Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) ipo katika hatua za mwisho za mchakato wa manunuzi ya boti mpya mbili za kisasa zinazokwenda kasi zitakazofanya safari kati ya Tanga, Pemba, Unguja, Dar es Salaam na Mombasa nchini Kenya.

Taarifa hiyo imetolewa leo Agosti 19, 2024 na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla alipozungumza na wanachama na wafuasi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Pangani mkoani Tanga.

Makamu wa Rais Abdulla alisema uundwaji wa boti hizo unatarajia kukamilika ndani ya  miezi mitatu ijayo na zitafungua njia zaidi za uchumi kati ya Zanzibar na maeneo zitakapokwenda ikiwemo Tanga.

Alisema manufaa ya boti hizo yatachochewa zaidi na kukamilika kwa Bandari ya Shumba kisiwani Pemba ambayo kutokana na ukaribu wake na Mombasa, Tanga itakuwa miongoni mwa wanufaika wa mtandao huo wa usafiri wa majini.

Aidha alisema baada ya kuwasili na kuanza safari kwa boti hizo atashirikisha nia ya kuwepo safari za kupitia Pangani kama ilivyowasilishwa na Waziri Aweso, kuwa ni miongoni mwa mahitaji ya wakazi wa wilaya hiyo.

Awali Waziri wa Maji na Mbunge wa Jimbo la Pangani, Jumaa Aweso aliiomba serikali kuwasaidia kupatikana kwa boti ya uhakika ya mwendokasi katika wilaya hiyo Ili iweze kurahisisha usafirishaji kati ya wilaya hiyo pamoja na visiwa vya Pemba na Unguja.

“Mlezi wetu nikuombe utusaidie kwani mazingira ya Pangani pamoja na Zanzibar yanalingana hivyo iwapo tutapata boti ya uhakika ya mwendokasi tutaweza kufungua fursa za kimaendeleo katika wilaya ya Pangani”alisema Waziri Aweso.