Wale wanaofanya rejea ya hali ya kisiasa nchini mwetu watakumbuka Augustino Mrema alivyokuwa na nguvu kubwa kisiasa mwaka 1995. Wapo ambao wanaamini hadi leo kuwa kama si mbinu na ushawishi wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, historia ya leo ya nchi hii ingekuwa tofauti.
Mrema alikuwa na nguvu kubwa kisiasa. Alipendwa na alipata wafuasi wengi kuanzia kwa makabwela hadi kwa matajiri; wasiosoma na waliosoma. Wakati Mrema nyota yake ikiwa angavu, upande wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mwalimu Nyerere alipuuzwa. Huo ndio ukweli.

Hata gazeti la CCM lilimnanga Mwalimu kweli kweli. Maandishi hayafutiki. Yangali yapo. Wapo waliofikia hatua ya kumtaka anyamaze maana alishang’atuka! Wapo walioamwandika katika makala kuwa nchi ilimshinda, kwanini ajifanye kuwa mshauri wa hali ya uchumi, kisiasa na maendeleo. Hii ndio tabia ya binadamu wanapotofautiana.
Chuki yote dhidi ya Mwalimu ilisababishwa na kitabu chake cha Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania. Awali, kitabu hicho kilikuwa kichapwe hapa nchini, lakini wachapaji, ama waliogopa, au walizuiwa. Mwalimu akaamua kwenda kukichapisha nchini Zimbabwe. Kilipoletwa nchini kikauzwa kwa hadhari kama ‘nyara za Serikali’.

Mwalimu alichukiwa kwa sababu msimamo wake ulionekana kwa baadhi ya wana CCM kuwa ni usaliti, na hasa wakirejea kauli yake ya kwamba “CCM si mama yake”, kwa hiyo kuachana nayo halikuwa jambo la ajabu.
Basi, wakati hayo yakiendelea CCM, upande wa pili kukawa na vuguvugu kubwa la Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995. Mrema akawa Mrema. Akawavuta wengi. CCM, pamoja na jeuri yao, wakatafakari na kufikia uamuzi. Wakaandaa wanachama wenye kuheshimika. Wakapelekwa Butiama kuonana naye ili wamshawishi awasaidie kwenye ‘mapambano’ dhidi ya Mrema.
Wakati fulani Mwalimu hakusita kusema kwa furaha kuwa Mrema amemsaidia kumrejeshea heshima ndani ya CCM. Alimaanisha kuwa kwa sababu ya Mrema, CCM waliona umuhimu wake; na kwa maana hiyo iliwabidi ‘wamwangukie’. Hapo ndipo wengi huamini bega haliwezi kukivuka kichwa.

Wengi wanatambua kazi kubwa na ngumu iliyofanywa na Mwalimu wakati wa kumpitisha na kumnadi mgombea wa CCM, Benjamin Mkapa. Baadhi ya maeneo Mwalimu alipopolewa mawe akiwa jukwaani kumnadi mgombea huyo. Baadhi ya maeneo hayo ni Moshi na Tarime. Fikiria, pamoja na heshima na kupendwa kwake kote, bado wapo waliompinga Mwalimu, si kwa maneno tu, bali kwa kumpopoa mawe! Mara kadhaa alikasirika na kuwaambia: “Mtake msitake, huyu ndiye rais wenu [akinyoosha kipeperushi chenye picha ya Mkapa].
Lakini ikumbukwe kuwa kabla ya hapo, Serikali ilitumia nguvu kubwa sana kumdhibiti Mrema. Mabomu ya kutoa machozi yalitumika kuwatawanya wafuasi wake. Farasi, mbwa na hata wakati mwingine risasi za moto vilitumika kuwatawanya wafuasi wake.

Mwalimu aliiona mbinu hiyo ya Serikali [ambayo bila shaka yalikuwa maagizo ya CCM], ni ya hatari na ilikuwa ikimsaidia Mrema zaidi badala ya kumpunguza makali kisiasa.
Ndipo Mwalimu akasema alimradi wabebaji wapo, hakuna sababu ya kuzuia Mrema asibebwe. Akasema hata wakitaka kupokezana kama jeneza, waachwe tu. Hakuna ubaya.
Bahati nzuri vyombo vya dola [nadhani kwa maelekezo ya CCM], vikatii ushauri wa Mwalimu. Kuanzia hapo mabomu ya machozi yakapungua. Wafuasi wake wakambeba huku wakiimba kwa furaha. Punde, ule ‘moto’ wa ushabiki ukapungua.

