msimamo huo na kuunga mkono kwa asilimia mia moja amri halali ya Mkuu wa Mkoa juu ya watu wachache wanaofanya maeneo yenye misitu ya asili kugeka jangwa.
Isitoshe, wanapoona eneo fulani limeharibika kiasi cha kuweza kutumika kwa kujipatia riziki ya kila siku huliacha na kuhamia sehemu nyingine kendeleza hiyo dhana ya uharibifu wa misitu asilia na mazingira kwa ujumla.
Naomba wasimamizi wengine wa mazingira katika maeneo wanamoishi, wakiwamo wabunge na wakuu wa wilaya wakemee kwa nguvu zote uharibifu wa misitu ya asili; siyo tu katika maeneo wanamoishi sokwe, bali hata katika maeneo ambayo yana misitu ya asili.
Sikatai binadamu tusitumie misitu ya asili, lakini tunapoitumia tuwe waangalifu na kujali mahitaji ya bidhaa za misitu kwa matumizi ya kesho na mahitaji kwa vizazi vijavyo.
Kwa maneno mengine, tutumie rasilimali misitu na rasilimali ardhi tuliyopewa na Mwenyezi Mungu kwa misingi endelevu kwa faida yetu na vizazi vijavyo. Tumwombe Mwenyezi Mungu atupe hekima na busara ili uamuzi wetu uwe ni yenye tija kwa kizazi hiki na vizazi vitakavyokuja.
Kulingana na sera na sheria tulizonazo za kuhifadhi wanyamapori ni wajibu wetu kama taifa, kuhakikisha kunakuwapo utunzaji na usimamizi endelevu wa rasilimali wanyamapori; kama urithi wa watu wa Tanzania na ulimwengu mzima.
Kwa mantiki hiyo, ni wajibu wa kila mmoja wetu kuhakikisha urithi tuliopewa na Mwenyezi Mungu, kwa Tanzania kuwa na wanyamapori wengi na misitu ya asili iliyosheni mimea na viumbe hai ambavyo havipatikani sehemu nyingine duniani isipokuwa nchini mwetu tu; ni jambo la kujivunia sana na hivyo kufanya kila linalowezekana ili urithi huu tuwarithishe Watanzania watakaotufuata.
Tumethubutu, tunaweza na sasa tusonge mbele kwa kutofumbia macho uharibifu wa mazingira kwa nyanja zote za maisha yetu ya kila siku. Kilimo chetu nchini kote kiwe endelevu na chenye tija kwa kutumia eneo dogo la ardhi na kuzalisha mazao mengi.
Vilevile, ufugaji wetu uwe wenye tija na na wa kibiashara kwa kuwa na mifugo michache yenye tija kuliko kuwa na mifugo mingi isiyomsaidia mfugaji kwa mapato.
Kuwa na mifugo ni jambo jema na kizuri katika maisha yetu; na kama hivyo ndivyo, lazima fikra zetu zibadilike na kuweza kufuga kwa kuzingatia umuhimu wa mifugo hiyo kwa maendeleo ya familia mojamoja, jamii na taifa.
Hili litawezekana iwapo wafugaji watatengewa na watapewa maeneo ya kufugia kulingana na uwezo wa ardhi ndani ya kijiji.
Wafugaji watakaokwenda kinyume wachukuliwe hatua za kisheria kulingana na sheria za nchi pamoja na sheria ndogondogo (by-laws) kwenye halmashauri za wilaya na serikali za vijiji na vitongoji.
Halmashauri za vijiji na wanajijiji wanatakiwa kuzingatia farsafa ya matumizi endelevu ya rasilimali ardhi na maliasili zilizopo juu ya ardhi ya kijiji husika.
Utekelezaji wa falsafa hii ni kwa kupitia uandaaji na usimamizi wa mipango ya matumizi bora ya ardhi ili kuepuka migogoro isiyokuwa na tija katika matumizi ya rasilimali zilizopo vijijini.
Wafugaji wakiwa na maeneo yao rasmi na wakulima wakawa na maeneo yao ya kilimo, kukawapo maeneo rasmi ya makazi, pia kwa ajili ya huduma za kijamii na sehemu zenye misitu iliyohifadhiwa kulingana na uamuzi ulioidhinishwa na Mkutano Mkuu wa Kijiji; hakuna sababu ya kuwapo mapigano au ugomvi kati ya wakulima na wafugaji.
Serikali kwa ujumla wake – Serikali Kuu na Serikali za Mitaa- na watalaam wote katika sekta za umma na sekta binafsi kwa pamoja tuweke nguvu katika kufanikisha jambo hili muhimu kwa ajili ya kuwezesha maendeleo endevu ndani ya nchi yetu.
Misitu ya asili inapozidi kuteketezwa, ardhi ikaendelea kuharibika; maji katika mito yakakauka; ukame kila mahali ukazidi na usalama wa chakula ukalegalega; tutakimbilia wapi? kwa sokwe na wanyamapori wengine hali itakuwa mbaya zaidi. Tumerithi nasi tuwarithishe wajao.