Swabaha Shosi, ambaye wiki iliyopita alimweleza Rais John Magufuli namna anavyosumbuliwa na vyombo vya utoaji haki, kwa sasa analindwa na vyombo vya ulinzi ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais.
“Kwa kweli nashukuru, nimepewa ulinzi, ninao,” amesema Swabaha alipozungumza kwa simu na JAMHURI.
Tofauti na kile kinachosambazwa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii, Swabaha amesema kuwa ana haki zote za mirathi ya mumewe, marehemu Mohamed Shosi Yusuf.
Mjane huyo ameweza kulionesha JAMHURI nyaraka kadhaa, ukiwamo wosia ambao anasema umeghushiwa na genge la watu wanaotaka kumdhulumu yeye na wanafamilia wengine wenye sifa za kurithi kisheria.
Swabaha anasema yeye ni mke halali wa marehemu Shosi, kwa kuwa hata Mahakama, mbele ya Jaji Lugazia, ilithibitika hivyo.
“Kwenye kesi ya Jaji Projest Lugazia, niliwasilisha vyeti vya ndoa vya BAKWATA, vya Serikali (RITA) na ikaonekana mimi ni mke halali. Huyo anayesema ni mke wa marehemu Shosi alitakiwa awasilishe vyeti akasema kasahau nyumbani. Jaji akamwuliza inawezekana vipi aende shamba bila jembe? Akapewa muda awasilishe vyeti, akashindwa hadi kesi ilipokwisha na hukumu kutolewa.
“Mimi ndiye mke wa marehemu Shosi kwa sababu niliwasilisha hata Power of Attorney nilizotumia kusimamia masuala mbalimbali ya mume wangu wakati akiwa hai. Sasa hizi taarifa za kwamba mimi ni tapeli ni kunichafua tu kwa sababu wanajua wao ndiyo matapeli wanaotaka kudhulumu hizi mali,” anasema.
Miongoni mwa nyaraka hizo ni nakala ya uchunguzi wa Polisi Kitengo Maalumu kinachoshughulika na makosa ya jinai (Forensic) na nakala ya cheti cha ndoa. Anasema baada ya kubaini wosia umeghushiwa, aliona ni vema vikatumika vyombo vya kisheria kubaini ukweli.
Katika ‘wosia’ huo unaodaiwa kuandikwa na Mohamed Shosi, Polisi walichunguza saini iliyo kwenye ‘barua ya mirathi’ na kubaini kuwa ilighushiwa. Makosa 12 yameainishwa na mtaalamu wa forensic.
Kazi hiyo ya kitaalamu ya kugundua makosa ya kihalifu ilifanywa Julai, 2013 na Mrakibu Msaidizi wa Polisi, Amani Saad, kutoka Idara ya Uchunguzi wa Makosa ya Jinai, Makao Makuu ya Polisi jijini Dar es Salaam.
“Mimi Amani Renatus Saad, ambaye ni Mrakibu Msaidizi wa Polisi, katika kitengo cha forensic Idara ya Uchunguzi wa Makosa ya Jinai, kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Polisi, Dar es Salaam, nikiwa nimefundishwa na kufuzu kwa mujibu wa fasili ya Sheria ya Ushahidi, Cap 6 (R.E.2002) ambaye pia ni ofisa niliyefuzu katika utambuzi wa miandiko kwa kutumia vifaa maalumu, nimegundua makosa kadhaa,” inasomeka sehemu ya taarifa ya Polisi.
Wanatajwa Alfred Akaro na Abubakary Shaban, kuwa ni kati ya walioshiriki kughushi barua hiyo ya mirathi, na kwa sababu hiyo Jeshi la Polisi liliwafungulia mashitaka ya jinai. Hata hivyo, Swabaha anasema Shaban ameingizwa kwenye kesi hiyo ili kuvuruga ushahidi kwa sababu hahusiki.
“Wahusika ni Wakili Akaro; Karani wa Baraza la Ardhi na Nyumba, Pili Kondo, na Karani wa Wakili Akaro anayeitwa Luciani Wisso. Hawa waliweka saini kwenye mirathi ya kughushi wakithibitisha kuwa wakati marehemu anaandika mirathi (ya kughushi), walikuwapo.
