*Hotuba ya Kikwete, kupinda kanuni vyamkaanga

*Wapinzani wapoteza imani naye, wadai ni wakala

*Wasema Bunge hili ni kikao cha CCM, bora livunjwe


Mwenyekiti wa Kudumu wa Bunge Maalum la Katiba, Samuel Sitta, ana wakati mgumu.

Uchunguzi uliofanywa na Gazeti JAMHURI, umebaini kuwa hatua ya Sitta kufanya mbinu akabadili Kanuni za Bunge la Katiba na kubadili ratiba ya Rais Jakaya Kikwete kulihutubia Bunge, imewapunguzia wengi imani juu yake.

Ukiacha mchezo mchafu wa kubadili kanuni kwa nia ya kumwezesha Rais Jakaya Kikwete kuziba mashimo yaliyoachwa na Jaji Joseph Warioba, wapinzani walioshiriki kampeni za kuhakikisha Sitta anashida, sasa wanasema wamepoteza imani na wanaona atakuwa anapokea maelekezo kutoka CCM.

Wachambuzi wa masuala ya Katiba wanasema ukiacha udhaifu huu aliouonesha Sitta kwa kubadili kanuni bila kutumia vikao, sasa amejitengenezea mazingira magumu ya kuendesha kikao cha Bunge, kwani kila uamuzi atakaokuwa anaufanya utatiliwa shaka kwa kurejea jinsi alivyovunja kanuni.

Awali, kanuni ilikuwa inataka Rais Jakaya Kikwete ndiye ahutubie Bunge kwanza, kisha Jaji Warioba awasilishe Rasimu ya Katiba bungeni, lakini katika kinachoonekana kujiandaa kumdhibiti Jaji Warioba, CCM ilifanya mbinu Jaji Warioba akalazimika kuwasilisha Rasimu kwanza na kama ilivyotarajiwa Rais Kikwete alipofika akaichanachana vipande Rasimu hiyo.

Rais Kikwete alitoa msimamo wa chama chake, CCM, na kushangiliwa kwa nguvu kuwa wao wanasimamia Serikali Mbili. Hili na mengine aliyosema Rais Kikwete kama ukomo wa kugombea ubunge, kuondoa suala la mafuta katika Muungano na Zanzibar kuruhusiwa kuendesha ushirikiano wa kimataifa bila kuomba kibali cha Muungano, yanatajwa kuwa yatamtesa Sitta wakati wa kujadili rasimu.

Mbunge wa Karatu, Mchungaji Israel Natse (CHADEMA), ameikosoa hotuba hiyo ya Rais Kikwete kwamba ina upungufu mkubwa wa kuibeba CCM, badala ya kusimama katika mhimili wa Serikali.

“Rais ameonekana ku-act kama Mwenyekiti wa CCM badala ya nafasi yake ya urais. Kanuni zinasema Rais afungue Bunge kwanza halafu shughuli nyingine zifuate, lakini haikuwa hivyo,” amesema Mchungaji Natse, ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani wa Wizara ya Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu).

Ameongeza, “Hotuba ya Rais haikuzungumzia kitu chochote kuhusu ufunguzi [wa Bunge Maalum la Katiba], badala yake imejibu Rasimu ya Katiba.”

Mbunge huyo ameeleza kusikitishwa kwake na hatua ya Rais Kikwete ya kuisifia Rasimu ya Katiba alipokabidhiwa miezi kadhaa iliyopita, lakini ameigeuka na kuipiga teke wiki iliyopita bungeni.

“Inashangaza kuona Rais wa nchi, chombo alichokiunda [Tume ya Mabadiliko ya Katiba] anakifuta hadharani licha ya kukisifia mwanzoni,” amesema Mchungaji Natse.

Kwa upande mwingine, mbunge huyo wa Karatu amelifananisha Bunge Maalum la Katiba na Mkutano Mkuu wa CCM.

“Kama maoni ya wananchi yanapigwa teke licha ya kugharimu fedha nyingi, kuna sababu gani ya kuwa na Bunge la Katiba?” amehoji na kuongeza: