Ili Waafrika weusi sisi tupate maendeleo katika nchi zetu, hatuna budi kujitafiti na kujitambua upungufu wetu wote. Upungufu wa kutamani kuwa kama Mzungu au Mwarabu haujaondoka katika fikra zetu ingawa wakoloni hawapo; lakini kwa mazoea yetu sisi Mzungu ni wa kuogopwa tu.

Mzungu anaelezwa tangu kwao kwamba Waafrika wanaogopa Wazungu, nenda kaishi kama Mzungu kulinda hadhi yetu. Nina mfano wa kijana kutoka Sweden au Norway. Sikumbuki sawa sawa. Aliajiriwa Idara ya Misitu. Huko nyuma Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii katika mikutano yake ya kikazi nchi za Nordic, alitembelea nyumbani kwa huyu afisa mtarajiwa. Nyumba yao ilikuwa mlimani mbali kabisa na ufukwe wa bahari; ilikuwa ya mbao na choo cha shimo la mbao.

 

Kijana yule alipofika Tanzania mwaka 1973 kama utaratibu wa General Orders aliwekwa hotelini New Africa Hotel kwa siku saba za mwanzo wakati Wizara ikimwombea nyumba Utumishi Housing “A”. Siku ya sita alioneshwa nyumba yake pale Oysterbay Madai Cresent-Bungalow Batchelors’ Quarters. Eti akatikisa kiberiti!, “Hapa ilipo hakuna view nzuri, sioni bahari na ni nyumba ndogo siitaki, nitafutiwe nyumba ya hadhi yangu”.

 

OS wa Maliasili na Utalii aliripoti kwa wakubwa wake na hatimaye habari zilimfikia yule Katibu Mkuu. Bila kumung’unya maneno yule Katibu Mkuu alimwita Balozi wa nchi ile na kumwambia Wizara haina nyumba mbadala, hivyo kijana wake aingie mle au arudi kwao Ulaya. Ifikapo kesho Serikali haitamlipia zaidi pale New Africa Hotel. Balozi alimfokea yule Afisa Misitu na kumtaka ahamie katika nyumba aliyopewa mara moja. Yule Mzungu hakukumbuka kuwa yule Katibu Mkuu alifika kibandani kwao kule Ulaya na kuona kajumba familia yake ilimoishi.

 

Balozi alimkumbusha yule kijana kuwa je, pale anapoishi mama yake ni sawa na nyumba hii ya hapa Dar es Salaam? Kijana alihamia jioni ile ile. Wanatakiwa maafisa wenye uzoefu na wenye kujiamini kuwaonesha Wazungu kuwa enzi za utawala wa wakoloni weupe ulishapita, sasa wafuate usemi, “In Rome do as the Romans do” – fuata hali ya mahali, si kung’ang’ania ya kwenu tu! Hii inaonesha Waafrika tu binadamu kama Wazungu na tunatakiwa kujaliwa, kuaminiwa, kuogopwa na kutumikiwa kama weupe. Tuachane na wazo la kuwatetemekea Wazungu kwa kila kitu.

 

Upungufu mwingine ni ulevi wa kupindukia. Waafrika wasomi waache pombe za Kizungu na wachape kazi kwa kadri ya elimu na uwezo wao. Kule Lusaka, Zambia, Mmarekani fulani kutoka Benki ya Dunia alidharau sana wasomi Waafrika kwa kuwasema walikuwa wapiga maji sana (walevi) wala hawakujishughulisha kamwe na kuboresha elimu yao wala mazingira yao kama wasomi.

 

Hawajiendelezi wala hawafanyi utafiti wa kuisaidia nchi yao kiuchumi. Kwa muda wa miaka mitatu aliyokaa Lusaka aliona walevi wengi sana miongoni mwa wasomi – urithi kutoka kwa Wazungu – beer, whisky, brandy, gin na cognac. Je, huo ndiyo Uzungu? Upungufu mwingine ni ile tabia yetu ya kujipendelea, yaani ubinafsi. Tusipobadilika na kuacha hiyo hisia ya umimi na kulifikiria Taifa kwanza kuliko nafsi zetu, basi hatutakuwa tumepiga hatua ya kujikwamua. Hili la ubinafsi ndilo linalozaa udugunaizesheni na upendeleo ofisini. Ni tabia ya kujilimbikizia mali viongozi wenyewe, koo na jamaa zao. Wakikaa madarakani wanasita hata kustaafu wasije wakaumbuliwa maovu yao nje ya ofisi zile.

 

Upungufu mwingine ni ukosefu wa lugha moja katika Taifa. Nchi nyingi za Afrika hazina lugha moja ya kitaifa, isipokuwa sisi Watanzania tunayo lugha ya Taifa – KISWAHILI. Nchi nyingine karibu zote licha ya kuwa huru wanatumia lugha ya mtawala wao wa mwisho – Kiingereza (Anglophone countries), Kifaransa (francophone countries), Kireno (lusophone countries) na Kispaniola eti ndizo lugha za kitaifa!

 

Ukosefu wa lugha ya Taifa unazaa mfarakano mkubwa katika Taifa na watu kukuza ukabila zaidi katika uchaguzi. Wengi wanafuata makabila yao na kupeana madaraka kimakabila.

 

Mwisho, nadhani msingi imara wa kila Taifa ni UZALENDO. Kila Taifa lijijengee moyo huo wa utaifa. Kupata umoja wa Taifa lenyewe na kuweza kujenga uchumi wao ili wajitegemee badala ya kuwa ombaomba kwa nchi zilizoendelea. Viwanda, kilimo, madini katika kila nchi ndiyo chimbuko la mtaji wa maendeleo. Rasilimali hizi kweli zinalisaidia Bara huru la Afrika? La muhimu hapa ni kuchapa kazi kwa manufaa ya Taifa na si kutorosha rasilimali za nchi nje kuwanufaisha wageni.