“Mtu anayetajwa kuwa ndiye msimamizi wa mirathi ya mume wangu, ni Humud Mohamed Ali – huyu wala si ndugu yetu, alikuwa mpangaji tu. Nikawa nahoji iweje Pili na Luciani wasishitakiwe kwa kula njama kuweka saini kwenye mirathi wanayojua kuwa ni ya kughushi?
“Lakini pia Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Tanga anayeitwa Balisidya (a.k.a Dakika Tatu), alishatoa hukumu mbili tofauti kwa kesi ile ile moja na kwa tarehe ile ile moja. Hizi zote ni njama za kunidhulumu,” anasema na kuongeza:
“Kwenye hukumu ya kwanza akasingizia kuwa mama wa marehemu kafariki dunia. Tulipokata rufaa akabadili hukumu. Kesi hiyo hiyo, tarehe hiyo hiyo; alitoa hukumu akijua mama wa marehemu – mama mkwe yu hai.”
Swabaha anasema haikuwa kazi rahisi kwa Polisi kuwashitaki Akaro na Shaban, kwani alilazimika kwenda ngazi za juu serikalini kueleza hilo jambo na ndipo walipoweza kufunguliwa mashitaka.
Juni 20, mwaka jana, Swabaha alimwandikia barua Waziri wa Sheria na Mambo ya Katiba, Dk. Harrison Mwakyembe, akimshukuru kwa kusaidia kuandaliwa kwa hati ya mashitaka ya shauri la Jinai namba 10 la mwaka 2016, dhidi ya Akaro na Shaban.
Swabaha anasema shauri hilo limekuwa likipigwa ‘danadana’ na Ofisi ya Upelelezi Mkoa wa Tanga tangu mwaka 2012 hadi malalamiko yake yalipomfikia Dk. Mwakyembe, miaka minne baadaye na hatimaye shauri hilo kupelekwa mahakamani Januari 20, mwaka jana.
Katika barua yake ya Januari 16, mwaka huu kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju, Swabaha alimwomba aingilie kati kile anachokiita ‘mchezo mchafu’ unaofanywa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) wa kutaka kuharibu shauri hilo.
“Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka inaonekana kufanya mbinu za kuharibu kesi kwa kumsaidia mmoja wa watuhumiwa ambaye pia ni wakili, DPP hajachukua hatua zozote tangu nimplekee malalamiko kwake, ikiwa ofisi yake ndiyo iliyotayarisha hati ya mashtaka,” inasomeka sehemu ya barua hiyo.
Msingi wa kumlalamikia DPP unatokana na kitendo cha walioandaa mashtaka dhidi ya Akaro na Shaban (wanaodaiwa kughushi wosia wa marehemu Mohamed Shosi Yusuf), kutoingiza shitaka la kula njama (conspiracy).
Anasema kwa kuwa suala la kughushi barua ya mirathi lilihusisha watu zaidi ya mmoja, ni wazi kuwa hapo kulikuwa na mpango wa kula njama.
“Mwanasheria Mkuu, malalamiko yangu nimeyafikisha katika ofisi ya DPP na Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), na kuwaona uso kwa uso bila mafanikio yoyote, mara ya mwisho wakili wangu alimwandikia DPP barua ambayo mpaka sasa haijapatiwa majibu.
“Ofisi ya Mwanasheria wa Serikali Tanga walijitoa kwa barua yao ya Septemba 26, 2016, yenye kumb namba AGC/C.1/V/15 kwa maelezo kwamba uchunguzi kuhusiana na malalamiko yangu pamoja na hati za mashtaka ziliandaliwa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) Makao Makuu,” inasomeka sehemu ya barua ya mjane huyo.
Katika barua hiyo yenye kurasa tatu, Swabaha anahoji kitendo cha yeye kama mke wa marehemu, watoto wake na mama wa marehemu kutokuwa sehemu wa warithi.
JAMHURI limeona barua iliyoandikwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu yenye Kumb.Na. AGC/C.1/V/15, ikikiri kupokea barua ya mlalamikaji, Swabaha.
“Tumepitia pia hati ya mashitaka iliyoandaliwa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka na kuridhika kuwa hati hiyo ya mashitaka haina dosari, kwani ushahidi uliokusanywa jaladani unawagusa zaidi mshitakiwa wa kwanza Afred Akaro na mwenzake Abubakary Sadiki.
