Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali amesema Serikali imeweka uwekezaji mkubwa wa miundombinu ya Afya kutokana na umuhimu wa sekta hiyo kwa jamii.

Rais Dk.Mwinyi ameyasema hayo Ikulu, Zanzibar alipozungumza na Meneja Mwandamizi wa Mfuko wa dunia (Global Fund), Dk. Sara Asiimwe na ujumbe wake ulioongozwa na Waziri wa Afya, Nassor Ahmed Mazrui.

Aidha Rais Dk.Mwinyi ameishukuru “Global Fund” kwa jitihada zake za kuiunga mkono Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuisaidia kwenye masuala mbalimbali ya Maendeleo ikiwemo Sekta ya Afya.

Halikadhalika, Rais Dk. Mwinyi ameeleza juhudi za  “Global Fund” kuisaidia Zanzibar kwenye sekta ya Afya na nyengine za maendeleo ni kuendeleza jitihada za Serikali anayoiongoza katika kutekeleza adhma ya Serikali kutoa huduma bora za afya.

Akizungumzia huduma ya bima ya Afya kwa wageni wanaoingia Zanzibar, Rais Dk. Mwinyi, ameieleza “Global Fund” dhamira ya Serikali kuja na bima hiyo kutokana na umuhimu wake kwa wageni, hivyo ameuomba Mfuko huo kuangalia namna ya kuiungamkono Serikali.

Naye, Dk. Sara Asiimwe alimueleza Rais Dk. Mwinyi kwamba “Global Fund” inafanyakazi kwa karibu zaidi na Serikali ya Mapinduzi ya  Zanzibar kupitia Sekta zake za Maendeleo ikiwemo Wizara ya Afya. Aidha, aliiahidi Serikali kwamba taasisi yao itaendeleza ushirikiano wake na Zanzibar hasa kwenye miradi ya maendeleo.

Please follow and like us:
Pin Share