 

Umaskini wetu mkubwa ni ukosefu wa kufikiri ili kupambanua nini muhimu kwa maendeleo ya mwananchi. Huu umasikini wa fikra umetudumaza sana Waafrika weusi. Je, Waafrika weusi tulimwelewa Mwalimu Nyerere aliposema, “education means liberation of the mind? “Tumefumbuka kweli kifikra na kuuthamini weusi wetu, uwezo wetu wa kazi na kadhalika? Waarabu wote wale wa Afrika Kaskazini wamekuwa “liberated” ndiyo sababu kila taifa — Misri, Libya, Tunisia, Morocco na Algeria — wamekuwa tofauti na sisi Waafrika kusini mwa Jangwa la Sahara ukiondoa Afrika Kusini kwa Mzee Madiba na Zuma.

 

Tusiuthamini Uzungu wala Uarabu zaidi kuliko Uafrika wetu huu. Kule Marekani, Wanegro wamekuwa wakidai watambulike kwa wenzao Wamarekani weupe kwa miaka mingi karne na karne, lakini hadi leo hii bado wanabaguliwa kwa ile rangi yao tu kuwa nyeusi. Weusi imekuwa balaa, ndiyo sababu wanajaribu hata kutumia vipodozi kujichubua kupata weupe kama alivyofanya mwanamuziki Michael Jackson alivyobabuka ilimradi wabadilike kuwa Wazungu. Waafrika WEUSI TUKOJE jamani?  Mwalimu Nyerere anasema, “our greatest weakness is that of spirit and mind. This is the problem of our generation” (Nyerere on Education vol. II pg 77). Tatizo hili la kihisia kwetu Waafrika hatuwezi kulimaliza?

 

Watu weupe — Wazungu na Wamarekani — wanaona Waafrika wana tatizo la kujijua, wao wanaita “Lack of Black African Cultural Identity”. Katika tatizo hili watu weupe kwa ujumla wao wanaona kama vile Waafrika hasa wasomi tunaelekea kuukana Uafrika wetu na kung’ang’ania kule tulikopatia elimu yetu. Kwa maneno yao, nanukuu wanasema, “Educated Blacks tended to imitate all the traits of the white group with which they were most closely associated. In British controlled Africa, educated Blacks became black British intelligentsia, those in French dominated areas became Frenchmen. In America, Blacks acquired the traits of their white compatriots, and so on all over the World”.

 

Yaani weusi wasomi wameiga sana yake ya weupe waliowatawala. Waliotawaliwa na Waingereza wameiga mila na desturi za Waingereza na kuwa Wazungu weusi, waliotawaliwa na Wafaransa wamekuwa Wafaransa na Wareno ndiyo wamekuwa wakijichanganya na Wareno hata wanaitwa “Maasimilado” yaani Wareno weusi; waliotawaliwa na Wabelgiji nao wamelowea mila na desturi za Kibelgiji. Mzungu mmoja kule Dakar, Senegal, Bi. A. Doris Banks Henries amethubutu kuandika katika “PRÉSENCE AFRICAINE” kule Paris maneno haya, “White was a symbol of esteem, progress and everything desirable: while black was associated with evil, stupidity, backwardness and all that was low and degrading. Generations of blacks became ashamed of all the characteristics of their race”.

 

Haya tena kwa tafsiri yangu Bibi A. Doris Banks Henries anasema weupe ndiyo ulikuwa ishara au alama ya enzi au utukufu na maendeleo na kila jema ulimwenguni. Weusi ulikuwa alama ya uovu au ulilinganishwa na uovu, upumbavu au uzuzu, kutokujiamini, ulofa na uduni — watu wa hali ya chini. Vizazi kwa vizazi vya weusi wameona aibu au wamekuwa na soni kwa hali hiyo ya taifa lao hilo jeusi.

 

Kwa mtazamo namna hiyo wa Wazungu na kwetu sisi weusi kuonea haya weusi wetu, ndipo najiuliza tena sisi watu weusi tukoje? Kama alivyosema Mwalimu Nyerere, “This is the problem of our generation”. Na kweli tuna tatizo katika kizazi hiki. Je, mnaona kwenye runinga vijana wetu wanavyoshabikia BONGO FLAVOR? Mavazi ya wana muziki wa kigeni na michezo yao, mitindo ya nywele na uozo wote wa mambo ya kigeni? Mmomonyoko wa maadili unaanzia hapo pa kuukataa Uafrika na kuukumbatia Uzungu/Uarabu au kwa ujumla mambo ya kutoka nje ya Bara letu la Afrika. Tunaondokaje hapo?

 

Mimi namshukuru sana yule mjukuu aliyeniletea kitabu “Waafrika Ndivyo Tulivyo?” Yeye ni Mhadhiri pale Chuo Kikuu kitivo cha Uhandisi. Wewe msomaji wangu umewahi kukisoma au kile cha ‘False Start Africa?’ Ikiwezekana jaribu kupanua mawazo yako kwa kusoma moja ya vitabu hivyo. Kwa hili naungana na ndugu yangu Deodatus Balile, SITANII. Ngozi nyeusi tumezidi ulimbukeni! Mpaka lini hali hiyo? Mbona tumejitawala tangu mwaka 1961? Kwanini bado tunauhusudu Uzungu tu? Tubadilike kifikra tuwe “liberated mentally” na tuwe Waafrika weusi.