“Hata hivyo, baada ya kupitia jalada halisi kwa makini, kumbukumbu zinaonesha kuwa mnamo tarehe 15/11/2012 lilifunguliwa jalada la uchunguzi kuhusiana na malalamiko ya ndugu Hamoud Mohamed kufanyiwa fujo na Swabaha Mohamed. Jalada hilo lilikuwa ni TAN/IR/3160/2012 ambapo na wewe Swabaha ulifungua jalada TAN/IR/3160/2012 linalohusu kughushiwa kwa wosia unaodaiwa kuandikwa na Mohamed Shosi,” inasomeka sehemu ya barua hiyo iliyosainiwa na Wakili wa Serikali Mfawidhi, Saraji Iboru.
Barua hiyo ambayo imeainisha mwenendo wa sakata zima la Swabaha, inasema upelelezi ukiendelea kuhusu tuhuma za kughushi wosia, Swabaha alionekana kutoridhishwa na taratibu za kipelelezi katika Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Mkoa (RCO) wa Tanga, hivyo akamwandikia barua Inspekta Jenerali wa Polisi ili jalada halisi la shauri hilo liweze kuitishwa Makao Makuu ya Polisi, Dar es Salaam.
“Hivyo ofisi yetu inapenda kukutaarifu kuwa uchunguzi kuhusiana na malalamiko yako na kuandaa hati ya mashitaka ziandaliwe na Ofisi ya Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai na Mkurugenzi wa Mashitaka Dar es Salaam na kwa mujibu wa kumbukumbu zinavyoonesha, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mkoa wa Tanga ni watekelezaji tu wa yale yaliyoamuliwa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka,” inasomeka sehemu ya barua hiyo.
Maisha ya Swabaha na Shosi
JAMHURI: Lini na wapi uliolewa na Shosi?
SWABAHA: Nilifunga ndoa mwaka 1993. Tulifungia Lumumba, Dar es Salaam. Aliyetufungisha ndoa ni Sheikh Abdallah Bassasar.
JAMHURI: Mlibahatika kupata watoto wangapi?
SWABAHA: Watoto wawili.
JAMHURI: Mama mkwe wake yuko? Kama yupo kwenye mvutano huu yuko upande upi?
SWABAHA: Mama mkwe yuko hai. Kwenye wosia huu wa kughushi alikuwa ametolewa kabisa. Mahakama ya Mwanzo kwenye kesi iliyoendeshwa na Hakumu Balisidya pale Tanga, hukumu ilionesha amefariki dunia. Yuko hai na anaishi Barabara ya 20 Tanga. Anaitwa Fatuma Khamis Chalenja. Vita kubwa nampigania mama mkwe maana maisha yake ni ya shida. Haiwezekani mali za mwanawe zichukuliwe na watu wengine tu, tena wasiokuwa na uhusiano hata kidogo.
JAMHURI: Kina nani wanaostahili kurithi mali za marehemu Shosi?
SWABAHA: Wanaostahili ni mimi Swabaha, watoto na mama wa marehemu. Marehemu mume wangu Shosi tulioana kindugu, mimi ni mke-ndugu.
Wengine wanaostahili kupata mirathi ni watoto wake wengine aliowazaa, japo ilikuwa nje ya ndoa, kiungwana sharti nao wapate maana hakuwahi kuwabagua. Watoto wake wengine jumla yake ni kama 14. Hawa aliwazaa kwa mama wengine sita au saba hivi. Sina hakika sana, lakini mwenye cheti cha ndoa, mke halali ni mimi. Lakini kwenye mirathi hii watoto wote itabidi wapate.
JAMHURI: Mumeo Shosi alikuwa na mali kiasi gani na ziko wapi?
SWABAHA: Alikuwa na nyumba Bombo (Tanga), viwanja viwili Tanga (kimoja kipo Jet, na kingine kipo Barabara ya Pili). Ana viwanja viwili Korogwe. Hapo kimoja kauziwa Habat Dafa. Hicho kiwanja kilikuwa na kesi na. 64 ya Baraza la Ardhi na Nyumba, Korogwe. Ameuziwa na hawa walioghushi mirathi. Hati yake ni Na. 1/1/1999 ambayo ilitolewa kwa mume wangu kisheria kabisa.
