Wakazi wa kisiwa kidogo cha Kokota katika Wilaya ya Wete kisiwani Pemba, wameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kwa kushirikiana na washirika wa maendeleo kuwatatulia kero zilizokuwa zikiwakabili kwa muda mrefu.

Wakazi hao wapatao 370 wametoa shukurani hizo mbele ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Shariff Hamad (pichani), alipotembelea kisiwa hicho kwa ajili ya kukagua miradi ya maendeleo inayosimamiwa na Community Forest Pemba.

Katika risala yao iliyosomwa na Mwalimu Juma Ali Hamad, wamesema kwa kipindi kirefu walikuwa wakilazimika kufuata huduma za maji na elimu katika mji wa Wete, lakini wamefarijika baada ya kuja kwa miradi hiyo miaka miwili iliyopita.

Amefahamisha kuwa kwa sasa wanafaidika na huduma ya umeme wa nguvu za jua (solar power) ambapo kila nyumba imewekewa taa moja ya kuonea, maji safi na salama yanayotokana na uvunaji salama wa maji ya mvua, pamoja na kuwapo skuli mpya ya msingi ambayo tayari watoto wameanza kusomea.

Hata hivyo, wameiomba Serikali na wafadhili kuiendeleza miradi hiyo ili kila nyumba iweze kupata umeme kikamilifu, pamoja na kujenga kituo cha afya pamoja na nyumba za walimu ili kuondosha usumbufu kwa walimu wanaosomesha skuli hiyo ya kisiwa kidogo cha Kokota.

Mradi huo unaosimamiwa na Community Forest Pemba kwa ushirikiano na Community Forest International chini ya ufadhili wa Jumuiya ya Ulaya, pia unajishughulisha na utengenezaji wa majiko sanifu, upandaji miti na ufugaji.

Kwa upande wake, Maalim Seif amewapongeza washirika hao wa maendeleo kwa kuamua kupeleka huduma hizo katika kisiwa hicho, jambo ambalo pia limeisaidia Serikali katika mipango yake ya maendeleo.

Amesema Serikali itaendelea kushirikiana na wafadhili kuifanya miradi hiyo kuwa endelevu na kuwanufaisha wakazi hao na Taifa kwa ujumla.

Ameongeza kuwa miradi hiyo ni msaada mkubwa kwa wananchi na Serikali, na kwamba ni mkakati imara wa kukabiliana na uchafuzi wa mazingira, ikizingatiwa kuwa majiko sanifu yatapunguza matumizi makubwa ya kuni na ukataji miti ovyo.

Mwakilishi wa Community Forest International kutoka Canada, Dafmen Hardie, amesifu ushirikiano walioupata katika utekelezaji wa miradi hiyo, na kwamba dunia inajifunza suala la ushirikiano kutoka Zanzibar.

Amesema mafanikio ya miradi hiyo ni mfano wa kuigwa kwa kisiwa chote cha Pemba, Zanzibar, Tanzania na duniani kwa ujumla, na kueleza kuwa matunda ya miradi hiyo yatawanufaisha wananchi.

Naye Mkurugenzi wa mradi wa Community Forest Pemba, Mbarouk Mussa Omar, amesema lengo la kuu la mradi huo ni kuwasaidia wananchi wa Kisiwa cha Kokota kuondokana na matatizo yaliyokuwa yakiwakabili kwa muda mrefu.

Amesema katika kipindi cha miaka miwili tangu kuanzishwa kwa mradi huo, wamefanikiwa kujenga tangi la maji kwa ajili ya kuhifadhia maji ya mvua, ambayo huyasafisha na kuyaingiza kwenye tangi yakiwa tayari kwa ajili ya matumizi ya kawaida ya kupikia na kunywa.

Ameyataja mafanikio mengine waliyoyapata kuwa ni pamoja na ujenzi wa skuli ya msingi, kuweka mitambo na kutumia umeme wa nguvu za jua, kutekeleza mradi wa utengenezaji wa majiko sanifu, kuhamasisha ufugaji wa nyuki pamoja na upandaji wa miti.

Mbali na Kisiwa cha Kokota, Makamu wa Kwanza wa Rais pia alitembelea maeneo mbalimbali kukagua miradi ya maendeleo inayosimamiwa na Community Forest Pemba ikiwamo kituo cha mradi kilichoko Minyenyeni, mradi wa upandaji miti na utengenezaji wa majiko sanifu wa Wingwi Mapofu, pamoja na mradi wa ufugaji nyuki na kilimo cha mbogamboga wa vijiji vya Hindi na Kambini.