Aliokota chuma chakavu kusaka ada

“Baada ya dhiki faraja,” ni msemo ambao unaakisi maisha halisi ya msanii maarufu nchini kwa jina la kisanii ‘Sir Nature’. Msemo huu una maana sana kwa Sir Nature kutokana na madhila, majanga na misukosuko lukuki aliyokutana nayo katika maisha tangu akiwa mdogo.

Kama ilivyo kwa watu wengine, Sir Nature aliamua kujikwamua kimaisha ili naye aishi kama wengine – katika raha. Mungu si mchoyo, kutokana na juhudi zake, Sir Nature alifanikiwa hadi kufikia hatua ya kuwa mtu wa kutegemewa katika familia yake.

Jina lake halisi ni Juma Kassim Ally. Alizaliwa mwaka 1980 katika Hospitali ya Ocean Road, jijini Dar es Salaam na kupata elimu ya msingi katika Shule ya Kurasini,  wilayani Temeke mkoani humo.

Hata kabla ya kuwa msanii, fikra zake tangu akiwa shule ya msingi zilitawaliwa sana na kucheza kandanda badala ya kuzingatia masomo darasani.

Tangu akiwa mdogo, Sir Nature aliamini kabisa hakuna fani nyingine ambayo ingeweza ‘kumtoa’ katika maisha, ila soka pekee.

Kutokana na ugumu wa maisha ya uswahilini, Sir Nature alisoma kwa shida. Ingawa alimaliza elimu ya msingi, lakini  kwa misukosuko mingi.

Kutokana na hali hiyo, Sir Nature hakufanikiwa kufaulu mtihani wa darasa la saba, na kwa kuwa wazazi wake hawakuwa na uwezo, walishindwa kumlipia elimu ya sekondari katika shule binafsi ambazo zilikuwa ni za gharama kubwa.

“Elimu ya ‘kibongo’ bila kuwa na mpango mbadala wa masomo ya ziada (tuition), ni vigumu kufaulu. Wenzangu waliokuwa na wazazi wenye uwezo wao, walisonga mbele mimi nikaishia hapo,” anasema Sir Nature.

Kutokana na familia yake kutokuwa na uwezo wa kumsomesha, licha ya yeye binafsi kuwa na moyo wa kusoma, Sir Nature alilazimika kufanya kila aliloweza ili ajiunge na masomo ya sekondari.

Mwaka uliofuata alifanya kila juhudi zikiwa ni pamoja na kuzunguka majalalani kusaka chuma chakavu.

“Nilikuwa nikiishi uswahilini, biashara ya kwanza wakati ule kwa watoto kama mimi, ilikuwa kuuza chuma chakavu, hivyo nilikuwa kiguu na njia kutafuta malighafi hiyo na kuuza, lengo likiwa kutafuta ada,” anasema Sir Nature.

Hata hivyo, kazi hiyo ya kukusanya na kuuza chuma chakavu haikumwezesha kupata fedha nyingi za kumwezesha kulipa ada ya shule. Akaamua kujiingiza katika shughuli ya kugonga kokoto maeneo ya Kurasini, akiamini kuwa kazi hiyo ingempatia fedha zitakazomwezesha kulipa ada.

Hakuishia hapo. Tamaa yake ya kuendelea na masomo ilimfanya ajihusishe na shughuli nyingine nyingi kama vile kusukuma mkokoteni wa maji, kubeba mizigo, kucheza kamari, kuokota mkaa na kuuza vitumbua vya watu.

Juhudi zake hizo zikamlipa, kwani alifanikiwa kupata fedha za kulipia ada ya shule, hivyo akaweza kuendelea na masomo ya sekondari.

“Baada ya kukusanya fedha hizo zikawa kama kianzio kwa kulipia karo ya shule binafsi iliyopo maeneo ya Temeke,” anasema Sir Nature, japo haitaji shule hiyo.

Licha ya kurudi shuleni, Sir Nature hakuacha kuendelea kufanya kazi hizo ili kujikimu katika mahitaji mbalimbali ya shule, ikiwamo kulipia mitihani ya kila wiki, kununulia madaftari, vitabu na vifaa vingine muhimu.

Hakupenda kucheza mpira akiwa shuleni peke yake, Sir Nature alifikia kiwango cha kucheza soka katika timu nyingi za mitaani maarufu kama ‘chandimu’.

Mawazo yake ya kudhani kuwa soka ndilo lingemtoa katika maisha yaliyeyuka alipofika kidato cha tatu.

Sir Nature alipata marafiki kadhaa shuleni hapo, akawa akifuatana nao kwenda katika kumbi za starehe, ambako 

walikutana na vijana waliokuwa wakiimba kutoka shule mbalimbali.

Miaka hiyo ya 1990 wakiwa shuleni, ulikuwepo mpango maalumu wa waimbaji wa muziki kutoka shule moja kupelekwa katika semina ili kuhamasisha kujikinga na maradhi ya ukimwi, matumizi ya pombe na dawa za kulevya.

Sir Nature na wenzake walikuwa wakifanya uhamasishaji katika Ukumbi wa Amana Center uliopo Ilala, pamoja na Ukumbi wa Ruaha Galaxy uliopo Kimara, jijini Dar es Salaam.

Hapo ndipo alianza kutunga mashairi akioanisha na kile walichokuwa wakifundishwa.

Makala hii imeandaliwa kwa msaada mkubwa wa mitandao mbalimbali.

Mwandaaji anapatikana kwa simu namba: 0784331200, 0713331200, 0767331200 na 0736331200