Nilipobaini kimeuzwa, nikafungua kesi Mahakama ya Mwanzo wasimamishe. Nikaonesha mipaka ya michongoma. Hakimu kasema Dafa alimradi kakichukua, na kwa kuwa mume wangu (Shosi) amefariki dunia, basi Dafa aendelee tu. Waliochukua hela kwa Dafa ni upande wa pili unaonga’ng’ania mirathi.
Kiwanja kingine kipo Korogwe karibu na Shosi Hotel. Huyo mama Mariam Juma (anayedaiwa pia kuwa mke wa marehemu Shosi) na wanawe – Saburia na Mohamed Shosi – walimpangisha askari anayeitwa Rich Mshane (trafiki).
Amemwaga kifusi na lami. Nilipoenda Korogwe kasema kapangishwa na Saburia. OCD akamwita, akatoa nyaraka za kupanga. Usimamizi wa mirathi batili ukaletwa wa Suburia. Akaleta hukumu, akaleta na hukumu ambayo iko tofauti na yetu sisi ya Mahakama ya Mwanzo (orginal) kwenye kesi Na. 220/2016 ambayo ina hukumu mbili tofauti. Nikaenda polisi maana hukumu ziko tofauti.
Saburia na mama yake (Mariam) walienda Airtel wakachukua saini za wanafamilia, wakaandika muhtasari kuwa ni wasimamizi wa mirathi. Wakamtilisha saini mtoto wa miezi miwili aitwaye Afua na cheti cha kuzaliwa tunacho. Huyu mtoto alizaliwa 23/9/2012 na akatia saini 20/11/2012! Fikiria mtoto wa miezi miwili anaweza kutia saini kwenye muhtasari wa mirathi?
Haya, mtoto wa pili alizaliwa 19/3/2007 Korogwe, anaitwa Lea. Huyu naye akaweza saini kwenye hati hizo! Nayasema haya kwa sababu hata vyeti vya kuzaliwa vya watoto ninavyo. Mtoto mwingine ni Mohamed Mohamed Shosi ambaye wakati huo alikuwa chini ya miaka 18, lakini eti naye akasaini muhtasari wa mirathi.
Kwa hiyo, wakaenda Airtel wakasaini – Saburia na mama yake kwa kutumia muhtasari feki. Wakasaini, wakawa wanaenda kutoa hela nikatokeza. Kesi hadi leo haijapelekwa mahakamani. Huku ni kughushi, lakini hawajapelekwa mahakamani kushitakiwa.
Wakaenda Arusha wakachukua hela kwenye kampuni ya Kibo Seed na kuikodisha kwenye nyumba niliyojenga mimi na marehemu. Ipo karibu na Annex Hotel.
Mali nyingine ni viwanja viwili vipo Mkumbara – kimoja kina nyumba hadi kwenye lenta na kingine bado.
Eneo la Manga Mikocheni, Tanga kuna kiwanja kinachochimbwa madini ya jasi; Mkomazi pia kuna kiwanja cha madini ya jasi, lakini hakijaanza kazi; Mgombezi kuna shamba la katani kubwa.
“Alikuwa na magari, photocopy machine za kibiashara, televisheni, kompyuta, AC, jokofu; hoteli ya Shosi inaendelea ipo Korogwe na mali nyingine nyingi.
Alivyojipenyeza na ujumbe wake kwa Rais Magufuli
Swabaha alimweleza Rais Magufuli namna anavyotishiwa maisha kwa kutumiwa ujumbe mfupi wa maneno kutoka kwa wabaya wake na pia kuzungushwa kila anakokwenda kwa nia ya kudai haki.
Mjane huyo alisubiri Rais Magufuli amalize hotuba yake na ndipo ghafla, huku mshereheshaji akiendelea na matangazo, akatoa bango la kitambaa lililokuwa na ujumbe uliokuwa ukimsihi Rais Magufuli amsaidie asidhulumiwe haki yake inayotaka kunyang’anywa na Polisi, Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) na Mahakama.
Sehemu ya bango hilo la kitamba aliloliinua juu ili Rais apate ujumbe uliopo, lilisomeka, “Rais Magufuli naomba unisaidie. Polisi, DPP, Mahakama wanataka kuninyang’anya haki yangu”.
