Mwanamuziki anayetamba na kibao cha ‘Twende’, alichomshirikisha Barnaba Classic kinachoshika chati ya juu katika vituo mbalimbali vya redio na televisheni, Frank Ngumbuchi, maarufu Foby, amesema hana mpango wa kujiingiza kwenye ‘kiki’ zisizokuwa na maana.

Akizungumza na Gazeti la JAMHURI kuhusu kazi zake za sanaa, Foby amesema alianza kutambua kwamba ana talanta ya muziki mwaka 2012 wakati akiwa anasoma katika Shule ya Sekondari ya Ruhuwiko iliyopo Wilaya ya Songea, Ruvuma.

Foby ni tofauti na wasanii wengine katika tasnia ya muziki wa kizazi kipya. Si mtu ambaye anatangaza matukio yasiyo kuwa na tija ili yamvumishe kimuziki (kiki).

Akizungumza kuhusu siri ya kutopenda kiki, amesema malezi aliyoyapata ndiyo yamekuwa nguzo ya kumsaidia kujiheshimu kupitia muziki wake.

“Wazazi wangu wanafuatilia muziki wangu, sidhani kama inapendeza kufanya matukio yasiyo kuwa na maana ili niweze kulisimamisha jina langu. Kama unafanya vizuri hauna haja ya kutegemea kiki…kiki ni mbaya, nimekwishawahi kumshuhudia mwanamuziki mwezangu akikosa dili la biashara, kisa kiki,’’ amesema Foby ambaye licha ya kuwa na talanta ya kuimba muziki pia ni mcheza mpira wa miguu.

Wimbo wake wa ‘Star’ aliourekodi katika studio za C9, ulichagiza kumpatia mashabiki wengi ndani na nje ya nchi. Kutokana na tungo kali zilizomo katika wimbo huo ambao unamwelezea Foby kuwa baada ya nyota wawili wa Bongo Fleva kutamba kwa muda mrefu; Alikiba na Diamond yeye ndiye atakuwa nyota wa tatu.

Foby amesema umahiri wake umesababisha ‘lebo’ nyingi za muziki nchini kumtumia maombi ili aweze kujiunga nazo. Ameongeza kuwa juhudi zake binafsi zimemfanya akache kusainiwa katika lebo hizo kutokana na mikataba na masharti anayofikiri hayatamfanya akue kimuziki zaidi ya kumdidimiza.

Licha ya utunzi wake binafsi, Foby anasifika kwa kuwatungia wasanii wenzake nyimbo ambazo zimewafanya wavume na kuwatambulisha kupitia tasnia ya muziki wa kizazi kipya.

Miongoni mwa nyimbo alizowatungia wasanii wenzake ni wimbo wa ‘Madam Hero’ ulioimbwa na msanii Hamisa Mobetto.

“Nakumbuka mwaka 2016, nilidhamiria kuingia rasmi katika tasnia ya muziki, hapo ndipo nilipotoa wimbo wangu wa ‘Star’ ambao ulikuwa na mapokezi makubwa kwa wapenzi wa burudani na kunitambulisha katika tasnia ya muziki wa Bongo Fleva,” amesema.

Aidha, Foby ameliambia JAMHURI kuhusu safari yake ya muziki tangu ametoka Songea na kuingia jijini Dar es Salaam ili aweze kufanya shughuli zake kwa ufasaha kutokana na  upatikanaji wa studio kubwa na za kisasa za kurekodi muziki wake, watayarishaji na waandaaji wa video za muziki.

Amesema akiwa jijini Dar es Salaam alikumbana na changamoto nyingi na za kukatisha tamaa lakini aliendelea kupambana hadi leo muziki wake umeanza kumzalishia matunda kutokana na kumudu mahitaji yake mbalimbali.