Nimejaribu kuirejea historia hii kwa ufupi baada ya kuona kinachoendelea sasa. Yapo malalamiko kuwa vyombo vya dola vinakandamiza demokrasia. Vyama vya upinzani vinalalamika kutopewa fursa ya kushiriki siasa.
Polisi wanapovunja au kuzuia mikusanyiko ya wanasiasa, hasa wa vyama vya upinzani – wanarejea msimamo wa Rais John Magufuli, kwamba uchaguzi mkuu ulishapita, sasa apewe fursa kwa yeye na Serikali anayoiongoza watekeleze waliyowaahidi wananchi kupitia Ilani ya Uchaguzi ya chama chake.
Kwa upande wao, wanasiasa wa vyama vya upinzani hawaafiki msimamo huo. Wanasema kwao siasa ndio shughuli yao, na kwamba mwisho wa uchaguzi ndio mwanzo wa uchaguzi mwingine. Wanajenga hoja kuwa muda huu ndio wa kujijenga ili mwaka 2020 waweze kutoana jasho na CCM.

Kila upande unajitahidi kujenga hoja sasa na kwa maana hiyo waamuzi ni wananchi wenyewe. Jambo moja ambalo liko wazi ni kuwa hatuwezi kuwa nchi ya mikutano, maandamano na siasa kwa siku saba, miezi 12, wiki 52 kwa miaka mitano. Tunahitaji muda wa kujikita kwenye shughuli za kimaendeleo.
Kweli kuna mambo ambayo wananchi wanaamini Rais Magufuli, hayapendi. Yapo mambo yanayotolewa uamuzi wakatambua ‘kuna mkono wake’. Lakini ni ukweli kuwa yapo mambo yanayofanywa na wasaidizi wake au vyombo vya dola bila yeye kuwatuma. Tumeona mifano kadhaa ya uamuzi uliotolewa na mawaziri au watendaji fulani, lakini baadaye Rais akayapangua. Hii inasaidia kutufanya tuamini kuwa si kila linalotendwa na polisi au vyombo vya dola, lina maagizo ya Rais. Mimi si msemaji wa Ikulu, lakini utashi wa kawaida unanifanya niamini hivyo. Lakini wapo wanaohoji, kama hawatumi, mbona hawazuii? Ndio maana wananchi tunaozungumza nao mitaani wanatutuma tumweleze- kupitia kwenye maandishi yetu- kuwa hii kamata-kamata inapaswa ifanywe pale tu inapobidi.
Napata wakati mgumu kuamini kama kweli hii kamata-kamata inayoendelea nchini ni maagizo ya Rais Magufuli. Kamata-kamata nyingine zina taswira ya amri zinazotolewa na watu ambao, ama wanataka kuonyesha wapo kazini, au wana nia ya kuchafua taswira ya Serikali.

Kumekuwapo kamata-kamata ya wanasiasa. Kuna kamata-kamata ya watu walio kwenye mitandao ya kijamii, na kadhalika.
Wakati mwingine natafakari sababu zinazotolewa kabla au baada ya kuwakamata watuhumiwa, nashindwa kuona hatari inayovilazimu vyombo vya dola kutumia nguvu na rasilimali nyingi kwenye kamata-kamata hii. Hapa naweza kujitetea kwa uthibitisho wa kesi zinazofikishwa mahakamani. Mara nyingi kesi zinazowakabili watuhumiwa hawa zimekwisha kwa upande wa walalamikaji (dola) kushindwa.
Kusema hivyo si kwamba naunga mkono watu wanaohatarisha usalama wa nchi wasikamatwe, la hasha! Hoja yangu ni kuwa hadi mtu au watu wakamatwe, basi kuwe na sababu ya kweli yenye mashiko ya kuchukua hatua hiyo. Watu wasikamatwe tu kama fasheni au mashindano ya ma-RPC. Inapotokea kiongozi wa kisiasa, wa kidini au mwananchi yeyote akahamasisha uvunjifu wa amani kupitia tofauti zetu za kiitikadi, kidini, kikabila, kanda, jinsi au vyovyote vile, huyo au hao wanapaswa kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria. Wajibu wa dola ni kulinda usalama wa nchi na wananchi.

