*Baadhi wadaiwa ‘kuzikacha’
Matumizi ya nyumba za mawaziri jijini Dar es Salaam yamegubikwa na siri nzito. Inadaiwa kuwa baadhi ‘wamezitosa’ kwa kisingizio cha kukosa usiri.
Ukaribu wa nyumba moja hadi nyingine walizojengewa na Serikali katika maeneo ya Victoria na Mikocheni, unatajwa kuwa ndiyo sababu kuu ya baadhi ya mawaziri kutofurahia kuishi huko.
“Baadhi ya mawaziri hawakupenda kuishi kwenye nyumba hizo kutokana na kujengwa karibu karibu kiasi cha kutolinda siri za familia zao,” kimesema chanzo cha habari.
“Unajua, masuala ya wakubwa hayahitaji kujulikana sana, yanahitaji usiri, ndiyo maana baadhi hawapendi kuishi pamoja kiasi kile,” kimedokeza chanzo kingine. Habari zaidi zinaeleza kuwa baada ya kukabidhiwa nyumba hizo, baadhi ya mawaziri walizikabidhi ama kwa watoto wao, au ndugu na jamaa zao, na wao kurejea kuishi kwenye nyumba zao binafsi.
Inaelezwa kuwa baadhi ya mawaziri kwa sasa wanakazania kujiimarishia maisha katika nyumba zao binafsi, ikiwa ni pamoja na kuendesha miradi ya uzalishaji mali.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ujenzi Tanzania, Elius Mwakalinga, amesema hana taarifa za baadhi ya mawaziri kutoishi katika nyumba walizokabidhiwa.
Hata hivyo, Mwakalinga amesema kuna nyumba iliyopaswa kutumiwa na waziri lakini wamekabidhiwa maofisa wa tume ya kuchunguza wizi katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA).
Mwakalinga hakuwa tayari kusema waziri aliyepaswa kuishi kwenye nyumba hiyo anaishi wapi.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano katika Wizara ya Ujenzi, Martin Ntemo, amesema kitendo cha baadhi ya mawaziri kuonekana mara kwa mara katika nyumba zao binafsi wakisimamia miradi mbalimbali, ndicho kinachosababisha baadhi ya watu kudhani hawaishi kwenye nyumba za Serikali.
“Unajua viongozi kama hawa (mawaziri) lazima wajipange katika makazi yao binafsi,” amesema Ntemo.
Kwa upande wake, mkazi wa Tabata, Dar es Salaam aliyezungumza na JAMHURI kwa sharti la kutotajwa jina, amekosoa hatua ya Serikali kuwajengea mawaziri nyumba katika eneo moja kwamba ni hatari kiusalama. Mwananchi huyo ametofautiana na Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya Jamhuri Media Limited, Deodatus Balile, ambaye anaunga mkono utaratibu huo wa Serikali.
“Ni vigumu kuimarisha ulinzi kwa mawaziri wanaoishi maeneo tofauti. Lakini ni rahisi kuwaimarishia ulinzi wanapoishi pamoja,” amesema Balile.
Kwa mujibu wa Ntemo, Serikali ilitumia Sh bilioni tisa kugharamia ujenzi wa nyumba 82 kwa ajili ya makazi ya mawaziri.
“Lengo la mpango huu wa Serikali ni kuhakikisha kuwa viongozi na hasa mawaziri, makatibu wakuu na wakurugenzi wanakuwa na mahali bora na salama pa kuishi kwa mujibu wa kazi zao,” amesema Ntemo.
Amesema gharama za ukarabati wa nyumba hizo hutoka katika bajeti za matumizi ya kawaida kwenye wizara husika kila mwaka.
“Wapo viongozi ambao wana makazi yao binafsi Dar es Salaam na Dodoma, lakini wizara inahusika na nyumba za Serikali pekee,” ameongeza.
Hata hivyo, Ntemo naye hakuwa tayari kueleza ni mawaziri wangapi wanaoishi na wasioishi kwenye nyumba hizo kwa sasa.
Kwa upande mwingine, wakazi wa maeneo ya Victoria, Mikocheni na Kijitonyama waliozungumza na JAMHURI, wameeleza kuridhishwa na huduma za maji, umeme na ulinzi zinazotolewa katika maeneo hayo kutokana na uzito wa viongozi hao.