Ripoti mpya iliyotolewa na Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa masuala ya Amani (SIPRI) imesema matumizi ya kijeshi duniani kote yameongezeka mwaka jana huku migogoro inayoongezeka ikichochea ongezeko la matumizi hayo.
Ripoti hiyo ya taasisi ya SIPRI yenye makao yake katika mji mkuu wa Sweden Stockholm iliyotolewa leo Jumatatu imesema matumizi ya kijeshi yameongezeka kote duniani kwa kasi zaidi tangu kumalizika kwa Vita Baridi na kufikia dola trilioni 2.7, huku ikisisitiza kuwa ongezeko kubwa la matumizi ya kijeshi limeshuhudiwa zaidi barani Ulaya na Mashariki ya Kati.
Ripoti hiyo imesema mataifa yote ya Ulaya kasoro Malta yameongezekamaradufu matumizi yao ya kijeshi huku Marekani ikisalia kileleni ambapo matumizi yake ya kijeshi yalifikia dola bilioni 997. Wakati vita nchini Ukraine vikiingia katika mwaka wake wa tatu, matumizi ya kijeshi yameendelea kuongezeka kote barani Ulaya, hadi kufikia asilimia 17 ambayo ni sawa na dola bilioni 693.
Mwaka 2024, Urusi iliongeza matumizi yake ya kijeshi hadi kufikia dola bilioni 149, Ukraine bilioni 64.7, Ujerumani iliongeza matumizi yake ya kijeshi kwa asilimia 28 hadi kufikia dola bilioni 88.5 bilioni, na kuiweka katika nafasi ya nne duniani. Mataifa mengine kama Israel yametajwa pia kuongeza matumizi yao ya kijeshi.
Xiao Liang, mtafiti wa Mpango wa Matumizi ya Kijeshi na Uzalishaji wa Silaha katika taasisi ya SIPRI amesema matumizi hayo ya kijeshi yamekuwa yakiongezeka katika nchi zaidi ya 100 duniani, jambo ambalo amesema ni la kushangaza mno na linalochochewa na kuongezeka kwa mivutano duniani na pia athari za migogoro inayoendelea. Aidha Liang ametahadharisha juu ya ongezeko hilo:
” Ongezeko hili la matumizi ya kijeshi ambalo halijawahi kushuhudiwa, litakuwa na athari kubwa sana kijamii, kiuchumi na kisiasa kwa sababu ili kufadhili ongezeko hilo kubwa, nchi zitatakiwa kuchukua maamuzi kuhusu bajeti zao. Kwa mfano, tumeshuhudia nchi nyingi za Ulaya zikipunguza matumizi mengine kama misaada ya kimataifa ili kufadhili ongezeko la matumizi ya kijeshi, na baadhi ya nchi zinajaribu kuongeza ushuru au kuelekea kwenye madeni ili kufanikisha hili la ongezeko la matumizi ya kijeshi.”
