“Kinachoonekana ni kwamba CCM na Serikali yake hawana dhamira ya kuleta Katiba mpya.”

Kwa upande wake, Mjumbe wa Tume ya Katiba, Profesa Mwesiga Baregu, amesema Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Samuel Sitta,  atashindwa kuliongoza Bunge hilo kutokana na kufuata maagizo ya chama chake.

Amesema Sitta alianza kuonesha kuyumba baada ya kuvunja Kanuni za Bunge hilo tangu mwanzo, baada ya kuruhusu Rais Kikwete kuhutubia baada ya Jaji Warioba kuwasilisha Rasimu ya Katiba.

“Tumenza kuona kuyumba kwa Sitta, ile siku alipovunja Kanuni za Bunge, kwani Mwanasheria Mkuu alipendekeza Rais aanze halafu Jaji Warioba awasilishe Rasimu yake, lakini ilibadilishwa ghafla na hivyo Warioba kuwasilisha kabla ya ufunguzi, jambo ambalo si sawa,” amesema Profesa Baregu.

Amesema kubadilishwa kwa ratiba hiyo kulifanywa kwa makusudi ili Rais Jakaya Kikwete  aweze kujibu mapigo kwa Tume.

Akizungumzia hotuba hiyo ya Rais Kikwete, Profesa Baregu amesema kwamba hotuba hiyo italeta mitafaruku ndani ya Bunge hilo kwa kuwa imekuja kinyume cha kanuni.

“Naweza kusema haya ni matumizi mabaya ya madaraka, hotuba ile haikuwa mahali pake,  alitakiwa kuitoa katika mikutano ya CCM na si katika vikao vya Bunge, sasa ameleta mitafaruku ndani ya Bunge kitu ambacho si sahihi.

“Alitakiwa kushauri na kuwajengea umoja, upendo na mshikamo,  pia alitakiwa kujua kuwa katika Bunge hilo kuna vyama vingi na vina wenyeviti wake, kama kila mwenyekiti angetakiwa kujibu hoja si ingekuwa vurugu hapo maana yake wangepishana kauli,” amesema.

Ameongeza kuwa  maneno ya Kikwete katika hotuba hiyo yanaweza kupanda mbegu ya chuki kwa wabunge wa CCM dhidi ya wale wa upinzani.

“Mchakato wa kutunga Katiba unaendeshwa kwa sheria, Rais aliteua Tume, Tume ikakusanya maoni kwa wananchi, tukampa nafasi hata yeye ya kutoa maoni, tukaandaa Rasimu ya Kwanza tumempelekea rasimu tukaijadili naye, Rasimu ya Pili, Rais anatakiwa kuheshimu maoni ya wananchi na siyo Jaji Warioba,” amesema Profesa Baregu.

Mjumbe wa Bunge la Katiba, Julius Mtatiro, amesema Rais hakwenda kulihutubia Bunge hilo la kihistoria lenye mchanganyiko wa Watanzania wa makundi, mitizamo na itikadi tofauti kama Rais, bali kama Mwenyekiti wa chama.

Amesema hotuba yake ilikuwa na lengo la kuwatisha wananchi kuwa Serikali Tatu zitaleta vita na matatizo makubwa.

“Kwa bahati mbaya, katika mchakato huu wa Katiba, binafsi nilishasema interest yangu siyo Muungano, na mara kadhaa nimesema kwamba hata kama tukiwa na serikali 10, tatu, mbili au moja, sioni kama ina uhusiano wowote na kina mama wanaolala lundo hospitalini na wala haina uhusiano na baba yangu kupata chakula cha usiku au kulala njaa.

“Kilichonisikitisha sana ni kumuona mkuu wa nchi akiweka msimamo wa chama chake katika baadhi ya masuala muhimu na zaidi akitumia muda mwingi kuichambua rasimu na kuelekeza namna sahihi inavyopaswa kuwa.

“Kwa mtizamo wangu, Rais hakupaswa kuichambua rasimu mbele ya wajumbe na kuchukua upande katika jambo hilo,” amesema na kuongeza kuwa ikiwa Rais ana misimamo yake katika rasimu hiyo, anapeleka ujumbe kwa wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kufuata upande wake, na kwa sababu wengi wa wajumbe si weledi na wachambuzi wazuri wanaweza kuibeba hotuba yake na kufuata kile alichosema.

Amesema Rais Kikwete kama Mkuu wa nchi, ndiye aliyeanzisha mchakato huu na ameuunga mkono kila ulipokwama, sasa mchakato umefika mahali ambapo wajumbe wanapaswa kutulia na kuamua bila vishawishi vya wenye mamlaka, amekuja na msimamo wake na kisha kuwaeleza wajumbe waamue wakati ameshawapa msimamo.

“Kwa mtizamo wangu, Rais wetu alikuja kufanya kazi kubwa ya kuponda mawazo thabiti ya Jaji Warioba, Salim Ahmed Salim, Dk. Mvungi (kwa sasa ni marehemu), Profesa Baregu na wazalendo wengine wengi ambao wanaijua nchi hii vizuri mno, lakini kwa matakwa ya hali tuliyomo walilazimika kuweka pembeni misimamo yao na kuja na rasimu ya wote.

“Rais anapoipondaponda rasimu husika ina maana ya kukanyaga kazi kubwa ya Tume na kuyasaga maoni ya wananchi kwa imani ya chama chake.

“Laiti kama Jaji Warioba na wenzie wangelijua kitakachotokea, nina hakika wangekataa kutumika kufanya kazi kubwa sana ambayo inakuja kutupwa jalalani na aliyewatuma,” amesema.

Amesema Rais alipaswa kujua kuwa anahutubia Taifa ambalo lina mawazo tofauti na Bunge ambalo lina mitizamo tofauti.

“Kuja na hotuba ambayo ina misimamo ya chama chake ni kudharau kundi kubwa la Watanzania wenye misimamo tofauti kwa sababu aliahidi kuwa Katiba ya sasa inaandikwa na utashi wa wananchi wenyewe ni vema angeacha kuweka misimamo ili kusaidia wananchi na hata wajumbe wa Bunge la katiba kufikiri kwa uhuru mpana,” ameongeza.

Naye Mjumbe Bunge hilo, Profesa Abdallah Safari, amemshangaa Rais Kikwete kuzungumzia msimamo wa chama chake badala ya mambo ya msingi ya kitaifa.

“Dakika kumi za mwanzo alianza kunipa matumaini, lakini baada ya muda huo nikashangaa anaongea vitu ambavyo havikuwa na msingi wowote, kuna mambo mengi alitakiwa kuongea pale,” amesema.