Utaratibu wa kamata-kamata kwa kila anayeonyesha mtazamo tofauti na viongozi walio madarakani hauisadii Serikali, bali unawasaidia hao wanaokamatwa.
Hapa ni vizuri ikajulikana kuwa ajenda nyingi zilizotikisa nchi, sasa hazipo; au kama zipo, basi hazina nguvu. Ajenda za ufisadi, ujangili, uporaji rasilimali za nchi, uzembe kazini, rushwa, uonevu na nyingine nyingi, sasa zinashughulikiwa kwa nguvu zote. Kwa miaka mingi hizi zimekuwa ajenda za wanachama na viongozi wa vyama vya upinzani na hata ndani ya CCM wenyewe.
Katika mabadiliko haya makubwa, watu wa vyombo vya ulinzi na usalama wasipokuwa na uvumilivu kwa baadhi ya mambo wanaweza kujikuta wanahama kwenye mada hizi na kuishia kwenye taarifa za kila siku za kukamata huyu au kukamata yule.

Watanzania wanahitaji maendeleo. Wanataka kushirikishwa kuondoa kero zinazowakabili. Wanahitaji kupata huduma za kijamii zilizo bora. Mwitikio kwenye ulipaji kodi ya majengo ni ishara ya wazi kuwa wananchi wanataka maendeleo.
Si jambo la faida kuona kuwa badala ya kuhangaikia masuala haya makubwa, yakiwamo ya ulinzi wa rasilimali za nchi, sasa tunageuka kuwa wasomaji na wasikilizaji wa nani amekamatwa, au nani atakamatwa.
Kama nilivyosema, yapo mambo ambayo kwa kweli yakitendwa na mtu, vyombo vya dola vikimkamata hata wananchi wenyewe wataunga mkono. Lakini haya mengine ya kuwakamata hata wale wanaokosoa tu mambo ya kawaida, hayaisaidii Serikali. Yanaiumiza. Yanajenga hofu na chuki visivyo vya lazima.

Rais Magufuli, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, mawaziri na watendaji wakuu wengine serikalini wanatambua kuwa hawawezi kupendwa na watu wote. Wanajua wapo waliokwenda mbali hata kuwatukana mitume na manabii. Wanajua pamoja na kazi kubwa ya uumbaji, wapo wasioamini kama Mungu yupo. Unaweza kujiuliza, kama Mungu, mitume na manabii wana wapinzani, seuze binadamu?
Waasisi wa Taifa letu wamefanya kazi kubwa sana ya kulijenga Taifa letu. Wapo Watanzania wapo wasiowakubali. Kama imekuwa hivyo kwa hao, hawa wa sasa wasione shida kuandamwa. Muhimu ni kuchapakazi tu. Baada ya miaka mitano hawatahukumiwa kwa namna walivyowakamata wanaowakosoa, bali kwa walivyotekeleza ahadi zao.

Hapa naomba ieleweke kuwa siungi mkono matusi au dharau kwa viongozi wetu wakuu. Rais wa nchi sharti aheshimiwe. Kumkosoa si kosa hata kidogo. Kinachogomba ni lugha inayotumika kumkosoa. Mkosoaji anaweza kuwa na hoja nzuri sana, lakini uwasilishaji wa huo ukosoaji unaweza kupoteza maana nzima na ukosoaji wake ukapuuzwa. Tumkosoe Rais kwa staha.
Mwisho, niombe haya mambo yafuatayo; kamata-kamata hii isiwe kama santuri. Watu wakamatwe kwa tuhuma zenye ushawishi hata kwa wananchi. Vyombo vya ulinzi na usalama visikurupuke tu kuwashika watu wanaokuwa na mtazamo tofauti, hasa kama mtazamo huo hauashirii au hauhamasishi uvunjifu wa amani.

Polisi wajiepushe kuonekana wanatumwa na Rais Magufuli kufanya wanayofanya sasa. Wasimjengee mazingira ya lawama asizostahili. Yanamwumiza. Hatuna magereza ya kutosha kuwafunga wakosoaji, hasa hawa wa kwenye whatsapp, facebook, twitter nk. Mambo mengine ni ya kupuuza, na kwa kufanya hivyo Serikali na watendaji watatumia muda mrefu kuhangaikia masuala ya maendeleo badala ya kila siku ‘nani kamatwa’. Hii kamata-kamata ni kuwapa watu umaarufu ambao pengine hawaustahili. Busara ya Mwalimu aliyoitumia kwa Mrema huu ndio wakati wa kuitumia. Tujifunze kutokana na historia.

Na Manyerere Jackton
Simu: 0759 488 955
Email: [email protected]