Ujasiri wa Swabaha ulitaka kumponza baada ya wanausalama kumzonga na kujaribu kumtoa eneo hilo.
Baadaye, Rais Magufuli akaamuru Swabaha apewe nafasi ili amweleze shida yake, huku Rais akisisitiza kuwa kufanya hivyo ni sahihi kwa sababu “ndiyo siku yenyewe ya Mahakama”.
Baada ya kupata nafasi hiyo, huku akilia kwa kwikwi, Swabaha alianza kusimulia kwa kueleza kuwa mumewe aitwaye Mohamed Shosi alifariki mwaka 2012 na kwamba, tangu wakati huo amekuwa akizungushwa katika Mahakama ya Wilaya mkoani Tanga kuhusiana na mirathi. Alieleza kilio chake kwa takribani dakika 13.
Swabaha alimtuhumu wakili mmoja kuwa ndiye aliyeshiriki katika kuandaa wosia bandia wa mumewe kwa nia ya kufanikisha dhuluma dhidi yake.
Alidai wakili huyo amekuwa akishirikiana na watu wenye fedha ambao wamekuwa wakitumia nguvu zao kiuchumi, kukwamisha haki yake hata pale alipofuatilia kwenye maeneo yote muhimu ya kufuatilia haki yake kuhusiana na jambo hilo.
Uchunguzi wa JAMHURI umebaini kwamba Swabaha anacho cheti kinachothibitisha ndoa yake na marehemu Mohamed Shosi, cheti kilichotambuliwa na Wakala wa Usajili, Ufilisi, Udhamini (RITA).
Mama huyo mjane alisema marehemu mume wake alikuwa na wanawake wawili wa ndoa na kwamba yeye na huyo mke mwenzake, kila mmoja ana cheti halali cha ndoa.
“Mimi leo nimeamua kuja hapa nikijua kama kufungwa na nifungwe, na lolote na liwe… Mheshimiwa Rais, naomba unisaidie.” Amesema Swabaha, akiomba watu hao wenye fedha wasiachwe wamdhulumu haki yake, yeye mjane kwa sababu ya umasikini wake.
Baada ya mjane huyo kumaliza maelezo yake, Rais Magufuli alimwambia amemsikia na hapo hapo akatoa maelekezo kwa IGP, Ernest Mangu, ikiwa ni pamoja na kumhakikishia mjane huyo ulinzi.
“Kesi anazozizungumzia mama huyo bado zinaendelea mkoani Tanga na nilimkabidhi DCI ambaye naye alizungumza na DPP kwa kuwa upelelezi ulikuwa umekamilika,” amesema Mangu.
Mara baada ya IGP Mangu kutoa maelezo yake, ndipo Rais Magufuli alipotoa maagizo yake kuhusiana na suala hilo, na ambayo kwa kiasi kikubwa yalijaa mwanga wa matumaini juu ya kupatikana suluhu ya jambo hilo.
Rais Magufuli alitoa maelekezo kwa ofisi za DPP, AG na Jaji Kiongozi kulishughulikia kwa haraka suala hilo, huku akitaka kesi ya mjane huyo ihamishiwe haraka kutoka Mahakama ya Wilaya na kupelekwa katika mahakama za juu.
“Kama kesi ipo Mahakama ya Mwanzo kule muivute haraka haraka…ishughulikiwe haraka na IGP pia uishughulikie,” amesema Magufuli.
Swabaha azungumza na ‘JAMHURI’
Akizungumza na JAMHURI, Swabaha amesema, amefurahi sana kuona amesikilizwa na Rais John Magufuli na kwamba ana imani sasa haki itapatikana. “Nimefurahi sana, namshukuru sana Rais Magufuli kwa kusimama na sisi wanyonge, nina imani sasa hata suala langu litasikilizwa na haki itatendeka.
“Bado nipo Dar es Salaam, lakini nimeambiwa nisiongee na waandishi, nimeambiwa nipumzike. Mahakama sasa wananisimamia na mambo yanakwenda vizuri…namshukuru sana Rais Magufuli kwa usaidizi alionipatia, hapa sasa nina ulinzi kwa saa 24,” amesema Swabaha.